Sabtu, 15 Agustus 2009

Kanisa Katoliki sasa lamkabili Kingunge

KIONGOZI WA KANISA KATOLIKI NCHINI TANZANIA Polycarp Kardinali Pengo

KANISA Katoliki nchini limekataa rai iliyotolewa na mwanasiasa mkongwe na Mbunge wa Kuteuliwa, Kingunge Ngombale-Mwiru (CCM) ya kulitaka limuombe radhi kwa madai ya kumkashifu kwa kumwita fisadi.
Msimamo huo ulitangazwa jana na Msemaji wa Baraza la Maaskofu Kanisa Katoliki (TEC), Padre Modest Katonto wakati alipofanya mahojiano ya ana kwa ana na waandishi wa habari wa gazeti hili. Baraza hilo linaongozwa na Askofu Yuda Thadei Ruwaich.
Padre Katonto alikanusha madai yaliyotolewa na Kingunge wakati akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam juzi kuwa, kanisa lilipata kumwita fisadi kutokana na msimamo wake wa kuupinga waraka wao unaohimiza waumini wake kuchagua viongozi waadilifu.
Badala yake kiongozi huyo alimtaka Kingunge kuchukua uamuzi wa kwenda mahakamani iwapo anao ushahidi na anaamini kwa dhati kuwa, kanisa lilipata wakati wowote kumkashifu.
“Waraka umejieleza wazi wazi kuwa kiongozi atakayechaguliwa, anatakiwa kuwa mwadilifu, bila kujali itikadi ya chama wala dini. Tulichosema anayepinga kuchaguliwa kwa kiongozi mwadilifu na mkweli ana harufu ya ufisadi. Iwapo Kingunge anaona amekashifiwa na ana ushahidi, basi anayo haki ya kushitaki,” alisema padre huyo kwa kujiamini.
Aliendelea kueleza kuwa, kanisa haliwezi kunyamazishwa na mtu au taasisi yoyote kama lisivyotaka kumnyamazisha mtu mwingine yeyote kutoa maoni yake.
“Siasa ni ‘property’ (mali) ya nani? Na ipo kwa ajili ya nani? Haya ndiyo maswali ambayo najiuliza, huku ni kuwanyamazisha watu wengine wasizungumze.
“Ukishaanza kusema wewe usizungumze, yule asiongee, ni kuvunja katiba ya nchi, unapoanza kuwanyima baadhi ya watu wasijishughulishe na siasa, maana yake unafikiri kuwa siasa ni mtaji au ni kwa ajili ya watu fulani au kwa ajili ya viongozi. Hayo ni makosa,” alisema Padre Katonto.
Mbali ya kusisitiza kwamba, hawataki kuingia katika malumbano na mwanasiasa huyo mkongwe au mtu mwingine yeyote, padri huyo alisema, kanisa haliwezi kamwe kutishwa na kauli za wananasiasa kwani kanisa ni jamii, na jamii inaongozwa na katiba ya nchi.
“Waraka umeshatoka, ni jukumu la watu kuusoma na kujadili, ni kama changamoto. Watu wapo huru kutoa maoni kama watakavyo kama wanavyoutazama, na hilo ndilo lengo letu.
“Nasema tena, hakuna mtu mwenye uwezo wa kumnyamazisha mtu mwingine, huu ni udikteta kutaka kuwanyamazisha watu kwa kutumia nguvu au madaraka. Sioni kama Kingunge ana haki au nguvu ya kuliambia kanisa nyamaza.
“Nikiangalia maneno ya wanasiasa wote waliojitokeza kuupinga waraka pamoja na Kingunge mwenyewe, hakuna mahali ambapo wanaonyesha au kujenga hoja kuwa kuna ubaya wa waraka huu. Ni kelele tu... ni maoni tu ya kutaka kupotosha na kusema waraka ni mbaya,” alisema padri huyo.
Alisema kanisa linamshughulikia mtu mzima kimwili na kiroho, haliwezi kumwacha muumini wake mwenye roho safi akae katika mazingira machafu na ya kuteseka, kwani hata vishawishi vya dhambi vinatokana na maisha kuwa magumu.
“Hakuna kiongozi ambaye yupo tayari kuona watu wake anaowaongoza wakinyanyasika. Huwezi kutenganisha maisha ya kiroho na ya kimwili, huwezi, ni lazima vitu vyote viende pamoja,” alisema msemaji huyo wa TEC.
Alisema kanisa limeshangazwa na kelele za baadhi ya wanasiasa wa wakati huu, wanaojitokeza kuupinga waraka huo wakati limekuwa likitoa nyaraka kadhaa mara kwa mara.
“Tumetoa huduma nyingi za kimwili kwa Watanzania bila kujali itikadi na imani zao, sambamba na nyaraka na miongozo inayoongoza huduma hizo, mfano afya, elimu, maji, upatikanaji wa haki kisheria na mengine, lakini utashangaa hakuna kiongozi aliyekuwa akipinga wala kusema kuwa kanisa kutoa huduma hizo ni kuingilia siasa za nchi, lakini tunapotoa waraka wa kumwelimisha mwananchi namna ya kudai haki zake, vita inakuja hapo,” alisema.
Aidha, alipinga madai mengine ya Kingunge kuwa, waraka wao unalenga kuwadhibiti na kuwalazimisha Watanzania kuwachagua viongozi fulani akisema, hakuna mahali penye msisitizo wa namna hiyo.
Alisema badala yake, waraka huo unalenga kuwapa raia wenyewe nguvu za kumhoji, kumuuliza hata kumwajibisha kiongozi wao kwa yale aliyoahidi na ambayo hakuyatekeleza.
“Nia ya maaskofu ni kuwapa raia wenyewe nguvu ya kuwahoji watawala wao, juu ya utekelezaji wa ahadi zao. Watu watakuwa na uwezo wa kuwadhibiti watu kwa kutoa elimu ya uraia na si kwa kutumia jeshi na vifaru,” alisema.
Aliongeza kuwa, kwa sasa kanisa linaona kama hoja hiyo ya waraka imegeuzwa na baadhi ya watu na kufanywa ya kulijadili kanisa, jambo alilosema si zuri.
Majibu hayo ya kanisa yamekuja baada ya Kingunge, kulitaka kanisa kumuomba radhi, ikiwa ni pamoja na kupinga hatua ya kuandaa waraka huo, akisema uamuzi huo unaweza kuliingiza taifa katika mgawanyiko wa kidini, na hivyo kuharibu misingi ya umoja na mshikamano iliyojengwa na waasisi wa taifa hili.
Kingunge ambaye mwenyewe alitamba kuwa miongoni mwa watu walioijenga misingi hiyo iliyokuwa ikizuia masuala ya dini kuhusishwa na siasa, alilitaka Kanisa Katoliki kutafakari upya uamuzi wake huo na akayaasa madhehebu na watu wa imani tofauti kutofuata mkondo huo.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar