Senin, 24 Agustus 2009

Nitapambana na mafisadi hadi kifo

PIKA wa Bunge, Samuel Sitta amesema kamwe hawezi kutetereka katika maamuzi yake, kwa kuwa anaamini kuwa Mungu yuko naye katika kila jambo jema analolifanya.

Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara ulioandaliwa na wenyeviti wa makanisa ya Mkoa wa Tabora, katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora jana, Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Magharibi, alisema hatatetereka katika maamuzi yake kwa kuwa anaamini anayatekeleza kwa nia njema.

"Katika maamuzi ninayochukua daima ninaamini kuwa ni mambo mema na ninajua kuwa Mungu peke yake ndiye anayenilinda, kwa hivyo sitatetereka hata kidogo,"alisema Spika Sitta ambaye siku za nyuma aliapa kupambana na mafisadi hadi ushidi upatikane.

Alisema hivi sasa kumeibuka tabia ya baadhi ya watu nchini, kulazimisha yale wanayoyafanya wao yaonekane kuwa ndiyo ya ukweli kabisa hata kama wanayoyafanya ni ya uongo.

"Katika nchi yetu kumeibuka tabia ya waovu wanaosambaza uongo uliopakwa asali, hugeuza uongo huo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo, siwezi kukubaliana nao sababu ni waovu,"alisisitiza kauli ambayo imetafsiriwa kuwa anawalenga wale ambao walitaka avuliwe uanachama wa CCM katika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mkewe ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Margaret Sitta, ambaye alinukuu kauli ya Askofu Norbert Mtega wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Songea, ambaye alisema kuwa maisha ni mpito na kifo ni faida, alipokuwa akizungumza katika msiba wa baba wa Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama.

"Kauli ile ya Askofu Mtega tunaichukua na sasa tunaifanya kuwa falsafa ya maisha yetu, kwa maana hiyo kwetu sisi sasa maisha ni mpito tu na kifo kwetu ni faida,"alisema waziri huyo.

Kwa upande wake mume wake (Sitta) alisema taifa linaelekea kubaya kwa sababu baadhi ya watu wanajaribu kulazimisha yale wanayoona kuwa ni sawa na kwamba wanatumia gharama kubwa kufanya hivyo.

Mwenyekiti wa umoja wa makanisa mkoani Tabora, William Lusito, alisema umoja huo umetokana na azimio kuwa nyuma ya Spika na kwamba, hawatakubali kumuona akiyumbishwa na kundi la aina yoyote.

Spika huyo pia alielezea kusikitishwa kwake juu ya hatua ya baadhi ya watu, kusambaza maeneo yasiyokuwa na ukweli kuhusu yeye, wakidai kuwa aliomba radhi kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC).

Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, aliyasema hayo jana nyumbani mjini Urambo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, akiwa katika ziara yake aliyoianza rasmi jana.

Mamia ya watu wa jimbo hilo, walijitokeza kwa wingi kumlaki mbunge wao.

"Kwa kuwa mimi niliwekwa katika kikao cha kujieleza, mimi ninarudisha swali kwa hao wanaosambaza hayo, waeleze niliomba radhi kuhusu kipi,"alisema.

Alisema hataki kuzungumzia yaliyotokea ndani ya kikao, lakini kwa kuwa kuna watu wamejitokeza kuzungumzia hayo, kuna haja kwa watu hao kueleza sababu za yeye kuomba radhi katika kikao cha siku mbili cha NEC.

"Ninachokisema ni hivi, kwa kuwa kikao cha NEC kimefikia mwisho na chama chetu kikatoa maamuzi ya kuunda jopo la watu watatu wenye busara wakaangalie hali ya Bunge letu, watawahoji wabunge, wanachama na kisha tutayasikia maamuzi yao Oktoba basi ni bora tusubirie matokeo yao,"alisema.

Alisema yeye kama mtu mwenye subira atakuwa mtu wa ajabu mno, kuzungumzia yaliyotokea ndani ya kikao cha NEC na CC na kwamba, kauli na maelezo yanayotolewa na baadhi ya watu kutaka kubadilisha picha halisi ya kile kilichotokea ni upotoshaji na inasikitisha.

"Nasikitishwa na makao makuu ya CCM Dodoma kwa ambavyo wanavyoshughulikia baadhi ya mambo, kwani ingekuwa kwa mara moja, kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Kapteni John Chilligati, ilitosha kumaliza mambo.

Alisema, hata hivyo, inashangaza kuona mambo hayo yanarudiwa wakati yanapaswa kushughulikiwa na na kamati maalumu.

"Inashangaza kuona mara anazungumza Katibu Mkuu, mara anazungumza mwanachama tu wa CCM, tena mambo ambayo ni dhahiri yanayoonekana kuwa ni tuhuma bila ya kuacha vyombo vilivyoundwa na chama vifanye maamuzi yake," alisisistiza Sitta.

"Nimesikitishwa na wakuu wa chama ambao waliruhusu, Chenge (Andrew) na Lowassa (Edward) wapokelewe, lakini wanazuia katibu na mwenyekiti wasinipokee, ingawa wanachama walijitokeza kunipokea, hii ndiyo inatufanya wanachama tuamini kuwa kuna wanachama wenye haki na wasio na haki, hii si dalili nzuri,"alisema.

Alielezea kushangazwa na hatua ya makao makuu ya CCM ya kuuzuia uongozi wa mkoa wake usimpokee.

Alisema hivi karibuni amesikia kauli zilizotolewa na viongozi wakuu wa CCM zikionyesha kuegemea upande mmoja, jambo ambalo si dawa na linaonekana kutotumika kwa busara katika wakati huu ambapo kikao cha NEC kimemalizika .

Hata hivyo, aliwashukuru wanachama wa CCM wa Jimbo la Urambo Magharibi, waliojitokeza kwa wingi kumlaki na akawataka kutokata tamaa na waendelee na moyo huo.

Kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kuwa amekuwa akiendesha Bunge kwa kuwapanga wabunge, alikanusha na kwamba, utaratibu wa Bunge unafahamika.

"Vikao vya Bunge vinaendeshwa kwa taratibu na kanuni, kila mbunge anayetaka kuchangia anapitisha hoja zake kwanza kwa Katibu wa Bunge na au kutoa taarifa kwa katibu huyo, hivyo hakuna ukweli wowote kwamba nimekuwa nikipanga mambo,"alisema.

Spika Sitta juzi huko Urambo alipata mapokezi makubwa baada ya kuwasili jimboni humo ikiwa ni mara ya kwanza tangu apate msukosuko kutoka kwenye vikao vya chama chake.

Mwandishi wetu aliyekuwa huko, alisema Sitta alipokelewa na wapigakura wake wakiwa na pikipiki zaidi ya 100 na kutembea naye kwa maandamano kwa umbali wa kilometa moja.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar