Sabtu, 17 Oktober 2009

serikali yakataa wito wa Zitto kuitaifisha Dowans

Serikali yampuuza Zitto
Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hoja ya kutaifisha mitambo ya kampuni ya Dowans

YASEMA HAINA SERA NA SHERIA YA UTAIFISHAJI

Na Waandishi Wetu

HOJA ya mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe ya kutaka serikali itaifishe mitambo ya kuzalisha umeme ya kampuni ya Dowans Tanzania Limited, imevuta hisia tofauti huku serikali ikisema haitaweza kuitekeleza kwa kuwa haina sera ya utataifishaji.

Kauli ya serikali imekuja siku moja baada ya Zitto kuwaambia waandishi wa habari kuwa serikali haina budi kufumba macho na kutaifisha mitambo hiyo ya Dowans ili kuiondoa nchi katika janga kubwa la ukosefu wa umeme linaloongeza ugumu wa maisha kwa wananchi na kuiingizia serikali hasara kubwa.

"Mitambo ya Dowans ni mizuri kwa kuwa ukiweka gesi na kuwasha tunapata megawati 120, hivyo ni bora itaifishwe ili tuondokane na giza na kushuka kwa uchumi wetu," alisema Zitto katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam.

Juzi usiku, Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja alisema: "Sijaisoma taarifa yake wala kusikia kwenye televisheni, lakini sisi kama taifa tunaongozwa na sera na sheria.

"Siwezi kufikia hapo; kutaifisha mali si mwongozo na sera yetu. Sisi kama taifa hatuna sera za kutaifisha; huo ndio msingi. Kisera si sera ya CCM na hatuna sheria ya kutaifisha mali za wawekezaji. Sheria zinaeleza kutambua utawala wa sheria na kutatua matatizo au migogoro kwa kutumia sheria."

Ngeleja alifafanua kuwa kimsingi serikali ina matatizo na Dowans ambayo yapo mahakamani na ambayo yanapaswa kumalizwa kwa njia ya sheria, si kwa kutaifisha mitambo hiyo na kuongeza kuwa matatizo ya umeme yaliyopo nchini yanatafutiwa ufumbuzi kwa njia sahihi.

Hata hivyo, alisema Zitto kama Mtanzania yeyote ana uhuru wa kutoa maoni yake na kwamba, yeye (waziri) anayatambua na kuyaheshimu.

"Natambua ni maoni yake; nayaheshimu. Kama kuna lolote tutatue kwa misingi ya sheria," alisema Ngeleja alipozungumza katika hafla ya kampuni ya Songas ya kutimiza miaka mitano iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Serikali ilifanya uamuzi kama huo mwaka 1967 wakati wa Azimio la Arusha, ilipotaifisha mali binafsi na kuziweka chini ya miliki ya umma, uamuzi ambao ulikasirisha wawekezaji wengi ambao waliamua kuondoka nchini.

Mbali na mali za wawekezaji, serikali pia ilitaifisha mali za taasisi mbalimbali za kijamii na kidini.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar