Hatimaye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amekiri kwa niaba ya serikali kuwa kampuni ya TICTS imeshindwa kazi n a kuwa mkataba wake unaangaliwa upya. | ||||
HATIMAYE serikali sasa imeeleza bayana kuwa kampuni ya Ticts inayoendesha kitengo cha kupakua na kupakia makontena kwenye Bandari ya Dar es salaam imeshindwa kazi na sasa inapitia upya mkataba ulioipa kampuni hiyo haki peke.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema pia kuwa miongoni mwa mambo yanayofikiriwa ni kuufuta mkataba huo au kutafuta makampuni mengine na kuingia nayo mkataba wa kufanya kazi hiyo ili yaweke ushindani kwa Ticts na kuboresha huduma ya kitengo hicho kilichokuwa kiingizia Mamlaka ya Bandari (TPA) faida kubwa.
Waziri Pinda alitoa kauli hiyo jana Bungeni wakati akijibu swali la mbuge wa Tabora Mjini, Silaji Kaboyonga ambaye alitaka kujua serikali inafanya nini juu ya Ticts na kwanini isimalize mgogoro uliopo kwa manufaa ya taifa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo.
Pinda alisema kuwa anakerwa na huduma hiyo ambayo alisema kuwa
ni mbovu na haileti tija kwa Watanzania, ukilinganisha na huduma kama hiyo ambayo inatolewa katika nchi ya Ireland alikotembelea hivi karibuni.
“Unajua laizma tukubaliane kuwa tuliingia katika mkataba mbovu kabisa na watu Ticts ambao wanaonekana kuwa wameshindwa kabisa kutimiza majukumu yao kama tulivyotarajia hivyo mheshimiwa spika nalitaarifu bunge lako tukufu kuwa mkataba huo unapitiwa upya hivi sasa,” alisema Pinda.
Alisema kuwa bandarini kwa sasa hakuna ushindani kabisa ukilinganisha na bandari za nchi ningine ambazo zinakuwa na makumpuni zaidi ya tisa na kutoa mfano wa bandari ya Dublin iliyo nchini Ireland ambako alisema kuna makapuni mengi ambayo yanashindana kutoa huduma hiyo na hivyo kuongeza ufanisi.
Alisema katika kuangalia upya mkataba huo, ikionekana kuwa kuna umuhimu ni lazima kampuni hiyo ipelekwe mahakamani.
“Hapa suala halihitaji kuwa mwanasheria. Unaweza kuona kuwa kilichofanyika si sahihi hawa jamaa wamekiuka kanuni za mkataba hivyo naamini kuwa hata tukiwapeleka mahakamani bado serikali inaweza kushinda bila ya wasiwasi,” alisema Pinda.
Kiongozi huyo wa shughuli serikali bungeni alisema kuwa kama wataalamu wataona kuwa inafaa kuiachia kampuni hiyo iendelee na kazi yake kwa kipindi cha miaka 15 ijayo itakuwa ni vema, lakini akatahadharisha kuwa ni laizma kutakuwa na hasara kubwa mno.
Pamoja na kuupitia mkataba huo, Pinda pia alitaka miundombinu ya bandarini iboreshwe na kuweka mazingira kwa makampuni mengi zaidi ya kufanya kazi hiyo badala ya kutegemea kampuni moja ambayo inaonekana
kushindwa kufanya kazi yake.
Katika taarifa yake, mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Kabwe Zuberi Zitto alipendekeza kuangaliwa upya kwa mkataba huo na Waziri Pinda aliipongeza kamati hiyo kwa ufanisi mzuri katika kazi hiyo.
Ticts (Tanzania International Container Terminal Services), ambayo inamilikiwa kwa asilimia 75 na kampuni ya nje ya ICTS huku asilimia 25 zikimilikiwa na kampuni ya Vertex ya Tanzania, ilianzishwa baada ya ICTS kushinda zabuni ya mkataba wa miaka 10 wa kutoa huduma hiyo kwenye Bandari ya Dar es salaam mwaka 2000.
Ilikuwa ni miezi michache baada ya Ticts kuundwa Aprili mwaka 2000 kabla ya kushinda zabuni hiyo, na miaka mitano baada ya kufanya kazi hiyo, Ticts iliongezwa na kuwa wa miaka 25 kwa madai kuwa maagizo hayo yalitoka Ikulu.
Hata hivyo, Aprili 25 mwaka jana, Bunge lilipitisha uamuzi wa kuitaka serikali isitishe mkataba huo wa nyongeza ya miaka 15 katika mkataba wa awali wa miaka 10, kwa maelezo kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Manunuzi ya Umma wakati wa uongezaji wa mkataba huo, jambo lililotafsiriwa kuwa kulikuwa na mazingira ya rushwa.
Pia ilidaiwa kuwa mkataba huo uliongezwa wakati hali ya utendaji wa Ticts ikizidi kuwa mbovu na hivyo kudhihirisha kuwa kulikuwa na mazingira ya rushwa.
Kwa wakati wote huduma katika kitengo hicho cha upakuaji na upakiaji makontena kwenye Bandari ya Dar es salaam zimekuwa zikilalamikiwa sana licha ya hatua kadhaa kuchukuliwa kujaribu kurekebisha hali hiyo.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar