Sumaye ahamasisha wabunge kuendelea kuibua hoja
BAADA ya kimya cha muda mrefu, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ameibuka kuunga mkono mijadalaNa inayotokea bungeni na kuwataka wabunge waendelee kuibua hoja zaidi kwa manufaa ya taifa.
Kauli hiyo ya Sumaye imetolewa wakati tayari kuna mgawanyiko miongoni mwa wabunge, huku baadhi wakionekana kuwa mashujaa na wapambanaji wa ufisadi, wengine wakipinga na kutaka wachukuliwe hatua.
Hali hiyo imesababisha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kuunda kamati ndogo ya watu watatu wenye hekima chini ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, kufuatilia mwenendo wa wabunge na wanachama wake wanaoonekana kwenda kinyume na matakwa ya CCM.
Kabla ya kuundwa kwa kamati hiyo katika mkutano wake wa hivi karibuni mjini Dodoma, NEC ilimhoji Spika wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta kwa maelezo kuwa amekuwa akiruhusu mijadala inayoikosoa serikali na CCM.
Spika Sitta amekuwa akitajwa kama kiongozi wa kambi ya wabunge wa CCM bungeni, ambao wamekuwa wakijipambanua kama makamanda wa vita ya ufisadi baada ya matokeo ya Ripoti ya Uchunguzi ya Bunge kuhusu mkataba wa Richmond, ambayo ilimfanya Edward Lowassa, kujiuzulu mwezi Februari mwaka jana.
Wabunge wengine waliopo katika kundi hilo ni Mbunge wa Same Anne Killango, Mbunge wa Kyela Dk Harrison Mwakyembe na Lucas Selelii wa Nzega. Wengine ni Christopher Ole Sendeka wa Simanjiro na James Lembeli wa Kahama.
Hata hivyo, CCM ilieleza kugundua kuwepo kwa chuki miongoni mwa wabunge wake ndani ya bunge na Rais Kikwete akizungumzia hilo kwenye mazungumzo yake ya moja kwa moja na wananchi Septemba, mwaka huu.
CCM imeipa kamati ya Mwinyi ambayo wajumbe wake ni pamoja na Abdulrahman Kinana na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa kuchunguza kiini cha chuki miongoni mwa wabunge hao.
Akizungunza na Mwananchi Jumapili hivi karibuni, Sumaye alisema mijadala hiyo iendelee na kuwataka wabunge kutoogopa kuibuaĆ bungeni mijadala yenye masilahi ya taifa kwa sababu kufanya hivyo ni kukuza demokrasia nchini.
Sumaye alisema kuwa kutokea kwa mgongano wa mawazo baina ya wabunge ni hali ya kawaida na kwamba, hata lingekuwa bunge la chama kimoja, hali hiyo ingeweza kutokea kwa kuwa kila mmoja ana mawazo tofauti na mwingine.
"Mijadala na migongano ya mawazo bungeni ni jambo la kawaida, hata kama lingekuwa bunge la chama kimoja ingeweza kutokea.
Hali ya namna hiyo ni kukua kwa demokrasia hivyo sioni mantiki ya wabunge kuacha kufanya hivyo, nawashauri waendelee," alisema Sumaye.
Mwanasiasa huyo ambaye alishikilia nafasi ya Uwaziri Mkuu kwa kipindi kirefu zaidi ya wote enzi za utawala wa awamu ya tatu wa Rais Benjamin Mkapa, alibainisha kuwa anapoliangalia bunge la Tanzania anaona kuna dalili ya kugawanyika.
"Ninapoliangalia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naona kuna kila dalili ya baadhi ya wabunge kugawanyika," alisema Sumaye.
Alipoulizwa kama anafahamu kuwepo kwa baadhi ya wabunge ndani ya CCM wanaolalamikiwa kwa vitendo vya ufisadi na wananchi wa majimbo yao alisema: "Sifahamu kama kuna wabunge mafisadi walio ndani ya CCM".
Kuhusu kuwepo baadhi ya wabunge wa chama tawala kulalamikiwa kwa kushindwa kuwaletea maendeleo kama walivyoahidi, pia Sumaye alisema haamini kuwepo kwa jambo kama hilo.
Hata hivyo alisema iwapo kuna wabunge wameshindwa kuwaletea maendeleo wananchi, CCM isihusishwe na kushindwa kazi kwa wabunge hao.
Alisema kuwa wabunge wasiotimiza wajibu wao watahukumiwa na wananchi wenyewe kwa njia ya kura na kwamba, CCM bado ni imara katika kila nyanja.
Kama kuna mbunge hajatimiza ahadi zake basi hilo litakuwa tatizo lake na siyo la chama. Chama hakihusiki," alisema Sumaye.
Akizungumzia mustakabali wake kisiasa, Sumaye ambaye alikuwa Mbunge wa Hanang mkoani Manyara alisema tofauti na mawazo ya wengi kuwa yeye anataka kurejea katika siasa, lakini ukweli ni kuwa hatarajii kufanya hivyo.
"Pamoja na uwepo wa minong'ono kuwa nataka kurejea katika siasa na kugombea tena ubunge Jimbo la Hanang, habari hizo siyo za kweli. Sitarajii kuingia tena katika siasa zaidi ya kuwa mshauri endapo nitahitajika kufanya hivyo kwenye CCM," alisema Sumaye.
Alifafanua kuwa yeye alistaafu wakati bado anahitajika na wananchi wa Hanang pamoja na Watanzania kwa ujumla, pia bado ana afya njema itakayomwezesha kuendelea kuwatumikia wananchi na kusisitiza kwamba, hajawahi kufikiria kurejea katika siasa zaidi ya kujikita katika kilimo nyumbani kwake.
Hata hivyo Sumaye aliyekuwa mmoja wa wagombea kumi na moja wa nafasi ya urais mwaka 2005 ndani ya CCM na kuangushwa na Rais wa sasa Jakaya Kikwete alisema: "Si dhambi kwa kiongozi yeyote aliyestaafu kutamani na kurejea tena katika siasa kwani hajavunja sheria za nchi na pia kila mtu ana mtazamo wake katika muktadha wa kisiasa".
"Mimi nimestaafu siasa wakati bado nahitajika na wananchi wa Hanang na Watanzania kwa ujumla, lakini sitarajii kurejea tena katika siasa. Kama nitahitajika kutoa mchango wangu wa mawazo nipo tayari ili kuijenga nchi yetu," alisema Sumaye.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar