Senin, 07 September 2009

Mmiliki wa Chelsea Abramovich aelekea kileleni Kilimanjaro


MMILIKI wa klabu ya soka ya Chelsea inayoshiriki Ligi Kuu ya England, Roman Abramovich amefanikiwa kupanda Mlima Kilimanjaro na kesho anatarajiwa kufika kileleni.

Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya African Environment ambao ndio wanamsaidia tajiri huyo kupanda mlima huo, mteja wao leo anatarajia kufika eneo la barafu umbali wa mita 4,800 toka usawa wa bahari.

Mwongozaji wa kampuni hiyo aliiambia Mwananchi jana kuwa walikuwa katika eneo la Karanga umbalo lipo umbali wa mita 4,200 toka usawa wa bahari.

"Ni kwamba anapanda vizuri na amekuwa na juhudi kubwa na tuna imani atafika kileleni wa kuweka historia,"alisema mwongozaji huyo.

Hata hivyo, alisema katika mazungumzo yake anaonekana kufurahia kupanda mlima huo na kama akishawishiwa vizuri anaweza kuileta hapa nchini Chelsea ili kupanda mlima huo.

"Anafurahia sana kupanda mlima na alikuwa hajui kama anafahamika katikaTanzania, ameshangaa na hata kuona kuna mashabiki wa klabu,"alisema mwongozaji huyo.

Hata hivyo, katika upandaji mlima huo imekuwa ni vigumu billionea huyo kujichanganya na wasaidizi wake 115 ambao wanamsaidia yeye na wenzake watano kupanda mlima huo.

Tajiri huyo alianza kupanda mlima huo Septemba 3 kwa kupelekwa na helikopta maalum baada ya kutembelea viwanja vya farasi vilivyopo katika eneo la maji ya Chai, wilayani Arumeru

Amekuwa akisindikizwa na kikosi cha askari wa kampuni binafsi ya Warrior Security, walinzi wake na maafisa wa kampuni ya uwakala wa utalii ya African Environment.

Ziara hiyo imekuwa yenye ulinzi mkali huku walinzi wakiwaizuia picha kupigwa, Abromovich anapanda mlima huo akipitia njia ya Lemosho iliyopo eneo la West Kilimanjaro.

Bilionea huyo anatarajiwa kushuka mlima huo, Septemba 10 kupitia geti la Mwika ambapo anatarajiwa kupokelewa na kupewa cheti cha kupanda mlima huo ambapo tayari kuna taarifa mamia ya watu wakiwemo viongozi wa serikali, michezo na viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) watakuwepo.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar