Minggu, 12 Juli 2009

Dondoo za hotuba ya Rais Obama


Rais Barack Obama ametoa hotuba yake ya kwanza iliyolenga hasa bara Afrika huku akisisitiza umuhimu wa bara hili kwa ulimwengu mzima, utawala bora na akaangazia pia changamoto zinazotokana na migogoro pamoja na ufisadi.
Umuhimu wa Afrika
Sioni tofauti kubwa kati ya nchi na watu wa Afrika. Naitizama Afrika kama sehemu muhimu ya dunia. Naitizama kama mshirika wa Marekani hasa kwa kuzingatia mustakabali wa maisha ambayo tungependa kuwarithisha watoto wetu.
Ukoloni na wajibu
Ni rahisi mno kunyoosha kidole na kuwalaumu watu wengine kwa matatizo ya Afrika. Naam, ni dhahiri kwamba mipaka iliyowekwa na wakoloni ilibuni mizozo, na kila mara nchi zilizostawi hujiona kuwa mlezi na sio mshirika wa Afrika.
Lakini huwezi kulaumu nchi za Magharibi kwa uharibifu wa uchumi wa Zimbabwe katika mwongo uliopita au kuzilaumu kwa vita ambapo hata watoto husajiliwa kama wapiganaji.
Nyakati zile za babangu, matatizo yaliyokuwa yakiikabili Kenya baada ya kupata uhuru yalikuwa kwa kiasi ukabila au unayemjua mamlakani. Ni matatizo kama haya ambayo yaliparaganya amali yake na tunafahamu vyema kwamba imekuwa kawaida kwa watu wengi kukabiliana na aina hii ya ufisadi.
Utawala
Maendeleo yanategemea utawala bora. Huo ndio mhimili ambao unakosa katika sehemu mbalimbali na kwa muda mrefu. Hayo ndiyo mabadiliko ambayo yanaweza kuimarisha Afrika. Na hilo ni jukumu la Waafrika wenyewe.
Ufisadi
Ukandamizaji unatekelezwa kwa njia tofauti tofauti. Nchi nyingi zinakumbana na matatizo ambayo yametumbukiza wananchi wao katika umaskini.
Hakuna nchi yoyote ambayo itaweza kupata ufanisi ikiwa kiongozi wake anajilimbikizia mali ya umma au polisi wanapokula rushwa kutoka kwa wauzaji wa mihadarati.
Hakuna yeyote ambaye angependa kuishi katika nchi ambayo haizingatii utawala wa sheria, badala yake inatawaliwa kinyama na ufisadi.
Hiyo siyo demokrasia, ni udhalimu. Wakati umefika wakukomesha utawala kama huo. Afrika haihitaji wababe bali taasisi imara za utawala.


Msaada
Ingawa Waafrika wanatarajia kupata msaada, Marekani itatoa msaada wake kwa njia ya kuwajibika.
Tutapunguza malipo yanayotolewa kwa wataalamu na usimamizi wa miradi ili kiasi kikubwa cha msaada wetu kiwafikie walengwa na kutoa mafunzo ya kuwahamasisha watu kujitegemea.
Kwa sababu hiyo tumetoa dola za Marekani bilioni 3.5 kwa mpango wa kuhakikisha kuna chakula cha kutosha kwa kuzingatia njia mpya za uzalishaji na teknolojia kwa wakulima.
Sio tu kuuza bidhaa za Marekani barani Afrika. Msaada sio jawabu kwa matatizo.
Umuhimu wa msaada wa kutoka nje ni kubuni mazingira ambayo yataondoa mazoea ya kutegemea msaada.
Afya
Madaktari na wauguzi wengi kutoka Afrika wanavutiwa na mazingira mazuri ya kufanya kazi katika nchi zilizostawi. Wao huamua kwenda ng’ambo au kushughulikia aina moja tu ya maradhi.
Hali hii husababisha ukosefu wa huduma za kutoa afya ya msingi na kinga dhidi ya maradhi.
Hata hivyo, kila Mwaafrika ana wajibu wa kusaidia katika kuzuia maambukizo ya ugonjwa na kukuza afya bora katika jamii na nchi zao.
Migogoro
Hebu nikariri hili. Afrika sio kikaragosi cha bara lililoghubikwa na vita. Lakini kwa Waafrika wengi maisha ya vita yamekuwa ya kawaida.
Kuna mizozo kuhusu ardhi na rasilmali. Inashangaza kwamba bado kuna wale wenye dhamira mbaya ya kuwachochea kabila zima kupigana.Migogoro hii ni mzigo mkubwa ambao umeibana Afrika.
Sota tuna njia nyingi za kujitambulisha kama vile kabila na ukoo, dini au uraia. Lakini mtindo huu wa kujitambulisha kwa misingi hii haina nafasi katika karne hii ya 21.
Yafaa anuwai ya Afrika iwe chanzo cha nguzo na sio migawanyiko.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar