Selasa, 03 Februari 2009

TANZANIA KUJENGWA BARABARA KAMA HIVI..

Maeneo ya kujenga barabara za juu Dar yatajwa Bungeni Na mwandishi wetu toka DODOM


SERIKALI imelihakikishia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba mpango wa kujenga barabara za juu (fly over) kwenye makutano mbalimbali jijini Dar es Salaam unaendelea vizuri.

Naibu Waziri wa Miundombinu , Hezekiel Chibulunje aliliambia bunge jana mjini hapa kuwa, maandalizi yote ya awali yamekamilika, na kwamba kinachosubiriwa ni kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Alisema hata agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa hivi karibuni jijini Dar es Salaam litakwenda sambamba na ujenzi wa barabara zingine ndani ya jiji.

Alisema kazi ya awali, ikiwemo michoro tayari imekwishanza sambamba na kuwekwa kwa alama katika maeneo husika.

Chibulunje alisema Shirika la Ushirikiano la Japani( JICA) liliisaidia Serikali kwa kufanya uchunguzi wa namna ya kutengeneza mpango wa usafiri jijini(City Transport Master Plan) na kwamba uchunguzi huo ulipendekeza baadhi ya makutano ya barabara jijini yawe na barabara za juu.

Aliyataja makutano ya barabara yaliyopendekezwa kuwa na barabara za juu kuwa ni makutano ya Ubungo, Magomeni, Jangwani(Fire), kamata, Tazara na makutano ya Nyerere na Kawawa (Chang’ombe) ambapo alibainisha kuwa kwa sasa serikali inapitia ushauri huo.

Kuhusu barabara za katikati ya Jiji , Naibu Waziri, alisema Serikali imetenga Sh 20 bilioni kwa ajili ya kuzijenga kwa kiwango cha lami ili kupunguza msongamano wa magari na kuwezesha kuwa na ubora unaotakiwa.

Alizitaja barabara zinazohusika kuwa ni pamoja na barabara ya Kigogo-Jangwani-Jengo la Club ya Yanga (km.9.6), Tabata-Dampo-Kigogo, Ubungo-Maziwa-External na Old Bagamoyo (Morocco-JKT Mlalakuwa).

Nyingine ni TPDC, Mbezi (Morogoro road-Malamba mawili-Kinyelezi-Banana, Jet mwisho,Tangi bovu-Goba, Kimara Baruti-Msewe- Changanyikeni na barabara ya Kimara –Kirungule-External (Mandela) ambazo alisema kuwa zote ziko katika hatua mbalimbali za usanifu wa kina kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Alikuwa akijibu swali la Charles Keenja (Ubungo CCM) aliyetaka kujua ni nini kinasababisha kero ya msongamano wa magari katika barabara ya Ubungo na nini ufumbuzi wa jambo hili na lini.

Keenja pia alitaka kujua mipango ya Serikali kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam hususani kwenye makutano ya barabara za katikati ya Jiji.

Hata hivyo, Naibu Waziri alitoa sababu nyingine kuwa msongamano huo unatokana na idadi kubwa ya magari ya watu binafsi hali inayotokana na kipato cha Mtanzania kukua na kuwezesha watu wengi kumiliki magari tofauti na ilivyokuwa mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Alisema mikakati itakayosaidia kupunguza msongamano huo ni pamoja na mabasi yaendayo kasi na upanuzi wa barabara muhimu kama vile Sam Nujoma,barabara za Kilwa na Mandela ambazo shughuri zake zinaendelea.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar