Sabtu, 07 November 2009

Mengi atetea uanachama wake CCM


MWENYEKITI Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, amesema yeye ni mwanachama hai na halali wa CCM tangu mwaka 1977.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mengi alisema madai kuwa yeye si mwanachama wa CCM, ni uzushi na uongo.

“Nilikata kadi ya uanachama katika tawi la Kisutu, Dar es Salaam, Aprili 18, 1977 yenye namba B 124595,” alisema na kuonesha barua iliyoandikwa Oktoba 29 mwaka huu kuthibitisha kuwa ni mwanachama wa chama hicho.

Akijibu sababu ya kuchukua barua hiyo siku chache zilizopita inayoonesha kusainiwa na Katibu wa CCM Kata ya Kisutu, Musa Kambanga, alisema “nililazimika kuiomba ili kuthibitisha kuwa ni mwanachama baada ya Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Shaaban Kilumbe, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kudai kuwa ametembea kila shina hajaona jina la Mengi”.

Alisema madai hayo yaliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Sophia Simba, Kilumbe na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam John Guninita ni ya uongo, uzushi na umbeya wenye lengo la kudhoofisha juhudi za viongozi wa juu wa chama hicho na baadhi ya wanachama kupiga vita ufisadi.

Kauli ya Mengi imekuja baada ya Waziri Simba katika kikao cha wabunge wa CCM na kamati ya wazee wa chama hicho, kumshutumu Mengi kuwa si mwanachama wa CCM.

Wakati Mengi anaeleza hayo, Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango-Malecela ambaye pia alitajwa na Simba kuwa si mwadilifu na anayejifanya kupiga vita ufisadi kutokana na kinyongo cha kukosa kuwa mke wa Rais, alisema anatafakari ili kubaini chanzo cha tuhuma hizo juu yake hasa katika kipindi hiki cha vita ya ufisadi.

Mengi katika mkutano huo naye alidai kuwa Simba si mwadilifu: “Angalieni uchaguzi wa UWT(Umoja wa Wanawake Tanzania) ulikuwa na rushwa au haukuwa na rushwa?”.

Awali Simba alidai kuwa CCM ilimkatalia Mengi uanachama na kuwabeza wabunge wanaojiita wapambanaji na ufisadi wanaofuatana naye kutoa misaada lakini akiwa haitoi kwa CCM.

Katika tamko lake hilo aliloliita la kuweka rekodi sawa, Mengi alisema “ningemshauri kabla hajazungumza (Simba) aombe ushauri kutoka taasisi za Serikali kama vile Usalama wa Taifa badala ya kuropoka na kupotosha ukweli wa mambo”.

Hata hivyo alisema anamshauri Simba kwa sasa katika vita dhidi ya ufisadi anyamaze kutokana na kuamini kuwa si mwadilifu.

“Hawa wanaodai ndani ya CCM hakuna kiongozi msafi ni wazi wamedandia chama hiki hivi majuzi, ningetoa ushauri waondoke na watuachie chama chetu kwa kuwa hawafahamu msingi imara wa CCM”, alisema Mengi.

Kuhusu misaada yake kwa CCM, Mengi alisema viongozi wakuu wa CCM ambao ni waadilifu, wacha Mungu na wanaosimamia ukweli, wanalitambua hilo kwa undani. Hata hivyo alikataa kutaja misaada ambayo ameitoa kwa chama hicho akisema kufanya hivyo ni kukivunjia heshima na si vizuri.

Kilango katika taarifa yake jana, alisema Simba ni waziri mwenye dhamana ya utawala bora ambaye anafahamu vyombo vyenye mamlaka ya kushughulikia tuhuma hizo, ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) hivyo alitakiwa tangu mwaka 2005 kutoa taarifa hizo na si kusubiri sasa.

Alisema Simba atapimwa na wananchi kama malumbano anayoanzisha sasa yana chembe ya ukweli au yana lengo la kuwahamasisha Watanzania katika vita nzito ya ufisadi.

Alisisitiza kuwa yeye ni mbunge wa kuchaguliwa na wananchi wa Same Mashariki ambao walifanya hivyo kutokana na imani yao kwake na kuongeza kuwa atatetea na kushirikiana nao kwa maendeleo na maslahi yao na ya Taifa ndani na nje ya Bunge na si vinginevyo.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar