Sabtu, 30 Mei 2009

Ikulu yawabana makatibu wakuu


AWAZUIA KUWA WENYEVITI WA BODI ZA MASHIRIKA


BAADA ya kuwazuia wabunge kuwa wajumbe kwenye taasisi za kifedha, mianya ya ufisadi imezidi kubanwa baada ya Ikulu kuandaa waraka ambao utawaondoa makatibu wakuu wote katika nafasi za uenyekiti wa bodi za mashirika ya umma.

Katikati ya wiki, gavana wa Benki Kuu (BoT), alitoa maagizo kuwa taasisi za kifedha za umma hazitaruhusiwa kuwateua wabunge kuwa wajumbe wa bodi za taasisi hizo ili kuondoa mgongano wa kimaslahi.

Kwa mujibu wa duru za habari za kuaminika, agizo la Ikulu limetolewa na katibu mkuu kiongozi, Philemon Luhanjo. Habari hizo zinasema hatua hiyo imefikiwa ili kuondoa mgongano wa kimaslahi katika utumishi wa umma.

Kaimu msajili wa hazina, Geoffrey Msella alikiri jana kuwa alipata taarifa za waraka huo, lakini akasema hajapata barua rasmi kutoka kwa katibu mkuu kiongozi.

"Nafikiri, inawezekana amewaandikia kwanza makatibu wakuu wenyewe na baadaye anaweza kuleta kwetu, lakini hadi sasa (jana) sijapata taarifa rasmi," alisema Msella.

Alipoulizwa kuhusu waraka huo, Luhanjo alisema hakuwa katika nafasi nzuri kuzungumza. "Siwezi kuzungumza kwa sasa nipo kwenye mkutano," alisema Luhanjo kwa kifupi jana jioni.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe alikiri kupata taarifa hizo alipohojiwa na Mwananchi, lakini akasema si rasmi bali amesikia.

Kutolewa kwa waraka huo wa kudhibiti watendaji hao wakuu wa wizara ni moja ya hatua kubwa za serikali katika kuimarisha utawala bora na kuondoa mgongano wa kimaslahi.

Baadhi ya makatibu wakuu ambao ni wenyeviti wa bodi za mshirika ya umma hadi sasa, ni pamoja na Bliandina Nyoni wa Wizara ya Afya. Kwa sasa, Nyoni ni mwenyekiti wa bodi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii ( NSSF).

Mwingine ni Ramadhan Kijjah ambaye kwa sasa ni katibu mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi. Kijjah ni mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi wa Pesheni kwa Mashirika ya Umma (PPF) na Mfuko wa Jamii kwa Watumishi wa Serikali (PSPF).

Kwa mantiki hiyo, makatibu wakuu watabaki kuwa wajumbe wa bodi kutokana na mwingiliano wa shughuli za kiutendaji.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar