2009-04-25 16:51:37
Mheshimiwa Andrew Chenge, mbunge wa CCM wa jimbo la Bariadi Magharibi, kidogo awatoe chozi waheshimiwa wenzake pale alipoamua kuweka wazi machungu aliyonayo moyoni kutokana na mikasa ambayo amekuwa akikumbana nayo.
Amesema mikasa yote hiyo anayoipata ni mitihani ya kidunia ambayo ameamua kumwachia Mwenyeji Mungu ambaye ndiye mweza wa yote.
Chenge hadi sasa anakabiliwa na kesi ya jinai ya kusababisha vifo vya wasichana wawili baada ya gari lake kuhusika na ajali iliyotokea hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.
Licha ya hilo la ajali, pia aliwahi kupakaziwa uchawi ambapo alidaiwa kunyunyizia unga kwenye viti ndani ya Bunge.
Kana kwamba hiyo haitoshi, mheshimiwa huyo pia anadaiwa kujilimbikizia mihela katika akaunti nje ya nchi, sakata lililomfanya apoteze nafasi ya uwaziri.
Chenge, aliyekuwa Waziri wa Miundo Mbinu, alilazimika kuachia ngazi baada ya kukumbwa na kashfa hiyo.
Chenge alipata nafasi hiyo ya kuwaeleza wabunge kilicho moyoni, wakati aliposimama Bungeni kutoa maoni ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi kuhusiana na muswada wa Bima ambapo kabla ya kuhitimisha, aliwashukuru wabunge na wananchi ambao walimtumia salam za kumpa pole.
``Nawashukuru wabunge na wananchi wote walionitumia salam za pole, ninachoweza kusema ni kwamba yote namwachia Mungu,`` akasema Mbunge.
Mheshimiwa huyo akamalizia kwa kusema kuwa amelazimika kusema hayo kwa vile hiyo ni mara yake ya kwanza kusimama mbele ya Bunge hilo tukufu baada ya kukuktana na mitihani mbalimbali ya kidunia.
Baada ya kumalizia kutoa shukrani hizo, Mwenyekiti wa Bunge, Mhesimiwa Job Ndugai alimpa pole na kuongeza kuwa wabunge wote wapo pamoja naye.
Muswada huo ulipita kwa taabu baada ya wabunge kuibana Serikali kuhusiana na vifungu mbalimbali ikiwemo kinachompa uhuru Kamishna wa Bima kutoa muda usio na kikomo kwa kampuni ya bima ambayo itashindwa kumlipa mteja.
Msemaji wa kambi ya upinzani, Mheshimiwa Abubakary Hamis Bakari alisema kifungu hicho hakina tofauti na kile cha awali na kwamba kitaendelea kumnyanyasa mteja.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Fedha na Mambo ya Uchumi, Mheshimiwa Omari Yusuf Mzee aliendelea kung\'ang\'ania kifungu hicho akisema hakina madhara, hali iliyozua mvutano mkali Bungeni.
Hali hiyo ilimfanya Mheshimiwa Chenge kusimama tena na kutoa ufafanuzi kuwa Kamishna anapaswa kutoa muda usioziodi siku 45 (ambao umeainishwa katika sheria) kwa kampuni itakayoshindwa kumlipa mteja wake.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika.
Kutokana na ufafanuzi huo, Naibu Waziri alikubali kifungu hicho kibadilishwe.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar