UFUMBUZI wa mvutano wa uchimbaji wa nishati ya mafuta na gesi asilia visiwani Zanzibar uko katika hatua za mwisho baada ya mshauri mwelekezi kutoka kampuni ya Aupec LTD ya Uingereza kuwasilisha taarifa ya mapendekezo ya namna ya kugawana raslimali hiyo kwa serikali ya Muungano na ya Mapinduzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana juu ya mafaniko na changamoto kwa wizara yake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia mambo ya Muungano, Mohamed Seif Khatib alisema taarifa ya mshauri huyo kwa sasa iko katika hatua nzuri ya utekelezaji wa mapendekezo.
"Baada ya kugombana kwa muda mrefu kuhusu uchimbaji wa nishati hiyo, serikali ilimtafuta mshauri mwelekezi kwa lengo la kutushauri namna ya kugawana raslimali hiyo na kwa sasa tayari amekwishawasilisha taarifa rasmi ya mapendekezo katika serikali zote mbili namna ya kugawana raslimali hiyo," alisema Khatib.
Alisema gharama za kumlipa mshauri huyo zimelipwa na serikali zote mbili yaani serikali ya muungano na serikali ya mapinduzi.
Mbali na taarifa hiyo ya mafuta na gesi asilia, Waziri Khatib alisema serikali zote mbili zimeona umuhimu wa kuratibu shughuli za uvuvi kwa kuunda chombo maalum kwa lengo kuweka utaratibu wa kugawana mapato yanayotokana na uvuvi kwa ajili ya kuzinufaisha serikali zote mbili.
Alisema sheria ya Mamlaka ya Uvuvi katika ukanda wa Bahari Kuu imeainisha mgawanyo wa mapato yanayotokana na shughuli za uvuvi, ikieleza kuwa asilimia 50 hutumika kwa shughuli za uendeshaji wa mamlaka hiyo, wakati Serikali ya Muungano hupata 30 asilimia na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hupata asilimia 20.
Akizungumzia nafasi ya Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Waziri Khatibu alisema ili kufaidi matunda ya ushirikiano huo kwa sasa Zanziba itakuwa na sehemu yake inayotegemea tofauti na awali ilipokuwa ikishiriki kupitia Serikali ya Muungano.
"Kwa sasa Zanzibar imeingiza miradi yake nane ya maendeleo katika umoja huo ambayo utekelezaji wake utaiwezesha kunufaika moja kwa moja na ushirikiano huo," alisema Waziri Khatib.
Pia Waziri Khatib alizungumzia manufaa ya misaada ya kiuchumi na ya maendeleo inayotolewa na wafadhili kwa Serikali ya Muungano akisema umewekwa utaratibu wa kuhakikisha kwamba Zanzibar nayo inapata mgawo wake.
Alitaja mafaniko mengine ya wizara yake kuwa ni kuundwa kwa Tume ya Fedha ya pamoja kwa lengo la kuhakikisha kwamba Zanzibar inachangia na kunufaika na mapato ya taifa.
Alisema tume hiyo imetoa mapendekezo ya namna ya serikali zote zitakavyochangia uendeshaji wa shuguli za Muungano.
Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja malumbano baina ya viongozi wa serikali zote kwa kutumia vyombo vya habari badala ya kutumia vikao kutatua tofauti zinazojitokeza, akisema jambo hilo linawachanganya wananchi.
Akizungumzia muundo wa Muungano, Waziri Khatib alisisitiza kwamba mfumo wa sasa ndio unaofaa kwa kuwa mekubaliwa na wananchi wengi kwa mujibu wa taarifa ya maoni ya Kamati ya Jaji Kisanga.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar