Jumat, 30 Januari 2009

DAR ES SALAAM SASA KUWA NA BARABARA ZA JUU (HIGHWAY)

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akifuta machozi wakati akielezea mauaji ya Albino alipokuwa akijibu swali Bungeni kuhusiana na kauli yake aliyoitoa hivi karibuni katika mikoa ya kanda ya ziwa.

RAIS Jakaya Kikwete amewaagiza viongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuweka utaratibu wa kujenga barabara za kupita juu kwenye makutano yote ya barabara za jijini, ili kupunguza msongamano wa magari.


Rais Kikwete alitoa agizo hilo juzi jioni katika Ukumbi wa Karimjee wakati wa chakula cha jioni, kilichoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kumpongeza kwa mafanikio ya serikali yake katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Rais pia aliwaagiza madiwani na watendaji wote kuwa wabunifu katika kuaondoa kero zinazolikabili Jiji la Dar es Salaam, ikiwamo msongamano wa magari na makazi yasiyopangwa.

Aliwataka madiwani na watendaji hao kuweka mikakati ya kujenga barabara zinazopita juu (Fly-overs), ili kupunguza msongamano wa magari jijini unaosababisha kero kubwa kwa watumiaji wote wa barabara pamoja na kuathiri utendaji na shughuli mbalimbali za maendeleo.

Alisema tatizo la usafiri jijini linasababishwa na kutokuwa na usafiri bora wa umma, jambo ambalo linawafanya watu walazimike kununua magari binafsi.

"Wenzetu kule Ulaya wana huduma nzuri ya usafiri wa umma kama vile treni za mwendo kasi hivyo watu huona bora kutumia usafiri huo kuliko magari yao.

Ubora wa huduma ndio utakaopunguza msongamano," alisema na kuongeza: "Endeleeni kuwa wabunifu na fikirieni kujenga (Fly-overs roads) hasa katika makutano ya barabara; kama vile maeneo ya Ubungo,Tazara na Selander Bridge hiyo ndiyo njia ya kupunguza msongamano wa magari, kwa sababu wakazi wa jiji nao wanaongezeka haraka".

Rais pia alisisitiza ujenzi wa miji mipya ya pembezoni mwa jiji na kuweka huduma zote muhimu kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa watu katikati ya jiji.

Alisema kuwa msongamano wa watu katikati ya jiji hutokana na huduma zote muhimu kama vile mabenki na masoko kuwa eneo moja.

Kuhusu tatizo la mipango miji, Rais Kikwete alisema ingawa viongozi hao wameshindwa kulifanya Jiji la Dar es Salaam liweze kupendeza na hata kuwa kitovu cha utalii na kwamba, ingawa kuna wataalamu, lakini wanashindwa kuutumia ujuzi wao.

"Kwa mfano wenzetu kule Nairobi, Kenya wanayo, lakini sisi hapa sijui tumepitiwa na ugonjwa gani. Kila wakiona mahali pa wazi wao ni kwenda kwenye vikao vya halmashauri kujadili kugawa viwanja kwa matajiri," alisema na kuongeza:

"Tunao maofisa ambao wamesoma hadi Ulaya, lakini wakirudi hapa wanafanya mambo kinyume. Hata viwanja vya michezo wanagawa kwa matajiri".

Alisema viongozi hao wameshindwa kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kituo cha utalii licha ya kuwa na fukwe nyingi na kwamba, hiyo ni kwa sababu wameshindwa kuziendeleza fukwe hizo na kuzifanya zipendeze.

Rais pia alishangazwa na uamuzi wa jiji kuwazuia wananchi kupiga picha za harusi ufukweni, nyuma ya Ikulu na kubadilisha matumizi ya ardhi iliyoachwa wazi.

Alisema wakati fulani alipokuwa anapita katika eneo hilo alikuwa akiona watu wengi na hasa mwishoni mwa juma, wakienda kupiga picha za harusi katika eneo hilo baada ya kufunga ndoa, lakini baadaye akasikia kuwa halmashauri ya jiji imewazuia.

"Siku hizi watu wakioa wasipopiga picha pale baharini wanajiona kama hawajakamilika, lakini baadaye nikasikia kuwa halmashauri imepiga marufuku kupiga picha hapo.Hivi kuna dhambi gani kupiga picha hapo?" alihoji Kikwete na kuongeza: "Hebu waacheni watu wapate raha.

Kama ni suala la kuchafua mnaweza kuwapangia utaratibu wa kufanya au kuwapa masharti, hata kama ni kuwatoza kidogo kwa ajili ya usafi". Aliongeza: "Kuna watu mkiwa serikalini kazi yenu ni kuzuia kila kitu.

Watu wakienda kuogelea mnawafukuza. Namna hii mnawapa watu kimuhemuhe. Mnawabana kiasi kwamba, hawana hata pa kupumulia, hivi ni vitu vidogo tu wapeni uhuru," alisema Rais Kikwete.

Rais pia alieleza kukerwa na uamuzi wa viongozi wa jiji kuwaruhusu wafanyabiashara wa magari makubwa ya mizigo kuegesha katika eneo la Jangwani.

Alisema eneo hilo ni maalumu kwa ajili ya vijana kufanyia michezo mbalimbali, lakini sasa limegeuzwa la kuegesha magari hayo."Hata mimi nilikuwa nikienda kucheza pale, na pale palikuwa pana angaliwa sana wala hakuna maji yaliyokuwa yanajaa, lakini sasa mmeliachia na watu wamelitumia kwa matumizi yao.

Sidhani kama watu hao wamevamia, lakini pia sitegemei kuwa huo ni uamuzi wa halmashauri hii. Kama wamevamia basi watafutieni mahali pengine ili vijana wapate mahali pa kuchezea," aliagiza.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar