Sabtu, 30 Mei 2009

Wazungu wamwaga Sh milioni 120 kwa Simba



KLABU ya daraja la kwanza ya Norway imesema ipo tayari kutoa kitita cha dola 120,000 (kama zaidi ya Sh milioni 120) kwa Simba ili kuwasaijili wachezaji wake wawili, Henry Joseph na Emeh Izuchukwu.

Izuchukwu raia wa Nigeria tayari yupo Norway akiendelea kufanya mazoezi na timu hiyo yenye makao yake makuu katika Manispaa ya Kongsvinger IL.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa uongozi wa Kongsvinger upo tayari kutoa kitita cha dola 70,000 kwa Izuchukwu na dola 50,000 kwa Henry kuwasajili kwa msimu ujao wa ligi.

"Unajua weyewe wameona Emeh bado kijana, hivyo watatoa dola 70,000 na Henry dola 50,000. lakini hata hivyo wametakiwa kusubiri kidogo kwa kuwa Simba walikuwa na makubaliano mengine na klabu ya Molde FK kupitia wakala anayetambulika na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Mehd Rehmtullah.

"Unajua huenda wale Molde FK wakatoa fedha zaidi, ndio maana uongozi wa Simba unaendelea kuvuta subira, umetoa muda kidogo kuisubiri hiyo timu ya kwanza ili kujua uamuzi wake.

"Hata hii timu nyingine (Kongsvinger) iliwaona wakati wakifanya majaribio na Molde FK ambao wanasubiri kuanza kwa kipindi cha usajili ili waseme wanatoa kiasi gani halafu Simba itaamua," kilieleza chanzo.

Imeelezwa kuwa wakala, Rehtmtullah ndiye aliyewashauri Simba kuwapa nafasi Emeh na Henry kwenda kufanya mazoezi na Kongsvinger ili ikiwezekana watoe dau au kama hata si wao, klabu nyingine za Norway ziwaone kama ambavyo waliweza kuonekana wakiwa na Molde FK.

"Kweli nilishauri iwe hivyo kwa kuwa watu hao wameonyesha nia ya kutaka kuwasajili kama itakuwa inawezekana. Nikaona ni wazo zuri ndiyo maana tumetoa nafasi kwa Henry amalize majukumu ya taifa halafu akaungane na Emeh," alisema Rehmtullah alipozungumza na Mwanaspoti.

Lakini alipoulizwa suala la ofa waliota Wanorway hao alisema; "ameonyesha kweli wanawataka, wametoa ofa naweza kusema si mbaya kwa kuanzia lakini hili si suala langu na wanaoweza kulizungumzia ni Simba wenyewe," alisema wakala huyo.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Kassim Dewji alisema wanafanya mambo yote kwa wakati mmoja. Tunazungumza na timu ya sasa na pia tunasubiri ile ya awali.

"Kuna wakala na tunashulikia mambo yote kupitia yeye, hivyo tusingependa kuchanganya mambo kwanza kwa kuwa bado kuna mazungumzo. Tukijua kila kitu kwa uhakika basi mara moja tutawaeleza," alisema Dewji.

Timu ya Kongsvinger, si timu kubwa sana na inatokea kwenye manispaa ndogo ya Kongsvinger iliyo Kusini Mashariki mwa Norway. Ilianzishwa Januari 31 mwaka 1892 na inatumia jezi za rangi nyekundu na nyeupe ikiwa nyumbani au bluu tupu ukiwa ugenini.

Haijawahi kutwaa ubingwa wa Norway zaidi ya kushika nafasi ya pili na ya tatu na miaka kadhaa haijawahi kuwa na wachezaji kutoka Afrika, badala yake mwaka huu kikosi chake kinaundwa na wachezaji wengi wenyeji na wageni wachache kutoka nchi jirani za Sweden, Luxembourg na Colombia kutoka Amerika Kusini.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar