Selasa, 16 Juni 2009

Mbunge Shibuda alishutumu baraza la Mawaziri kwa kubariki ufisadi


Ahoji uzalendo wao, asema nchi inapoteza dira,mwelekeo
Ramadhan Semtawa na Tausi Mbowe, Dodoma

HALI inazidi kuwa mbaya kwa Baraza la Mawaziri baada ya mbunge wa Maswa kwa tiketi ya CCM, John Shibuda kuliangukia tena akihoji uzalendo wake na kueleza kuwa mikataba yote mikubwa ya kifisadi imepitishwa kwa baraka za chombo hicho.

Kauli ya Shibuda, ambaye ameweka bayana nia yake ya kugombea urais mwakani, imetolewa siku moja baada ya mbunge wa Nzega, Lucas Selelii kulishushia tuhuma nzito kuwa limejaa watu wabinafsi, wasiowatakia mema wabunge wenzao na kumwomba Mungu awalaani.
Kama kawaida yake akitumia lafudhi ya Pwani, Shibuda alihoji ni kipimo gani kinaweza kutumika kupata tafsiri ya uzalendo kwa mawaziri wakati mambo hayaendi vizuri nchini?

Shibuda, ambaye alikuwa akizungumza kwa mfano na vielelezo huku akinukuu katiba, alisema mambo mengi ambayo yanaonekana kuvurugika nchini, ikiwemo mikataba mikubwa, mibovu na ya kifisadi imepitishwa na baraza la mawaziri.

“Iko wapi tafsiri ya uzalendo kwa mawaziri wetu, mambo mengi tunayaona makubwa, ikiwemo mikataba mibovu kwa nchi inapitishwa na baraza la mawaziri?” alihoji.

Mbunge huyo machachari, alifafanua kwamba, mikataba mikubwa mibovu kama ya madini yote ilipata baraka za baraza la mawaziri.

Alisema watu hawana budi kurejea katika Azimio la Arusha na TANU ambayo iliweka dira ya maendeleo ya wananchi na kujitegemea.

“Ukisoma katiba yetu inasema ni nchi ya ujamaa na kujitegemea, lakini hadi sasa hakuna misingi yoyote ya kujitegemea. Wananchi wa kawaida wanazidi kuwa maskini,” aliongeza.
Kuhusu bajeti na wakulima, alisema serikali imeshindwa kutumia mitaji iliyopo kwa kushindwa kuwekeza kwa wakulima wa pamba na sekta ya mifugo.

Alisema wafugaji na wakulima wangewekewa misingi mizuri, nchi ingeweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kuachana na utegemezi wa misaada ya nje ambayo ni ya mabepari ambao huleta unyonyaji.

Mbunge huyo machachari alisema ndiyo maana hadi sasa uchumi mkubwa umeshikwa na wageni na kuhoji: “Tulipigania uhuru ili iweje?”

Shibuda pia alizungumzia mradi wa vitambulisho vya taifa, akisema umefika wakati sasa mradi ukahamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kuwa hakuna maendeleo yoyote zaidi ya malumbano.

Alisema vitambulisho vya taifa ni muhimu kwani ungewezesha nchi kuwa na mfumo ambao ungetambua walipakodi kutoka sekta rasmi na isiyo rasmi.
Naye mbunge wa Kishapu (CCM), Fred Mpendazoe, alihoji watuhumiwa wa ufisadi wa kampuni ya Richmond Development (LLC) kuendelea kuwepo hadi sasa bila kuchukuliwa hatua huku wakizidi kutengewa fungu la bajeti.

Alisema mafisadi wanakwamisha maendeleo ya uchumi wa nchi, pamoja na kusababisha umaskini kwa Watanzania.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar