Selasa, 16 Juni 2009

Viongozi Gabon kumpumzisha Bongo


Shughuli za mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa rais wa Gabon, Omar Bongo, zinaendelea katika mji mkuu wa nchi hiyo, Libreville.
Rais wa Ufaransa, Nicholas Sarkozy, na viongozi wengine wa Afrika wasiopungua kumi na wawili, tayari wamefika mjini Libreville.
Bw Sarkozy alizomewa na baadhi ya vikundi vya watu, kulingana na taarifa za sherika la habari la AFP.
Bw Bongo, ambaye aliiongoza Gabon kwa kipindi cha miongo minne, ndiye aliyekuwa kiongozi wa Afrika kuongoza nchi kwa muda mrefu zaidi.
Aliaga dunia wiki iliyopita katika kliniki moja nchini Uhispania, baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Atazikwa katika kijiji chake cha nyumbani, Franceville, kusini-mashariki mwa nchi, siku ya Alhamisi.
Bw Sarkozy alipowasili katika kasri ya rais mjini Libreville, baadhi ya watu walimshangilia, lakini baadaye wengine walianza kumzomea.
Chini ya uongozi wa Bw Bongo, nchi ya Gabon, na ambayo ina utajiri mkubwa wa mafuta, iliendelea kudumisha ushirikiano wake wa kiuchumi na kisiasa na Ufaransa, nchi ambayo iliitawala kikoloni.
Ufaransa ina kama wanajeshi 1000 mjini Libreville.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar