Rabu, 11 November 2009

Hatimaye Mitambo ya Dowans kupigwa mnada

HATIMAYE serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefungia mitambo ya kuzalisha umeme ya Kampuni ya Dowans, kwa kile kilichoelezwa kushindwa kulipa kodi.

Dowans, ni kampuni iliyorithi zabuni ya kuzalisha umeme wa megawati 100 kutoka kwa kampuni hewa ya Richmond Development LCC, baada ya kushindwa kuzalisha umeme kama ilivyokubaliana na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO).

Kupitia wakala wake, Majembe Auction Mart, TRA jana ilifungia mitambo ya Dowans iliyopo Ubungo Dar es Salaam, na kuhamisha baadhi ya vifaa vya kampuni hiyo ambavyo vimehifadhiwa kwenye ghala la madalali hao.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, wakati zoezi la kufungia mitambo hiyo na kuhamisha baadhi ya vifaa likiendelea jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Majembe, Seith Moto, alisema kampuni yake ilipokea notisi ya kuifungia mitambo hiyo kwa madai ya kushindwa kulipa kodi ya serikali yenye thamani ya zaidi ya sh bilioni tisa.

“Jana (juzi), tulipokea ‘warrant’ inayotutaka kuiuza mitambo hiyo kama Dowans hawatalipa kodi wanayodaiwa. Sisi tupo hapa kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato.

“Dowans wanadaiwa kodi mbalimbali, ikiwemo Domestic Revenue na Corporate tax. Kazi yetu ni kuhakikisha fedha hizo zinalipwa. Ili kuzipata, tumewapa viongozi wa kampuni hiyo muda wa siku 10 kuanzia leo (jana) vinginevyo, tunaipiga mnada mitambo na vifaa vyao,” alisema Moto.

Mkurugenzi huyo wa Majembe, alisema licha ya kuifungia mitambo ya Dowans, wametoa siku 10 kwa wamiliki na viongozi wa kampuni hiyo, kulipa kodi wanayodaiwa vinginevyo, mitambo na vifaa vyao vitapigwa mnada.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa Dowans ambaye ni raia wa Kenya, aliyetambulika kwa jina moja la Stanley, alikataa kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwepo Ubungo kwenye ofisi za Dowans kwa madai kwamba si msemaji wa kampuni hiyo.

Sheria iliyounda TRA imetoa uwezo kwa mamlaka hiyo kutaifisha na kuuza mali za mdaiwa sugu wa kodi ili kujilipa jambo lililoikumba Kampuni ya Dowans ambayo mkataba uliorithi ulilishtua taifa na kuzua mjadala kati ya watendaji wa TANESCO na wanasiasa wachache.

Licha ya mjadala mkali uliokuwa ukiendelea nchini kuhusu uhalali wa kampuni hiyo kuendelea kufanya kazi kupitia mkataba wa Kampuni ya Richmond, TANESCO iliazimia kununua mitambo yake, lakini ilishindwa kufanya hivyo kutokana na mashinikizo ya kisiasa.

Mashinikizo hayo, yalimlazimu Mkurugenzi wa TANESCO anayemaliza muda wake, Dk. Idris Rashidi, kuueleza umma kwamba shirika lake limeazimia kutonunua mitambo ya Dowans na kutahadharisha kuwepo kwa tatizo la umeme kuanzia Oktoba, mwaka huu.

Kwa shingo upande, baada ya kueleza nia ya shirika kutonunua mitambo hiyo, Dk. Rashidi alibainisha kwamba jambo hilo limetokana na kile alichokiita upotoshaji wa kisiasa.

Chimbuko la Dowans ni mkataba wa mradi wa kufua umeme wa dharura wa megawati 100 kati ya serikali kupitia TANESCO na Kampuni ya Richmond uliofikiwa mwaka 2006.

Richmond baada ya kushindwa kuutekeleza mradi huo iliuuza mkataba wake kwa Dowans ambao wameshindwa kulipa kodi na kulazimika kutaifishwa kwa mitambo yao.

Mkataba wa Richmond ulizua mvutano kiasi cha kusababisha Bunge kuunda Kamati Teule kuchunguza, ikiongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, ambapo ripoti yake ilimlazimu aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ajiuzulu.

Pamoja na Lowassa, mawaziri wengine wa awamu ya nne waliojiuzulu baada ya kashfa ya kuisaidia kampuni tata ya Richmond kushinda zabuni iliyodaiwa kuwa na harufu ya rushwa, ni Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.

Sakata la Richmond lilitikisa nchi kuanzia Juni mwaka 2006, miezi michache baada ya serikali ya awamu ya nne kuingia madarakani na nchi kukabiliwa na ukame na uhaba wa nishati ya umeme, hivyo kulazimu serikali kutafuta mitambo ya dharura ya kukodi kwa ajili ya kufua umeme.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar