Rais wa Marekani Barack Obama amesema kuwa, atafanya juhudi kuzuia kutolewa picha zinazoonyesha mateso yaliyofanywa dhidi ya washukiwa wa ugaidi baada ya madai kuwa huenda zikasababisha kulengwa kwa wanajeshi wa Marekani walioko mataifa ya nje.
Rais Obama alisema kuwa kutolewa kwa picha hizo kutachochea chuki zaidi dhidi ya Marekani na kuyaweka maisha ya wanajeshi wa Marekani walioko mataifa ya kigeni kwenye hatari.
Akizungumza na waandishi wa habari rais Obama alisema kuwa, hata hivyo ukiukwaji wa haki za wafungwa ni jambo ambalo haliruhusiwi.
Obama anachukua hatua hiyo, baada ya utawala wake kusema kuwa utatoa mamia ya picha zinazoonyesha mateso yaliyofanywa kwa wafungwa, katika magereza yanayosimamiwa na Marekani nchini Iraq na maeneo mengine duniani.
Hatua hiyo ni kama pigo kwa baadhi ya wanachama wenye mtazamo wa ukadirifu, ambao wanachukulia kutolewa kwa picha hizo kama njia ya kuwafanyia uchunguzi maafisa katika utawala uliopita wa rais George Bush na kuisafisha sura Marekani.
Obama anachukua hatua hiyo baada ya makamanda wa ngazi za juu na baadhi ya wanachama wa bunge la Marekani, kuelezea kuhusu hatari ya kutolewa kwa picha hizo ikiwemo ya kushambuliwa kwa wanajeshi wa Marekani nchini Iraq na Afganistan.
Obama aliutetea uamuzi wake na kusema kuwa kutolewa kwa picha hizo hakutaongezea chochote kwa kufahamu kile kilichofanywa na watu wachache, na kuongeza kwamba kutolewa kwa picha hizo badala yake kutazidisha hisia za chuki dhidi ya Marekani.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani Robert Gibbs alisema kuwa utawala wa rais Obama utaomba kutolewa kwa amri ya mahakama itakayozuia kutolewa kwa picha hizo.
Chama cha haki za kiraia nchini Marekani ambacho kilitaka kutolewa kwa picha hizo kilielezea hasira zake na kusema kuwa, hatua hiyo ni kinyume na ahadi za wakati wa kampeni ya rais Obama juu ya haja ya kuwepo na uwazi.
Wakati huo huo shirika la kimataifa kutetea haki za bidamu la Amnesty International, pia limeelezea kukasirishwa kwake na uamuzi huo. Mkurugenzi wa shirika hilo Larry Cox alisema kuwa wanadamu wamekuwa wakiteswa na kunyimwa haki zao,Wamarekani wamedanganywa na wahusika hawakuchukuliwa hatua zozote.
Hata hivyo uamuzi huo wa rais Obama uliungwa mkono na seneta Lindsey Graham kutoka chama cha Republican na Seneta Joe Liebarman, waliosema kuwa rais Obama amechukua hatua sahihi.
Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates alisema pia naye alisema kuwa, alibadilisha mawazo yake baada ya kuyasikiliza maoni ya makamanda wa ngazi za juu katika jeshi la Marekani lililoko nchini Iraq na Aghanistan.
Hata hivyo baadhi ya wanachama wa chama cha Democratic akiwemo spika wa bunge Nancy Pelosi wamekuwa wakitoa wito wa kuundwa kwa tume ya ukweli ya kuchunguza mbinu za mahojiano zilizofanywa na utawala wa rais George Bush.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar