Jumat, 16 Oktober 2009

CCM bado inatokota














Kamati ya Mzee Mwinyi kumkabili Spika Sitta


KAMATI ndogo ya wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyoundwa chini ya Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, kuchunguza kiini cha chuki miongoni mwa wabunge wake ndani ya bunge , pamoja na mambo mengine inatarajia kumhoji Spika wa Bunge, Samuel Sitta.

Spika Sitta amekuwa kiongozi wa kambi ya wabunge wa CCM bungeni, ambao wamekuwa wakijipambanua kama makamanda wa vita ya ufisadi hasa baada ya matokeo ya Ripoti ya Uchunguzi ya Bunge kuhusu mkataba wa Richmond, ambayo ilimfanya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, kujiuzulu mwezi Februari mwaka jana.

Akizungumza nyumbani kwa mzee Mwinyi, jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo inayoundwa na makada watatu wa CCM, Pius Msekwa, alisema kamati yake itaanza kufanya upelelezi wake baada ya kuanza kwa mkutano wa Bunge, unaotarajiwa kufanyika siku 10 zijazo.

Kauli ya Msekwa inakuja kipindi ambacho pia wabunge wake wanaojiita makamanda wa vita ya ufisadi wameonekana kukaidi onyo la Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) , lililotolewa katika mkutano uliofanyika Agosti 16 hadi 17, ambalo liliwataka wasizungumze ovyo nje ya vikao vya chama.

Lakini, licha ya kambi hiyo ya wabunge, makamanda wa ufisadi kuendelea kukaidi amri hiyo na kurusha makombora kwa kambi nyingine ya watuhumiwa wa ufisadi, pia wamekuwa wakijihami kwa kueleza umma kwamba, wanahujumiwa majimboni ili wasirudi mwakani.

Hata hivyo, Msekwa alifafanua zaidi kwamba, baadhi ya wabunge nao wanatarajiwa kuhojiwa na kamati hiyo.

NEC ilipokutana mjini Dodoma, iliunda timu hiyo ili kuchunguza tabia iliyozuka miaka ya karibuni ya baadhi ya wabunge wake, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na viongozi ndani ya chama hicho, kutoa matamshi hadharani yenye mwelekeo wa kuchafuana majina na yanayoashiria kuvunjika kwa umoja na mshikamano ndani ya CCM na serikali.

Wabunge ambao wamekuwa wakijinasibu kupambana na ufisadi, lakini pia wakiwa wa kwanza kulia kwa madai ya kuchezewa mchezo mchafu majimboni ni pamoja na Lucas Selelii (Nzega), Dk Harrison Mwakyembe (Kyela), Beatrice Shelukindo (Kilindi), William Shelukindo (Bumbuli), Fredi Mpendazoe (Kishapu), James Lembeli (Kahama) na Anne Kilango Malecela (Same Mashariki).

Lakini Msekwa alifafanua kwamba, kamati hiyo itaanza kwa kwenda Zanzibar wiki ijayo ambako itawachunguza wajumbe wa kamati ya CCM ya Baraza la Wawakilishi, kupeleleza kiini cha matamshi mengine yenye mwelekeo wa kusababisha mgawanyiko ndani ya chama na serikali juu ya hoja ya mafuta.

Msekwa aliweka bayana kwamba, baada ya kutoka Zanzibar watahamishia majukumu yao kwenye Bunge katika mfumo ambao pia utapitia Kamati ya wabunge wa CCM bungeni.

Alisisitiza zaidi kwamba, mfumo wa utendaji wa kamati hiyo ambayo inaundwa pia na Abdulrahman Kinana, hautekelezi kazi zake kwa siri na miongoni mwa kauli watakazozifanyia kazi, ni juu ya wabunge wake waliodai kuhujumiwa na mafisadi.

"Hatupelelezi kimya kimya. Ndiyo maana tunaweka wazi," alisema Msekwa, bila kutaja jina na kuongeza.

"Watachunguza ukweli wa madai ambayo yalitolewa na wabunge kadhaa bungeni kwamba, mafisadi wanatumia fedha kuwatishia maisha na hata kuwahujumu ili wasichaguliwe tena kwenye majimbo yao."

"Tutatafuta ukweli kujua, hivi kweli ni msingi wa ufisadi," alisema Msekwa ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge kwa muda mrefu.

Hata hivyo, aliweka bayana kwamba, kulingana na mfumo wa CCM, hakuna mbunge mwenye hati miliki kwenye jimbo lake na kila baada ya miaka mitano huwa wazi kwa mwana-CCM yeyote kuliwania.

"Ilionekana hii siyo hali nzuri kwa chama chetu, kwa sababu inavunja mshikamano ndani ya chama na serikali," alieleza Msekwa.

Msekwa ambaye pia alitumia muda kutetea uhalali wa kamati hiyo pamoja na umuhimu wa NEC kuiteua, alisema siyo mara ya kwanza kwa CCM kuwachunguza wabunge baada ya kuona mambo yanaenda shaghalabaghala.

Akitoa mifano ya kihistoria, Msekwa alisema mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1968 wakati wa enzi za serikali ya awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Safari ya pili, alisema ni enzi za Mwinyi akiwa Rais, ambako mwaka 1993 wabunge waliibuka na msimamo wa kutaka kuwa na serikali tatu, Tanganyika, Zanzibar na Muungano.

Mwaka 1993 muungano uliingia katika msukosuko mkubwa baada ya kundi la wabunge maarufu kama G55, kutaka kuvunja muungano wa sasa kipindi ambacho Waziri Mkuu alikuwa ni mzee John Malecela, kitendo ambacho kilimchukiza Mwalimu.

Kuhusu utaratibu huo kuonekana kwamba unawafunga midomo wabunge katika kushughulikia mambo yenye maslahi kwa umma, Msekwa alipinga.

"NEC haiwafungi wabunge midomo. Hili liko wazi. Wabunge wanaruhusiwa kuikosoa serikali kwa kadri wanavyoona inafaa. Na hii imekuwa ikifanyika bila kipingamizi chochote," alisema Msekwa.

Aliongeza kwamba, inachofanya NEC ni kutekeleza jukumu la mfumo wa nchi ambapo chama ndicho kinachosimamia serikali, hivyo kina mamlaka ya kusimamia utendaji wa shughuli zote za serikali yake.

Kuhusu uhuru wa wabunge kama unavyofafanuliwa na Ibara ya 100 ya katiba ya Tanzania wa kujadili mambo yote bila kuhojiwa na chombo chochote, alisema:

"Kifungu hiki kinazuia chombo chochote kuhoji maamuzi ya bunge, lakini hakizuii chama kukosoa mwenendo wa mijadala bungeni."

Akizungumzia hoja ya mafuta, alisema kwenye Baraza la Wawakilishi zilikuwepo lugha za kuzusha mgawanyiko ambao serikali ya Muungano, ilielezewa kama mkoloni anayeinyonya Zanzibar.

Msekwa alisema suala hilo liko wazi ndani ya katiba, kwamba mafuta yanasimamiwa na Serikali ya Muungano.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar