Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (kushoto) akizungumza na Spika wa Bunge Samweli Sitta (kulia) na Mbunge wa tabora mjini Silaju Kaboyonga nje ya ukumbi wa Bunge Mjini Dodoma jana. |
MSUGUANO kati ya mihimili miwili, Bunge na Serikali umejitokeza baada ya Spika Samuel Sitta na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutofautiana kuhusu hatua ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwahoji wabunge kuhusu tuhuma za watunga sheria hao kulipwa posho mara mbili.
Wakati tofauti hizo zikijidhihirisha kwenye kikao cha faragha cha wabunge kilichofanyika ukumbi wa zamani wa Bunge unaojulikana kama Pius Msekwa, mmoja wa vinara wa vita dhidi ya ufisadi, Dk Harrison Mwakyembe aliongea na waandishi wa habari na kushutuma vikali kitendo hicho cha Takukuru akikielezea kuwa ni cha kisasi na kusema kamwe hatakubali kuhojiwa.
Hatua ya Takukuru kuhoji wabunge hao imetokana na malalamiko kutoka taasisi na mashirika mbalimbali kulalamikia mwenendo wa Kamati za Bunge kudai posho mara mbili kwenye idara na taasisi za serikali. Bunge hugharimia posho kwa ajili ya shughuli za kamati zao zinazosimamia vyombo hivyo, lakini baadhi ya wabunge walidaiwa kuendelea kupokea posho mara mbili, hali ambayo iliilazimisha Takukuru kuanza kuwahoji wanaotuhumiwa kufanya hivyo.
Lakini wabunge, akiwemo Spika Sitta, wamekuwa wakipinga kitendo hicho na jana serikali ilionekana kuunga mkono wabunge kuhojiwa huku Bunge likiendelea kupinga.
Tofauti za watendaji hao wawili wa serikali na Bunge zilizijitokeza jana mchana wakati wabunge walipokutana kwa faragha kupokea taarifa ya agenda zilizopitishwa na Kamati ya Uongozi kwa ajili ya kujadiliwa kwenye mkutano unaoendelea mjini hapa.
Suala la kuhojiwa kwa wabunge lilizua mjadala mkali kiasi kwamba mkutano huo, ambao awali ulikadiriwa kuwa ungechukua takriban saa moja kuanzia saa 5:15 asubuhi, ulimalizika karibu saa 8:00 alasiri.
Katika mjadala huo, mbunge wa Dole, Juma Suleiman N’hunga (CCM) alienda mbali na kusema chombo kilichopaswa kuwahoji wabunge ni Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge na sio Takukuru ambao ni mhimili mwingine wa dola.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, kitendo cha Takukuru kuwahoji wabunge ambao ni mhimili wa Bunge ni ukiukwaji wa katiba na akapendekeza Takukuru ikatazwe kuendelea na zoezi lake la kuwahoji wabunge.
Mbunge mwingine aliyechangia mjadala huo mzito alipendekeza Bunge limpigie kura ya kutokuwa na imani na mkurugenzi wa Takukuru, Dk.Edward Hoseah kama ilivyotokea kwa taasisi kama hiyo nchini Kenya.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge walitofautiana katika suala hilo, huku baadhi wakihoji sababu za chombo hicho kukaa kimpya wakati Basil Mramba alipohojiwa na kushitakiwa mahakamani.
Mramba, aliyekuwa waziri wa fedha katika serikali ya awamu ya tatu na baadaye waziri wa miundombinu katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, anakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi iliyoiingizia serikali hasara ya mamilioni.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zimedokeza kuwa Mramba alitumia mkutano huo kuelezea kwa kirefu namna alivyohojiwa na Takukuru katika mazingira ya kudhalilisha tena na vijana wadogo ambao hawakustahili kumhoji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, William Shelukindo naye alitumia kikao hicho kuelezea masaibu yaliyomkuta wakati alipoitwa na Takukuru kutoka jimboni kwake hadi Dar es Salaam na kuhojiwa kwa saa nne.
Shelukindo alihoji inakuwaje Takukuru ianzishe uchunguzi huo sasa wakati ambao Bunge linatakiwa kupokea utekelezaji wa maazimio yake ambayo baadhi yanataka DK Hosea awajibishwe.
Pamoja na Spika kueleza kuwa tayari ameandaa mazingira mazuri yatakayotumika kuwahoji wabunge hao ikiwamo kuipatia Takukuru ofisi kwenye jengo la Bunge mjini Dodoma na Dar es Salaam Salaam, bado baadhi ya wabunge walipinga.
Kutokana na michango ya wabunge wengi kuonyesha dhahiri kukerwa na kitendo cha Takukuru, Spika Sitta alitangaza katika kikao hicho kuwa kuanzia hiyo jana mahojiano hayo yamesimamishwa.
Lakini Waziri Mkuu akaonyesha kutokubaliana na maamuzi hayo ya spika na kueleza kuwa uchunguzi huo wa Takukuru utaendelea kwa kuwa ofisi ya Rais Ikulu ndio ambayo imeagiza ufanyike.
Waziri Mkuu Pinda alisisitiza kuwa kinachotakiwa kufanywa si kusitishwa kwa uchunguzi huo bali ufanyike katika maeneo yenye staha na katika mazingira ambayo hayawadhalilishi wabunge.
Mkutano huo haukuelezwa pia kama ni lini ripoti ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge itawasilishwa bungeni katika mkutano huu wa 17 hali ambayo inazidisha usiri na uzito wa mjadala kuhusu kashfa ya Richmond.
Wakati hayo yakiendelea, mbunge wa Kyela, Dk Mwakyembe aliwaambia waandishi wa habari kuwa lengo la Takukuru kuendesha uchunguzi huo ni kuwafunga midomo wabunge wasishikie bango kashfa ya Richmond.
Dk. Mwakyembe, ambaye aliiongoza kamati teuli iliyochunguza kashfa ya Richmond, alisema binafsi hawezi kukubali kile alichodai ni upuuzi wa taasisi hiyo kutaka kuwahoji wabunge katika kipindi hiki tete cha Richmond.
Dk Mwakyembe aliishangaa taasisi hiyo akiitaka ijichunguze kwanza kabla ya kuamua kuwachunguza wabunge kuhusu malipo ya posho mbalimbali, huhusan posho za chakula.
“Takukuru waliponipigia simu kunihitaji, nilikataa kwa sababu kwa mazingira yenyewe hili zoezi linaendeshwa kwa malengo ya kuwafunga midomo wabunge kuhusu sakata la Richmond …mimi nilikataa,†alisema.
Alisema kuwa malipo hayo ya posho yamekuwepo miaka mingi na yamekuwa yakitengewa bajeti katika fungu la kuwakirimu wageni na haoni chembe yoyote ya rushwa katika suala la malipo hayo.
Dk.Mwakyembe alisema alikataa wito huo wa Takukuru kwa kuwa ulikuwa unakwenda kinyume na haki na madaraka ya Bunge na pia ni kinyume cha vifungu 100 na 101 vya katiba ya nchi vinavyotoa uhuru kwa Bunge.
“Sisi wabunge tunasubiri utekelezaji wa maazimio ya Bunge na moja ya maazimio hayo yanataka mtendaji mkuu wa Takukuru awajibishwe kwa kutofanya vizuri kazi yake katika uchunguzi wa Richmond,†alisisitiza Mwakyembe.
“Alisema mchakato bado haujakamilika na wewe unaenda kuwahoji wale wanaokuhoji... hilo halikubaliki na ni kinyume cha utawala wa sheria…mimi ni mwanasheria mwalimu wa sheria siwezi kukubali upuuzi huu.â€
Dk. Mwakyembe aliitaka Takukuru kumpeleka mahakamani kama ana makosa na kutamba kuwa hata ikifanya hivyo ataibwaga mahakamani na kusisitiza mafisadi wasitumie vyombo vya habari kumchafua.
“Tukiaanza kuongelea mambo ya posho Takukuru wenyewe ndio vinara wa kutoa posho…wametufanyia semina mara mbili mimi; naishi Dar es salaam, wanatulipa posho ya kulala wajichunguze wao wenyewe kwanza,†alisema.
Mwanasiasa huyo aliitaka Takukuru kuacha kukimbilia vitu vidogovidogo na badala yake ishughulikie mambo makubwa yenye maslahi kwa nchi.