WAKATI Serikali ikitoa masharti magumu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kurejea vyuoni baada ya kugomea Sera ya Uchangiaji Elimu, uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi umeonyesha kuwa migomo na maandamano ya wanafunzi hao hayana uhusiano wowote na siasa.
Vyuo saba vya serikali vimefungwa baada ya wanafunzi kugoma kuingia madarasani wakidai wakiishinikiza serikali kufuta sera ya uchangiaji elimu ambayo wanadai kuwa ina ubaguzi katika utoaji wa mikopo na pia kutaka wpte wapewe mikopo kwa asilimia 100 bila ya kubagua iwapo sera hiyo itaendelea.
Migomo hiyo iliyotapakaa kwa kasi kwenye vyuo hivyo vya serikali ilisababisha baadhi ya menejimenti za vyuo hivyo kudai kuwa kuna vyama vinavyofadhili wanafunzi ili waitingishe serikali.
Lakini matokeo hayo ya awali ya uchunguzi wa polisi yanakata nguvu za menejimenti za vyuo vya elimu ya juu.
Kwa mujibu wa habari za kuaminika kutoka kwa timu hiyo ya polisi inayochunguza migomo na maandamano hayo, tatizo kubwa linalochochea migomo vyuoni ni menejimenti.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu matokeo ya uchunguzi huo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba alisema uchunguzi wa polisi bado unaendelea.
Kamishna Manumba alipouilizwa zaidi nini hasa kimebainika katika uchunguzi wa awali, alisisitiza, "Uchunguzi wa polisi ni mpana."
DCI Manumba aliongeza kwamba katika uchunguzi huo si rahisi kuanza kutoa matokeo sasa kwani uchunguzi bado unaendelea lakini akakiri hadi sasa hawajabaini siasa katika migomo na maandamano ya wanafunzi.
"Unajua uchunguzi wa polisi ni mpana, kusema sasa hivi tumebaini nini si sahihi. Uchunguzi unaendelea," alijibu DCI Manumba kwa kifupi.
"Nafikiri tusubiri matokeo ya uchunguzi kamili, tusianze kutoa majibu ya uchunguzi ambao bado unaendelea. Matokeo yatajulikana tu baada ya muda wa uchunguzi kukamilika."
Wakati Kamishna Manumba akisema hayo, habari za kuaminika zinasema matatizo ambayo wanafunzi wamekuwa wakilalamikia ni pamoja na menejimenti mbovu za vyuo vikuu nchini.
Kwa mujibu wa matokeo hayo ya uchunguzi wa awali tatizo jingine lililobainika ni Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ambayo wanafunzi hawakubaliani nayo.
Matokeo hayo ya uchunguzi wa polisi yatakuwa pigo kwa menejimenti za vyuo vikuu nchini hasa vile vya serikali, ambavyo vimekuwa vikihisi matatizo ya wanafunzi yanatokana na siasa.
Naye Exuper Kachenje anaripoti kuwa wakati Jeshi la Polisi nchini likiashiria kuwa hakuna chama cha siasa kinachojihusisha kufadhili migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu, mwananchi mmoja amejitokeza na kulipia gharama za tangazo la nusu kurasa kwenye gazeti kueleza kuwa siasa ndio chanzo cha migomo hiyo.
Mwananchi huyo ambaye hata hivyo hakutaja jina lake alitoa barua ya wazi kwenda kwa Bodi ya Mikopo na Serikali kupitia gazeti hili toleo la jana ukurasa wa 18, iliyokuwa na kichwa kisemacho "Chanzo cha Migomo Vyuoni /Nini Kifanyike".
Mwananchi huyo aliyejitambulisha kama mfanyakazi wa serikali na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA) alisema viongozi wa wanafunzi wakishirikiana na viongozi wa vitivo wa kila kozi na wawakilishi wa wanafunzi wamekuwa wakiendesha vikao usiku wa manane na kwamba wana pesa kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo vyama vya siasa.
“Wale viongozi wa wanafunzi wakishirikiana na viongozi wa vitivo vya kila kozi na wawakilishi wa wanafunzi wamekuwa wakiendesha vikao mpaka usiku wa manane. Hawa lazima wanapesa toka sehemu mbalimbali na vyama vya siasa kama ilivyoelezwa kwenye vyombo vya habari,” alieleza
Aliongeza kuwa baada ya vikao hivyo viongozi hao wamekuwa wakiwalazimisha kutii maamuzi yao bila kufikiri na kueleza kuwa asiyetii atachapwa viboko, akiongeza kuwa asilimia 75 ya wanafunzi wa SUA hawakupenda migomo na kwamba aliyehamasisha watu wasiingie madarasani ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu na yupo chuoni hapo.
Ameishauri serikali kutokubali kuburuzwa na iwafukuze viongozi wote waliopo sasa pamoja na kubinafsisha vyuo vyote vya umma ili ibakie na jukumu la ukopeshaji na kuwaelimisha wanavyuo kuwa mkopo si msaada wala haki.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar