HALI ya usalama kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), Mbagala Kuu jijini Dar es salaam na maeneo ya jirani, bado haijawa shwari baada ya bomu moja kulipuka jana na kujeruhi wanajeshi saba, mmoja kati yao akiwa mahututi.
Habari kutoka maeneo jirani na kambi hiyo ya Kikosi cha 673 zinasema mabomu yamekuwa yakilipuka mara kwa mara kati ya saa 7:00 usiku na saa 9:00 alfajiri, ingawa la jana lilipuka majira ya saa 4:00 asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana kutoka ndani ya kambi hiyo na kuifikia Mwananchi zinadai kuwa bomu hilo lilijeruhi wanajeshi saba waliokuwa jirani na eneo la bomu kwenye kambi hiyo ambayo ilikumbwa na milipuko ya mabomu Aprili 29.
Habari zinasema wakati bomu hilo linalipuka, askari hao hawakuwa na taarifa yoyote.
"Ni kweli kuna bomu lililolipuka leo saa 4:00 asubuhi hapa kambini na kujeruhi wenzetu saba, mmoja kati yao yuko mahututi," alisema mwanajeshi mmoja aliyeomba jina lake lisitajwe.
"Hata sisi hali hii inazidi kutupa wasiwasi, kwa sababu hatufahamu maeneo sahihi ambayo mabomu yapo."
Kauli yake inalingana na ya mwanajeshi mwingine aliyefika kwenye ofisi za Mwananchi jana asubuhi kutoa taarifa ya mlipuko huo na kueleza kuwa takriban watu saba walijeruhiwa kwenye kambi hiyo na kukimbizwa hospitalini.
Alisema hali hiyo ya wasiwasi inasababisha washindwe kukamilisha zoezi la kufanya usafi na kazi ya kutafuta mabaki ya mabomu katika maeneo ya kambi hiyo kuwa ngumu.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo walisema bomu lililolipuka jana lilisababisha hofu kubwa kwa baadhi ya raia wa eneo hilo, ambao wengi wao walipoteza ndugu na nyumba zao wakati wa milipuko ya kwanza iliyochukua maisha ya watu zaidi ya 26, kubomoa nyuma zaidi ya 800 na kusababisha watu zaidi ya 8,000 kukosa makazi.
Grace Songo, aliyedai kupata matatizo ya moyo kutokana milipuko hiyo, alisema: "Ingawa mlipuko huu wa leo haujasababisha madhara makubwa kwa raia, ni hatari kwa sababu tunapata mshtukuko mkubwa."
Plasda Njimbari, 35, alisema mbali na kulipuka kwa bomu, milipuko mingine zaidi ya mitatu husikika kati ya saa 9:00 usiku na saa 10:00 alfajiri kila siku.
"He! We uko dunia gani hapa. Siku hizi hapaitwi Mbagala, hii ni Baghdad kwa sababu kila siku ni milipuko kwa kwenda mbele," alisema Njibari.
Alisema: "Utaratibu huu ambao wanajeshi wameuanzisha wa kulipua mabomu usiku ni hatari zaidi kuliko mchana kwa sababu baadhi yetu tunaishi kwenye nyumba zenye nyufa na ziko kwenye hatari ya kuanguka hivyo ipo siku wataongeza maafa."
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi alikiri kuwepo kwa mlipuko wa bomu la jana na kusema kuwa hayakuwa na madhara makubwa katika eneo hilo.
"Ni kweli kuna bomu limelipuka, lakini kwa muujibu wa taarifa za kijeshi walizonipa wao wenyewe, hilo lilikuwa ni kiwashio tu na sio bomu na hakikuwa na madhara makubwa," alisema Lukuvi.
"Hata kama kilipuka chenyewe, hakiwezi kuwa na madhara makubwa kwa sababu hakina uwezo wa kusafiri zaidi ya kilomita moja".
Kuhusu majeruhi, Lukuvi alisema: "Mimi sifahamu kuhusu suala la majeruhi, isipokuwa taarifa niliyopewa na wanajeshi wenyewe ni kwamba kiwashio hicho hakikuleta madhara makubwa".
Lukuvi aliwataka wakazi wa mbagala kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kwao.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar