Phiri: Mimi Yanga? Acheni masihala
KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Phiri amesema anaendelea kusaka wachezaji kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake, lakini ameshangazwa na habari kuwa atajiunga na Yanga na ameziita habari hizo kuwa ni masihala makubwa.
"Yanga! Kwa nini? Kwani kocha wao (Dusan Kondic) ameondoka? Nani kasema? Kila mtu anaweza kusema lake ila mimi nina mkataba na Simba na wala sijazungumza na Yanga.
Nakuhakikishia naelekeza nguvu zangu Simba na kila kitu ninafanya kwa ajili ya Simba kwa kipindi hiki,� alisema Phiri jana Ijumaa alipozungumza na Mwanaspoti kwa simu kutoka Zambia.
Phiri raia wa Zambia alisema hawezi kufanya kitu ambacho kitachanganya mipango yake; "Waambie niko Simba na hata huku ninafanya kazi za Simba," alisisitiza kocha huyo mpole.
Wakati Phiri akisema hivyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Dusan Kondic aliiambia Mwanaspoti jana Ijumaa kuwa kama viongozi wa Yanga watakuwa wameamua hivyo, atamkaribisha Phiri.
"Suala hili wanaweza kulizungumzia viongozi, lakini ni kitu kibaya sana ambacho mtu anaweza kujitangazia tu. Mimi nipo Yanga, naendelea na kazi za Yanga kwa ajili ya msimu ujao tena kwa umakini mkubwa. Lakini kama yatatokea mabadiliko mimi ni kocha. Kukaa katika klabu kwa siku kadhaa na kuondoka si kitu kigeni," alisema raia huyo wa Serbia.
Kwa upande wa uongozi wa Yanga, Katibu Mkuu wa klabu hiyo kongwe nchini, Lucas Kisasa alisema hawana mpango wowote na Phiri.
"Tunafikiria vitu vingine kabisa, suala la kocha ni kwamba Dusan Kondic ndiye kocha mkuu wa Yanga. Naomba watendeeni haki wasomaji wenu kwa kuwaandikia habari za kweli. Kwa kifupi hatuna mpango huo," alisema Kisasa.
Mwanaspoti ilipiga mguu hadi kwa Mfadhili wa Yanga, Yusuf Manji ambaye pia alisisitiza kuwa hizo taarifa ni mpya kwake na anazisikia kwa mara ya kwanza.
"Tayari tuna Kondic ambaye ndiye kocha bora Tanzania, amefanya karibu kila kitu na Yanga wanajivunia. Timu imechukua ubingwa ikiwa na mechi mkononi, tumetoa mfungaji bora, tuna wachezaji wanatakiwa Ulaya na kwingine kama China. Hatuna mpango wa kutaka kocha mwingine,' alisema Manji.
Lakini kwa upande wa Simba kupitia mwenyekiti wake wa usajili, Kassim Dewji wamesisitiza kwamba Phiri ana mkataba na klabu hiyo na hakuna mpango wowote wa kumwachia aende Jangwani.
Taarifa ya baadhi ya vyombo vya habari jana zilisema kuwa kocha huyo anataka kujiunga na Yanga jambo ambalo lilizua mjadala sehemu mbalimbali nchini.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar