Rabu, 14 Oktober 2009

Juhudi za amani ya Mashariki ya kati




Kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas
Fatah watia saini bila ya Hamas mswaada wa mkataba wa suluhu katika wakati ambapo ripoti ya jaji Goldstone inatazamiwa kuzungumziwa leo na baraza la usalama la umoja wa mataifa

Chama cha Fatah kinachoongozwa na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina,Mahmoud kimetia saini mswaada wa suluhu bila ya Hamas,waliopinga kushiriki katika sherehe za kutiwa saini mswaada huo ulioandaliwa na Misri.Wakati huo huo baraza la usalama la umoja wa mataifa linatazamiwa kujadili ripoti ya jaji Goldstone kuhusu uhalifu uliotokea wakati wa vita vya Israel katika Gaza.
Viongozi wa chama cha Hamas kinachotawala Gaza wanasema hawajaamua bado kama wataidhinisha au la mswaada huo wa suluhu.
Mbali na hayo,kuna kizingiti chengine kinachokorofisha kutiwa saini mswaada huo wa suluhu; Hamas wameilaumu Misri jana kwa kumtesa hadi kufa ndugu wa kiume wa mmojawapo wa wasemaji wao-tuhuma zilizokanushwa na viongozi wa Misri.
Duru za Fatah hazijafafanua nani ametia saini mswaada huo kwa niaba ya chama hicho.Ujumbe unaoongozwa na afisa wa ngazi ya juu wa Fatah,Azzam al Ahmed unatazamiwa kwenda Misri hii leo kuwasilisha mswaada huo.
Mkutano kati ya makundi mawili hasimu ya kipalastina,utakaofuatiwa na sherehe za kutiwa saini makubaliano ya suluhu,umepangwa kufanyika October 24 na 26 ijayo mjini Cairo.Lakini Hamas wanapinga kuhudhuria mkutano huo.
Kwa kufanya hivyo wanataka kulalamika dhidi ya uamuzi wa kiongozi wa utawala wa ndani Mahmoud Abbas,wa kutaka uakhirishwe mjadala wa baraza la haki za binaadam la umoja wa mataifa kuhusu ripoti ya jaji Richard Goldstone kuhusu uhalifu wa vita katika Gaza.
Afisa wa ngazi ya juu wa Fatah,Mohammed Dahlan amesema watajaribu kumshinikiza rais Mahmoud Abbas aitishe uchaguzi wa bunge na wa rais,ikiwa Hamas watapinga kutia saini mkataba huo.
Bildunterschrift: Jaji Richard Goldstone aliyefichua ukweli wa yaliyotokea Gaza
Wakati huo huo ripoti ya jaji wa Afrika kusini Richard Goldstone itajadiliwa hii leo na baraza la usalama la umoja wa mataifa mjini New-York,wakati wa mjadala jumla kuhusu hali ya mashariki ya kati.
Uamuzi huo wa maridhiano umefikiwa wakati wa mashauriano ya siri yaliyofuatia pendekezo la Libya ,inayoungwa mkono na nchi za kiarabu,kiislam na zile zisizoelemea upande wowote la kuitishwa mkutano wa dharura wa baraza la usalama kuzungumzia ripoti ya uchunguzi wa maovu yaliyofanyika Isreal ilipoishambulia Gaza msimu wa baridi uliopita.
Muakilishi wa Israel katika Umoja wa mataifa amesema anahakika Marekani ingetumia kura ya turufu kama baraza la usalama lingebidi kuipigia kura ripoti ya Goldstone.
Kwa mujibu wa wanadiplomasia mjini New-York,nchi za magharibi zimepinga kuitishwa mkutano maalum kuhusu ripoti ya Goldstone wanayosema "ina walakin ."

Tidak ada komentar:

Posting Komentar