Rabu, 11 November 2009

Dk Slaa awatimua maswahiba wa Zitto

Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbrod Slaa ambaye jana alitangaza kuwavua uongozi viongozi wawili wa kitaifa,huku hatua hiyo ikipingwa na Naibu katibu mkuu wake Zitto Kabwe

NI VIONGOZI WAWILI WA KITAIFA. ZITTO APINGA VIKALI

Ramadhan Semtawa na Fidelis Butahe

HATIMAYE yule bundi wa kisiasa ambaye alikuwa akiinyemelea Chadema, sasa ametua rasmi baada ya chama hicho kutangaza kuwatimua maafisa waandamizi wawili ambao ni washirika wakubwa wa naibu katibu mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, ambaye ameeleza bayana kutofautiana na maamuzi hayo.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa alitangaza jana kuwa kwa kutumia mamlaka yake amewavua nyadhifa zao David Kafulila, ambaye alikuwa ofisa habari wa chama hicho, na Danda Juju, ambaye alikuwa anahusika na mambo ya bunge.

"Tena andika mwandishi wala usiogope ni kwamba, leo (jana) kulikuwa na kikao, nimekiongoza mwenyewe na maamuzi nimeyatoa mwenyewe..., tumetengua uteuzi wao. Sasa ni wanachama wa kawaida," alisema Dk Slaa.

Uamuzi huo ambao unaonekana utagusa majeraha ya uchaguzi mkuu wa viongozi wa chama hicho mwezi Septemba, umekuja siku chache baada ya kuvuja kwa taarifa za mkutano wa siri kati ya Mwenyekiti Freeman Mbowe na baadhi ya viongozi, akiwemo Dk Slaa, ambao wanadaiwa kujadili nidhamu ya wanachama hao wawili pamoja na mama mzazi wa Zitto, Shida Salum.

Mbowe alikanusha kuwepo mkutano wenye ajenda hiyo ya kuwatimua wanachama hao akisema taarifa hizo ni "za kizushi", huku Dk Slaa akisema kuwa hakuna haja ya kuitisha kikao ili kuwashughulikia watendaji hao na kuwafananisha na sisimizi katika chama.

Jana Dk Slaa alisema kuwa ametengua ajira za watu hao wawili kwa maslahi ya chama na kuongeza:" Tunataka kusafisha chama..., maana tukiacha hali hii tunaweza kuingia Ikulu na mambo ya ajabu."

Kwa mujibu wa Dk Slaa, chama hicho kinaongozwa kwa taratibu na kwamba hakiongozwi na majungu hivyo anayekiuka lazima ashughulikiwe.

"Tuliwapa muda wa kutosha wa kujitetea," alisema mbunge huyo wa Karatu ambaye anatajwa kuwa atawania urais kwa tiketi ya Chadema.

Vyanzo vya habari vilidokeza kwamba wanachama hao walihojiwa kwa takriban saa tano katika mkutano uliofanyika makao makuu Kinondoni, Dar es Salaam kabla ya uamuzi wa kuwatimua.

Alipoulizwa sababu za kuwatimua, Dk Slaa alijibu: "Nimekwambia nimetumia mamlaka yangu, usiniulize vigezo au sababu.

"Kwani Rais Kikwete (Jakaya) akitengua ajira za watu mbona hamuulizi katumia vigezo gani... na mimi nina mamlaka ya kufanya hivyo bila kuulizwa."

Dk Slaa alifafanua kwamba, Chadema ni chama ambacho kina malengo hivyo lazima kijisafishe kwa kuweka misingi imara ya uongozi na si watu kufanya mambo bila taratibu.

Katibu huyo wa Chadema alisema haoni kama uamuzi huo unaweza kukiathiri chama hadi kikagawanyika, akisisitiza:"Nasema hakuna mpasuko wala kambi ndani ya Chadema mimi sioni mpasuko wowote.

"Lakini, pia ni bora mpasuko kuliko chama kufa, tukiachia mambo haya yakiendelea ya watu kujifanyia mambo bila taratibu, chama kitakufa... ninyi mnataka kife au?"

Dk Slaa pia alikanusha kuwa uamuzi huo ni kisasi cha mambo yaliyojitokeza katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa viongozi wa Chadema ambao ulitawaliwa na vurugu huku matokeo yakibatilishwa kwa kanuni kutofuatwa au rafu.

Lakini Zitto, ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi, alionekana kutofurahishwa na maamuzi hayo.

Katika ujumbe alioutuma kwa gazeti la Mwananchi jana, mbunge huyo wa Kigoma Mashariki alisema: "Ninasikitika kuwa tunachukua maamuzi kama haya kipindi hiki ambacho nchi inahitaji chama imara cha upinzani.

"Kafulila ni mgombea mtarajiwa wa ubunge katika Jimbo la Kigoma Kusini ambalo CCM wamefanya vibaya katika uchaguzi wa serikali za mitaa kuliko majimbo yote nchini. Uamuzi huu unaweza kuwashtua sana wanachama wetu Kigoma Kusini na mkoa wa Kigoma kwa ujumla."

Zitto alikumbusha kuwa Kafulila aligombea uenyekiti wa jumuiya ya vijana ya Chadema na akashinda, lakini uchaguzi ulivurugwa na kufutwa na hivyo utarudiwa na hivyo uamuzi wa kumfukuza Kafulila ni dalili za wazi za watu waliofuta uchaguzi huo kuleta vurugu kwenye chama kwani wanachama hawatakubali uonevu.

"Kwangu mimi Kafulila ni kijana mahiri mwenye kukipenda chama chetu na ndio maana niliamua kumgroom (kumkuza) ili aje kuwa mgombea ubunge na baadaye mbunge katika Jimbo la Kigoma Kusini.

Anakipenda chama chake, ana akili nyingi na mjuzi wa kujenga hoja katika kutetea chama bila woga," ameandika Zitto katika ujumbe wake kwa Mwananchi.

Zitto aliwasihi viongozi wake kuwa makini katika maamuzi wanayochukua kwa kuwa yanaweza kuvunja moyo juhudi zote za ujenzi wa chama na kuwataka wanachama kutulia mpaka hapo taarifa rasmi za chama zitakapotolewa.

Naye Kafulila alisema: "Sina kinyongo na mtu yeyote ndani ya Chadema na nitagombea ubunge wa Kigoma Kusini kama kawaida.

"Ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba nakipenda sana chama changu, namheshimu sana Dk Slaa, najua tatizo la msingi halijapatiwa ufumbuzi."

Naye Juju alihoji sababu za maamuzi hayo kuwalenga watu ambao wamekuwa wakionekana kuwa mstari wa mbele kumuunga mkono Zitto kwenye kampeni.

"Sasa angalia na jiulize mwenyewe kwanini sisi tuliokuwa kwa Zitto," alihoji.

Katika barua ya kumuita mbele ya mkutano huo kujieleza iliyoandikwa na kaimu katibu mkuu, Kafulila alitakiwa aeleze kuhusu matamshi yake kwenye magazeti na mengine anayoyafahamu kuhusu vyanzo vya habari hizo.

Habari zinasema kuwa Juju hakupewa barua ya kuitwa, lakini alipigiwa simu na kutakiwa kufika mbele ya mkutano huo saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya kuhojiwa. Imeelezwa kuwa mahojiano hayo yalifanyika hadi saa 9:00 alasiri

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, kikao hicho kilianza saa 3:00 asubuhi na kumalizika saa 9:00 alasiri, kisha kufikia maamuzi hayo ya kuvuliwa nyadhifa kwa Kafulila na Danda, ambao sasa ni wanachama wa kawaida.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar