Sabtu, 27 Desember 2008

Mbunge: Hatutaki kumuonea Mkapa

• Asema wanataka kujua undani wa Kiwira

na Christopher Nyenyembe, Rungwe




MBUNGE wa Mpanda Kati, Arfi Amour (CHADEMA), amesema chama hicho hakitaki kumuonea Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kuhusu madai ya kumiliki mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya isipokuwa kinataka kujua aliupataje.

Alisema kamwe CHADEMA haimwandami Mkapa bila sababu, bali kinaitaka serikali iwaambie Watanzania nani aliyeuziwa mgodi huo, kwa kuwa mikataba yote ya serikali hasa upande wa madini ni michafu.

Akihutubia katika uwanja wa Tandale, wilayani Rungwe, katika ziara ya Operesheni Sangara juzi, mbunge huyo alisema utaratibu uliofanyika wa kuuza mgodi wa Kiwira ni wa usiri mkubwa kwa kuwa mkataba wake haupo wazi na serikali inajua iliyemuuzia.

“Mikataba yote ni batili, ni michafu ina asilimia 10 ya viongozi wa serikali ndiyo maana inakuwa siri. Hata wabunge hawatakiwi wala kuruhusiwa kuipitia na hii ni hatari katika uchumi wa nchi,” alisema.

Alisema katiba ya nchi ndiyo tatizo kubwa kwa marais wastaafu waliojihusisha na tuhuma za ubadhirifu kwa kuwapa kinga iliyoandikwa mwaka 1977 na wana CCM wachache na haikuweza kuthibitishwa na Bunge licha ya kufanyiwa marekebisho mara 14.

“Ili Rais mstaafu Mkapa aweze kushitakiwa lazima katiba ifanyiwe marekebisho na kuridhiwa na Bunge ndipo anaweza kufikishwa mahakamani, lakini kinga aliyonayo kwetu ni kikwazo kikubwa,” alisema mbunge huyo.

Pia alisema madai ya wapinzani kuhusu mkataba wa Kiwira hakulengi kumdhalilisha mtu isipokuwa lazima serikali iweke wazi ni kiasi gani mgodi huo umeuzwa.

Aidha, alisema ucheleweshaji wa mabadiliko ya katiba kunachangiwa na idadi ndogo ya wabunge wa upinzani waliopo bungeni ambao ni 44 huku wabunge wa CCM wapo 279 kati ya wabunge wote 323 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aliwataka wananchi kuhakikisha katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 wanachagua idadi kubwa ya wabunge wa upinzani, ili kuleta ushindani wa kutosha ambao utalenga kuboresha masilahi ya wananchi wote na si kuneemesha kundi dogo la watu wachache.

Naye Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya, George Mtasha, alisema kazi kubwa iliyopo sasa kupitia Operesheni Sangara ni kuwaeleza wananchi uoza wote na ufisadi uliofanywa na serikali ya CCM.

Mtasha alisema umefika wakati ambao wananchi wanapaswa kusimama imara, kuacha woga na kutambua kuwa bila ujasiri hawawezi kushinda nguvu za kifisadi ambazo zimechangia idadi kubwa ya wananchi kuwa maskini.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar