Selasa, 17 Februari 2009

pongezi JK kwa kuifufua TTCL...

Serikali imechukua hatua za kuifufua Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ikiwa ni pamoja na kuipa dhamana kuiwezesha kukopa fedha za kujiendesha kutoka taasisi za fedha nchini.

Pia imeamua kuwa kampuni hiyo ndiyo itakayosimamia matumizi ya Mkongo wa Taifa ambao unalenga kuboresha matumizi ya teknolojia katika uchumi na maendeleo ya jumla ya Tanzania.

Mkongo wa Taifa, ambao utajengwa kwa fedha za mkopo kutoka Jamhuri ya Watu wa China, ikiwa ni moja ya mafanikio ya ziara ya siku tatu ya Rais wa nchi hiyo, Hu Jintao, ambaye aliondoka nchini juzi, utagharimu dola milioni 180 za Marekani.

Uamuzi huo ulifikiwa leo katika mkutano kati ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na mashirika yaliyoko chini ya wizara hiyo, Ikulu, Dar es Salaam. Mkutano huo ni mfululizo wa mikutano kati ya Rais na wizara na mashirika yaliyoko chini ya wizara hizo, inayolenga kutathmini utendaji wa serikali katika miaka mitatu iliyopita.

Kwenye mkutano huo wa leo, ilielekezwa kiundwe kikosikazi cha kuharakisha ujenzi wa mkongo huo, kujadili na kutoa mapendekezo jinsi utakavyotumika kunufaisha uchumi na hivyo kutumika katika maendeleo ya jumla nchini.

Katika mkutano huo uliozungumzia masuala mbalimbali, vilevile serikali imekubali kubeba madeni yote ya Shirika la Posta Tanzania (TPC), ili kuliwezesha kujiendesha kwa kukopa fedha kutoka taasisi za fedha, ikiwa ni moja ya hatua za kupambana na changamoto za ushindani katika dunia ya sasa ya teknolojia mpya.

Kuhusu Shirika la Posta, mkutano ulielezwa jitihada za serikali katika kulisaidia kwa kusafisha hesabu zake kwa kuchukua dhamana ya madeni yaliyokuwa yanalikabili. Serikali ndiye mmiliki mkubwa zaidi wa hisa za shirika hilo, kwa kuwa na asilimia 41.

Kuhusu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), walikubaliana kuwa ipo haja ya kuharakisha utungwaji wa sheria ya kusimamia na kudhibiti matumizi ya simu za mkononi na intaneti, na pia kufunga mitambo ya kukomesha wizi wa simu za mkononi.

“Lazima tujenge nidhamu haraka katika matumizi ya simu na intaneti … si huduma hizo kutumika kutukanana … kwamba kila mtu mwenye mtu wa kumtukana, basi kila akiamka asubuhi, kazi yake ni kumtukana mtu huyo kwa kutumia simu ama intaneti,” alisema Kikwete. Wakati huohuo, kupitia mkutano huo, ilikubaliwa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) iongezwe bajeti ya kufanya utafiti mbalimbali nchini, bajeti ambayo kwa sasa ni ndogo, asilimia 0.3 ya bajeti nzima ya serikali ya kila mwaka.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar