Mkutano wa mjini Sofia unalenga kutafuta njia za kuhakikisha usafirishaji wa kutosha wa gesi barani Ulaya kufuatia mzozo wa gesi kati ya Urusi na Ukraine. Mzozo huo ulisababisha kupungua kwa kiwango cha gesi kinachosafirishwa barani Ulaya katikati ya msimu wa baridi mnamo mwezi Januari mwaka huu.
Watumaiji wa gesi, nchi ambazo gesi inapitia na nchi zinazosafirisha gesi zimejadiliana kuhusu njia ya kupiga jeki mipango ya kupanua vyanzo na njia za gesi barani Ulaya. Lakini uamuzi wa dakika ya mwisho wa waziri mkuu wa Urusi, Vladamir Putin, kutohudhuria mkutano wa mjini Sofia, kumekwamisha mjadala kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la gesi litakalosafirisha gesi ya Urusi hadi barani Ulaya kupitia chini ya bahari ya nyeusi, Black Sea.
Pia kukosekana kwa waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, kwenye mazungumzo ya leo, kumetilia shaka mradi wa Umoja wa Ulaya wa ujenzi wa bomba la Nabucco, linalonuiwa kutumiwa kusafirishia gesi kutoka bahari ya Caspian hadi barani Ulaya kupitia nchini Uturuki, Bulgaria, Romania na Hungary bila kupitia nchini Urusi.
Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Wajumbe wa mkutano wa mjini Sofia wamelalamika kwamba miradi hiyo inakwamishwa na tofauti za kisiasa na kukosekana makubaliano juu ya udhamini na ugavi wa gesi. Wamewataka wahusika wakuu, hususan Umoja wa Ulaya, kutoa fedha zinazohitajika ili miradi hiyo iweze kuendelea kwa haraka.
Uturuki hivi karibuni imekosolewa kwa kulitumia bomba la Nabucco ili kuushika mateka Umoja wa Ulaya ikiutaka ulikubali ombi lake la kuwa mwanachama wa umoja huo kama fidia. Imeshutumiwa pia kwa kujaribu kuwa msafirishaji wa gesi barani Ulaya kwa kununua gesi kutoka nchini Azerbaijan na kuiuza tena kwa Umoja wa Ulaya.
Urusi imeongeza juhudi zake kuishawishi Azerbaijan kwa kuiahidi kununua kiwango kikubwa cha gesi yake. Mabomba ya Nabucco na bomba litakalopitia bahari nyeusi yatategemea gesi kutoka Mashariki ya Kati na eneo la Caspian. Urusi imekuwa kwa muda mrefu ikinunua gesi kutoka eneo hilo na kuiuza, lakini hakuna nchi hata moja kutoka muungano wa zamani wa Sovieti inayoiuzia gesi Urusi, iliyowahi kuuza gesi yake moja kwa moja barani Ulaya.
Mkurugenzi wa kampuni ya kusafirisha gesi ya Nabucco, Reinhard Mitschek, amesema ana matumaini kwamba licha ya waziri mkuu wa Uturuki kukosekana kwenye mkutano wa mjini Sofia, mazungumzo na Uturuki ni muhimu kwani yatasaidia kufikia hatua ya kusainiwa mkataba wa kimataifa kuhusu bomba la Nabucco kufikia mwezi Juni mwaka huu.
Mkutano mwingine kuhusu gesi
Mkutano wa mjini Sofia unafanyika sambamba na mkutano mwingine kuhusu nishati unaoendelea mjini Ashgabat, mji mkuu wa Turkmenistan. Marekani hii leo imetolea mwito Turkmenistan kupanua masoko yake ya nishati huku ikiwa na matumaini ya kupunguza ushawishi mkubwa wa Urusi katika taifa hilo la Asia ya Kati lenye utajiri mkubwa wa nishati.
George Albert Krol, naibu waziri wa mambo ya ndani wa Marekani
Akizungumza kwenye mkutano wa mjini Ashgabat, naibu waziri wa mambo ya ndani wa Marekani, George Krol, amesema ushirikiano na Turkmenistan na mataifa mengine ya Asia ya Kati umepewa kipaumbele katika ajenda ya rais wa Marekani, Barack Obama. "Tunaunga mkono kwa dhati masoko ya nishati na njia za usafishaji katika mataifa ya Asia ya Kati na kati ya eneo hili na masoko ya kimataifa." Krol ameupongeza utawala wa Turkmenistan na kuileza nchi hiyo kuwa mfano bora wa sera ya kimataifa ya ulinzi wa nishati.
Rais wa Turkmenistan, Gurbanguly Berdymukhamedov, ambaye ameanza kuielekeza nchi yake katika mataifa ya magharibi tangu kifo cha mtangulizi wake mnamo mwaka 2006, amevikaribisha vivutio vya mataifa ya magharibi.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar