Matukio muhimu | 11.05.2009
Amani idumishwe! asema Papa huko Israel
Papa Benedict wa XV1 alitua katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion ulioko nje ya mji wa Tel Aviv alikolakiwa na maafisa wa ngazi za juu wa serikali pamoja na viongozi wakuu wa kidini.Punde baada ya kuwasili kiongozi huyo wa kanisa katoliki aliusisitizia umuhimu wa kudumisha amani katika eneo hilo,''Ninaomba kuwa uwepo wenu Israel pamoja na maeneo ya Palestina utafanikiwa kudumisha amani na heshima kwa wakazi wote wa eneo hili lililotajwa katika Biblia.''
Papa akiwa na viongozi wakuu wa serikali ya Israel Israel ilichukua hatua zote kuchukua tahadhari za kiusalama kabla ya kuwasili kwa kiongozi huyo wa kanisa katoliki ulimwenguni.Maelfu ya maafisa wa usalama walishika doria katika eno hilo vilevile mji wa Jerusalem ulifungwa na ndege zote zilipigwa marufuku kutua Israel.
Kiongozi huyo aliyesisitiza kuwa anahubiri amani kote ulimwenguni hakusita kuwahakikishia waliomlaki kuwa nia yake ni njema,''Nimekuja kama wale wote walionitangulia kuzuru maeneo takatifu na kuombea mahsusi amani.Amani katika mataifa tukufu na amani kote ulimwenguni.Nawashukuruni nyote tena kwa kunialika na niwahakikishia nia yangu njema.Mungu awape nguvu…….Mungu awape amani.'' alisistiza Papa.
Papa Benedict hakuchelea kuutilia mkazo msimamo wa Vatican unaosisitiza kuwa unaunga mkono hatua ya kuwa na madola mawili ya Palestina na Israel kama njia ya kuutatua mzozo wa Mashariki ya Kati.Msimamo huo umezua mitazamo tofauti na serikali mpya ya Israel.Kiongozi huyo wa kanisa katoliki alitoa wito wa kupatikana kwa suluhu itakayowawezesha wakazi wote wa eneo hilo kuishi kwa amani katika nchi zao zilizo na mipaka inayotambulika kimataifa.Hata hivyo Papa Benedict hakulitaja neno taifa jambo ambalo serikali mpya ya Israel imekuwa ikijizuia kuwaahidi Wapalestina.Jamii ya kimataifa kwa upande wake imekuwa ikiishinikiza Israel kulitathmini jambo hilo.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwako katika uwanja wa ndege kumlaki Papa Benedict.Bwana Netanyahu anatarajiwa kukutana na Rais wa Misri Hosni Mubarak kwa lengo la kufanya mazungumzo ya amani kati yao na Palestina.
Itakumbukwa kuwa Mfalme Abdala wa Jordan aliyekutana na Papa Benedict katika kipindi cha siku tatu zilizopita amenukuliwa akisema kuwa uongozi mpya wa Marekani unashirikiana na nchi yake wakiwa na azma ya kufikia makubaliano ya amani na mataifa ya Kiislamu.
Mji wa Bethlehem Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni alitoa wito wa kuwaruhusu watu wote wa dini yoyote ile kuyazuru maeneo takatifu mjini Jerusalem.Israel imekuwa ikidhibiti maeneo mengi ya mji huo tangu vita vilivyotokea mwaka 1967.Hata hivyo Israel iliitenga sehemu ya mji huo ukiwemo mji wa Kale mipaka isiyotambulika kimataifa.
Papa Benedict anatazamiwa kukutana na viongozi wakuu wa serikali ya Israel ,viongozi wa kidini pamoja na wakimbizi wa Palestina wakazi wa eneo lililo na uzio uliowekwa karibu na eneo linaloaminika kuwa mahala alipozaliwa Yesu Kristo mjini Bethlehem.Kiongozi huyo pia atazuru makumbusho ya mauaji ya Holocaust ya Yad Vashem atakakoweka shada la maua kwa ajili ya kuwakumbuka Wayahudi milioni sita waliouawa wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia.
Mwandishi: Makidamakida
Mhariri: THE THOMCOM
Tidak ada komentar:
Posting Komentar