Minggu, 15 Februari 2009

Mkapa, Bunge mambo kuchemka tena....

SERIKALI imebanwa na Bunge, kiasi cha kulazimika kuanza kufikiria uamuzi wa kisheria na hata kutafakari fursa ya kumwondolea kinga Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, au kutafuta uwezekano wa kumhoji kuhusu mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira mkoani Mbeya, anaodaiwa kuwa mmoja wa wamiliki, kupitia kampuni ya ANBEN.
Mbinyo huo wa Bunge dhidi ya Serikali unatokana na kile kinachoelezwa kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kunasa nyaraka zinazobainisha kuwa Rais Mstaafu Mkapa ni mmoja wa wamiliki wa mgodi wa Kiwira, nyaraka ambazo baadaye zilifanyiwa mabadiliko ili kumwondoa Mkapa katika wingu hilo.
Nyaraka hizo ambazo Raia Mwema imefanikiwa kuziona zinabainisha kuwa Mkapa pamoja na mkewe Anna ni wamiliki wa hisa katika mgodi wa Kiwira kupitia kampuni yao ya ANBEN. Hata hivyo, kutokana na mwenendo wa mambo na hasa baada ya suala hilo kuonekana kumweka pabaya kisiasa na kisheria Mkapa, umiliki wa mgodi huo ulifanyiwa mabadiliko.
Rais Mstaafu Mkapa
Katika mabadiliko hayo, nyaraka za sasa zinabainisha kuwa mgodi huo unamilikiwa na kampuni ya Tanpower Resources Ltd, ambayo ni muungano wa kampuni nne tofauti.
Kampuni hizo ni Fosnick Ltd, ambayo wanahisa wake ni Nick Mkapa, Foster Mkapa na mwingine aliyetambuliwa kama B. Mahembe, kampuni nyingine ndani ya mwavuli wa Tanpower Resources ni Choice Industries ambayo wanahisa wake ni Joe Mbuna na Goodyear Francis, nyingine ni Devconsult Ltd yenye wanahisa D. Yona na Dan Yona jr, wakati kampuni ya nne ni Universal Technologies Ltd ambayo wanahisa wake ni Wilfred Malekia na Evans Mapundi.
Raia Mwema imedokezwa kuwa tayari nyaraka za awali (original) zenye kuonyesha kuwa mgodi wa Kiwira unamilikiwa na kampuni ya ANBEN ambayo ni ya Mkapa, zimefikishwa katika uongozi wa juu wa Bunge.
Kwa mujibu wa habari za uhakika zilizotufikia inaelezwa kuwa nyaraka hizo zimejitosheleza kiushahidi kwamba Mkapa ni mmiliki wa ANBEN kampuni ambayo inahusika katika umiliki wa mgodi wa Kiwira.
Kutokana na hali hiyo na hasa kile kinachobainika kuwa Bunge kupitia Kamati yake ya Nishati na Madini kuridhishwa na ushahidi katika nyaraka hizo, muhimili huo wa Taifa umedhamiria kuibinya Serikali katika mambo makuu mawili.
Jambo la kwanza ni kushinikiza mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira kurejeshwa serikalini kutokana na sababu kadhaa lakini kubwa zaidi ni wawekezaji wanaopaswa kuendesha mgodi huo kubainika kuwa ni wababaishaji walioshindwa kutekeleza ahadi zao kwa Serikali.
Kati ya mambo yanayodhihirisha kuwa mwekezaji huyo kushindwa kuendesha mradi wa uzalishaji umeme kwa kutumia makaa ya mawe katika mgodi huo ni kushindwa kuwalipa stahili zao wafanyakazi wa mgodi, ambao hadi Kamati ya Bunge inatembelea mgodi huo katikati ya Januari mwaka huu, walikuwa wakidai mishahara mipya iliyotangazwa na Serikali kwamba kima cha chini kwa sekta ya madini ni Sh 350,000.
Pia kamati hiyo ilibainika kuwa mwekezaji huyo alishindwa kulipa mishahara waliopanga ambayo ni kima cha chini kuwa Sh 60,000 kwa muda wa miezi takriban nane sasa.
Lakini kubwa zaidi ni wawekezaji hao kushindwa kuzalisha umeme kwa mujibu wa makubaliano kati ya kampuni hiyo na Serikali kupitia TANESCO. Kabla ya kubinafsishwa mgodi huo ulikuwa ukizalisha megawati 6 zilizokuwa zinaingizwa katika gridi ya taifa, lakini baada ya kampuni ya TanPower Resources Ltd kupewa mgodi walitakiwa wazalishe megawati 200 katika awamu mbili.
Awamu ya kwanza ilikuwa izalishe megawati 50 ifikapo Julai 2007 na uzalishaji wa megawati 150 zilizosalia ukamilike Machi, mwaka huu. Taarifa za uhakika zinabainisha kuwa hakuna chochote kilichofanyika hadi sasa na hasa ikizingatiwa kuwa awali umeme ulikuwa ukisambazwa na kutumika katika wilaya za Kyela, Ileje na Rungwe.
Kwa sasa inaelezwa kuwa uzalisha umeme katika mgodi huo umeshuka kutoka megawati 6 za awali kabla ya ubinafsishaji hadi megawati moja na hivyo kusababisha matatizo ya umeme katika wilaya hizo tatu. Sababu hizi na nyinginezo ndizo chanzo cha Bunge kuweka shinikizo mgodi huo urejeshwe serikalini kutoka mikononi mwa mwekezaji huyo.
Jambo la pili ambalo Bunge limekusudia kufanya ni kuishinikiza Serikali kumhoji Mkapa au hata kufungua milango ya kumwondolea kinga ya kushitakiwa. Kama Serikali itashindwa kuridhia kufungua milango ya kumwondolea kinga ya kushitakiwa, basi Bunge limekusudia kuweka shinikizo kwamba Mkapa ahojiwe ili akiri au la kuliko kuacha mambo yabaki ‘hewani’ kama nchi haina uongozi.
Kwa mujibu wa tathmini ya mwaka 1998, mgodi ulikuwa na thamani ya Sh bilioni 4.2, wakati tathmini iliyowahi kufanywa mwaka 1991 na Taasisi ya Ardhi inaonyesha kuwa mgodi ulikuwa na thamani ya Sh bilioni saba.
Lakini katika ziara yake Januari mwaka huu, mgodini hapo, Kamati ya Bunge ilibaini kuwa pamoja na tathmini hiyo kufanyika, licha ya kwamba ilifanyika miaka mitano kabla ya kubinafsishwa, kamati ilishindwa kuelewa ni vigezo gani vilitumika kutupilia mbali uthamini huo na kuamua kuuza hisa kwa gharama ya Sh milioni 700 tu.
Habari zaidi zilizotufikia zinaeleza kuwa wakati wa ziara hiyo, Kamati hiyo ya Bunge ilipokea taarifa mbili zinazogongana kuhusu umiliki wa hisa za mgodi huo. Kilichobainika ni kwamba taarifa ya mwekezaji kudai kuwa amenunua hisa asilimia 70, Serikali asilimia 12 na nyingine asilimia 18 hazijanunuliwa.
Taarifa hiyo inadaiwa kugongana na ile ya wafanyakazi iliyotolewa kwa Kamati hiyo ya Bunge. Taarifa hiyo ya wafanyakazi inaeleza kuwa mwekezaji anamiliki asilimia 85 na Serikali asilimia 15.
Kutokana na mkanganyiko huo, kamati hiyo ilitoa taarifa yake iliyobainisha kuwa wajumbe wa kamati wameshindwa kuelewa juu ya utata wa umiliki huo wa hisa na wamelazimika kukusudia kuiomba Serikali ieleze wazi kuwa inamiliki hisa asilimia ngani.
Kubwa jingine lililogunduliwa na Kamati hiyo ya Bunge mgodini Kiwira ni taarifa ya mwekezaji kuonyesha kuwa Serikali ilitenga Sh bilioni 17 kwa ajili ya ukarabati, kabla ya ubinafsishaji kufanyika lengo likiwa ni kukarabati mitambo yote ya uzalishaji iliyotajwa kuwa ilikuwa imechakaa.
Hata hivyo, kamati ilipigwa na butwaa baada ya kuelezwa na wafanyakazi kuwa hakuna ukarabati wowote uliofanyika na zaidi ni kwamba jenereta moja ya kuzalisha umeme imechakaa na haifanyi kazi, wakati jenereta ya pili ina uwezo wa kuzalisha si zaidi ya megawati moja tu.
Mgodi wa makaa ya mawe Kiwira uliopo katika wilaya tatu za Rungwe, Ileje na Kyela, ulianzishwa kwa msaada wa kifedha na ufundi kutoka Jamhuri ya Watu wa China na ulizinduliwa rasmi na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Novemba mwaka 1988.
Mgodi huo unatajwa kuwa na uwezo wa kiusanifu wa kuzalisha makaa ghafi ya tani 150,000 kwa mwaka. Kiwango hicho cha uzalishaji hata hivyo kinaweza kuongezwa hadi tani milioni moja kwa mwaka. Makaa hayo hutumika kuzalisha umeme.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar