Sabtu, 10 Januari 2009

DHANA YA UFISADI INALETA MAAFA NCHINI....

Mkutano wa Lowassa wazua balaa Monduli

2009-01-10 12:13:37

Mkutano wa viongozi wa jadi wa kabila la Kimasai ulioitishwa na kiongozi wake aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, umezua balaa, baada ya mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Mkoa wa Arusha, James Milya, kurushiana makonde mazito hadharani.

Tukio hilo lilitokea jana baada ya mkutano huo wa viongozi wa jadi wa Kimasai kuahirishwa kwa muda kwa ajili ya chakula cha mchana.

Mkutano huo uliokuwa wa siku mbili ulimalizika jana, lakini kwa mujibu wa Ole Sendeka, Lowassa hakuwepo wakati tukio la purukushani hiyo lilipotokea.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Ole Sendeka alisema aliamua kujitetea baada ya Milya kumrushia konde ambalo alilikwepa.

Alisema kutokana na hali hiyo, aliamua kujitetea kwa kumrushia konde moja ambalo lilimpata hadi kuanguka chini.

Akizungumzia zaidi juu ya mkutano huo, Ole Sendeka alisema kwa ujumla haukuwa wa kisiasa na haukupangwa kwa lengo la kumhujumu.

Alisema wakati akichangia mada, katika mkutano huo uliokuwa na ajenda mbili, ya kuzungumzia elimu ya mtoto wa kike kwa jamii ya wafugaji na nyingine ya matatizo ya ardhi, baadaye Milya alichangia hoja hiyo akiwashutumu wanasiasa na hasa katika jimbo la Simanjiro kwamba ni mafisadi na wanafiki.

``Huyu bwana mdogo alinishambulia akidai kuwa sisi wanasiasa na hasa wa Simanjiro ni wanafiki na kwa nini hatuchukuliwi hatua.

Alitamka wazi ingawa hakutaja jina langu, lakini alisema `kama mchangiaji huyo aliyemaliza kuzungumza sasa hivi` akimaanisha jina lake (Sendeka),`` alisema.

Alisema baada ya kuahirishwa kwa muda kwa ajili ya kupata chakula, alimuuliza Milya kwa nini alimshambulia kiasi hicho naye akamjibu kwamba sasa ameanza vita.

Alisema bila kutegemea alirushiwa ngumi, ambayo hata hivyo, alifanikiwa kuikwepa.

``Katika kujitetea niliamua kumrushia ngumi moja ambayo ilimpata na akaanguka chini, nilichofanya ni kujitetea tu katika mazingira kama yale...`` alisema.

Lakini kwa upande wake Milya alisema hakumrushia ngumi, isipokuwa Ole Sendeka ndiye aliyempiga hadi akaanguka chini.

Alisema baada ya kuanguka Ole Sendeka alitaka kuendelea kumpiga, lakini wajumbe wa mkutano huo walimnusuru.

Hata hivyo alisema aliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi cha Monduli na kufungua jalada namba Monduli/RB/35/09.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar