USHAHIDI uliowasilishwa katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, na Mbunge Halima Mdee, kuthibitisha tuhuma dhidi ya Yusuf Makamba kwamba amekuwa akimlinda Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa, katika tuhuma za ufisadi ikiwamo ugawaji viwanja eneo la Kawe, Dar es Salaam, msingi wake ni mpasuko wa madiwani wasioridhishwa na mwenendo wa meya huyo, Raia Mwema imebaini.
Imebainika kuwa, madiwani hao waliwahi kumwandikia barua Katibu wa CCM, Wilaya ya Kinondoni na nakala yake kufikishwa kwa Katibu Mkuu wa CCM- Taifa, Yusuf Makamba. Barua hiyo ni yenye kumbukumbu namba MAD/MK/01/08, ya Januari 24, mwaka 2008, inatoa ufafanuzi wa tuhuma za ubadhirifu na uongozi mbovu wa Manispaa ya Kinondoni, ikierejea barua ya awali, yenye kumbukumbu namba MAD/MK/01/08.
Inaelezwa kuwa baada ya madiwani kuchoshwa na kile kinachoelezwa kuwa ni "kumlinda" Meya Londa kwa gharama za walipa kodi wa manispaa, barua hiyo ambayo Raia Mwema imepata nakala yake, iliainisha tuhuma 10 dhidi ya Londa na kuhitimishwa kwa maelezo makali: "Kwa haya machache yanathibitisha kwamba Mstahiki Londa ameshindwa kusimamia utawala bora ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni."
Barua hiyo pia inaeleza ari ya madiwani hao kutaka kuitwa kwa Katibu wa CCM - wilaya na ngazi ya taifa ili kueleza kwa kina madhambi ya Londa ikisema; "Mheshimiwa Katibu utambue kuwa tunayo ya kuzungumza katika kikao ambacho chama mtatuita, lakini kwa haya machache yanathibitisha nani mbabaishaji."
Miongoni mwa tuhuma zilizoelezwa katika barua hiyo ni kuhusu kile kilichoelezwa kuwa; "Madiwani kugundua Halmshauri ya Manispaa ya Kinondoni imegubikwa na wizi wa mali unaotokana na vitendo vya kughushi nyaraka za malipo (payment vouchers).
"Juni, 2007, kwenye kikao cha bajeti tulipitisha kasma (fungu) ya kununua matrela 25 ya kubebea taka kwa thamani ya Sh milioni nane, kila moja baada ya zabuni kutangazwa na mshindi kupatikana. Lakini watendaji wa manispaa wakiwa na baraka za Mstahiki Londa walighushi nyaraka na kuongeza bei kutoka milioni nane hadi milioni 12. Matrekta hayo yakaagizwa tena kwa Sh milioni 15.5.
"Katika kikao cha kamati ya madiwani ya chama (CCM) Januari 7, mwaka 2008, Londa alitetea malipo hayo akidai walipwaji walisahau kuweka Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) walipowasilisha zabuni yao. Swali la kujiuliza hapa ni je, tangu lini VAT ikawa asilimia 50?''
Tuhuma nyingine inahusu ununuzi wa magari, ikidaiwa kuwa magari 15 aina ya Suzuki yalinunuliwa bila kuzingatia taratibu za ununuzi zinazotaka zabuni itangazwe kwanza na kuwa na profoma zaidi ya tatu.
Sehemu nyingine ya tuhuma katika barua hiyo inahusu uuzaji wa mali chakavu ya Manispaa ya Kinondoni na barua hiyo inaeleza; ''Mstahiki Londa aliamuru gari alilokuwa akitumia aina ya Toyota Land Cruiser GX ambalo lilikuwa kwenye orodha ya kupigwa mnada, likarabatiwe kwa kiwango cha juu kwa fedha za Manispaa na matengenezo yaligharimu Sh milioni 9, baada ya matengenezo hayo alilazimisha auziwe gari hilo kwa sh milioni 3.
''Ingawa ameshindwa kununua gari hilo baada ya madiwani kuja juu na kuzima njama zake, ameitia hasara Manispaa ya Kinondoni ya kiwango hicho cha pesa (sh milioni 9) wakati akijua mali chakavu zinazotakiwa kuuzwa hazistahili kukarabatiwa upya kwa fedha za umma''.
Kuhusu mgogoro wa kiwanja namba 695 na 696 ambao ndio umemhusisha Makamba baada ya Mbunge Mdee kudai kuwa amekuwa akimlinda Meya Londa tangu akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, madiwani hao wanasema; ''Mgogoro huu ulijitokeza katika eneo hilo ambalo liliuzwa na Mstahiki Salum Londa kwa Ishik, ilibainika kuwa kiwanja hicho ambacho kimemegwa na kupewa Ishik kilikuwa mali ya Manispaa ya Kinondoni.
''Ishik ilibidi alipe kwa kujenga madarasa kwa kulipa fidia hiyo kwa Manispaa, lakini zimekuwapo taarifa chafu zinazohusisha mchezo mchafu katika kummegea Ishik kiwanja hicho mali ya Manispaa, mchezo unaomhusisha Londa moja kwa moja''.
Mwishoni mwa mkutano uliopita wa Bunge, Spika Samuel Sitta alitoa uamuzi unaomtaka Mbunge Halima Mdee kutomwomba radhi Makamba na Londa kwa matamshi yake yanayoashiria kuwa wamekuwa wakilinda na kushirikiana kwenye mchezo mchafu wa utoaji viwanja namba 695 na 696.
Kwa mujibu wa madiwani wa Manispaa ya Kinondoni, wengi wao wameonyesha kufurahia 'hukumu' hiyo wakibainisha kuwa imewasilisha kilio na malalamiko yao ya muda mrefu.
Katika madai yake, Mdee alidai kuwa Makamba akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alimlinda Mstahiki Meya Salum Londa kwenye sakata la uuzaji wa viwanja namba 695 na 696 vilivyopo eneo la Kawe Ukwamani.
Alidai kuwa Yusuf Makamba, ambaye kwa sasa ni Mbunge na Katibu Mkuu wa CCM na Mstahiki Meya Salum Londa walishiriki kwenye vitendo vya kuhusiana na uuzaji wa viwanja hivyo na watendaji wa halmashauri walihamasishwa ili kuficha ukweli wa mambo hayo.
Kutokana na madai hayo, Makamba na Londa waliwasilisha malalamiko kwa Spika licha ya kukanusha wakitaka Spika achukue hatua ili Halima Mdee athibitishe madai yake.
Alisema Spika kuhusu suala hilo : '' Malalamiko yalipelekwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Desemba 31, 2008, kabla ya kamati haijaanza kazi ya kusikiliza shauri hili, nilipokea barua kutoka kwa Makamba akiomba kuyaondoa malalamiko yake na kutoa sababu kuwa amekwisha kuyasahau machungu aliyoyapata kutokana na kauli ya Mdee''.
Mara baada ya Makamba kutoa malalamiko yake, siku kadhaa baadaye Londa naye aliondoa malalamiko yake na hivyo Spika kuamua kuwa aliyelalamikiwa (Mdee) hana sababu ya kuomba radhi na matamshi yake yabaki kama alivyotamka ndani ya Bunge.
Habari za ndani ya CCM zinaeleza kwamba, Makamba na Londa walibaini mapema kwamba watabwagwa na Mdee katika kesi hiyo kutokana na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kuongozwa na Mbunge Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, ambaye amejijengea heshima kubwa kupambana na ufisadi.
Mbali ya kamati hiyo kuongozwa na Kilango, ushahidi ambao kina Makamba walibaini kuwa umewasilishwa katika kamati hiyo, ulikuwa na nguvu na hivyo kuamua kuondoa shauri hilo haraka kuepuka kudhalilishwa zaidi ikiwa kesi hiyo ingesikilizwa.
Wajumbe wengine wa Kamati ni Christopher ole Sendeka (CCM-Simanjiro), Ali Ameir Mohammed (CCM-Donge –Unguja), Abdulkarim Shaha (CCM-Mafia).
Wengine ni William Kusila (CCM-Bahi), Charles Keenja (CCM-Ubungo), Fatma Fereji (CUF-Baraza la Wawakilishi), Maulida Komu (Viti Maalum-CHADEMA) na Fatuma Maghimbi (CUF-Chakechake-Pemba).
Maamuzi yaliyotolewa na Bunge yameelezwa kulenga kurudisha imani ya wananchi kwa CCM, baada ya wana CCM wengi kusema kwamba chama hicho kitakuwa kinafanya mzaha mtupu kujieleza kwa umma kuwa kinapiga vita ufisadi wakati kivitendo inalinda mafisadi.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar