RAIS wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ambaye amekuwa akisakamwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi, huku akitakiwa kuvuliwa kinga na kupandishwa kizimbani, sasa anakabiliwa na tuhuma nyingine nzito; anatakiwa afikishwe Mahakama ya The Hague baada ya Wapemba kuuawa Januari 27, 2001.
Mauaji ya Wapemba hao yalitokea mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya urais wa Zanzibar wakati Amaan Abeid Karume alipotangazwa mshindi na kusababisha wapinzani kuandamana kupinga ushindi huo. Serikali inasema ni watu wasiozidi 27 ambao waliuawa, lakini wapinzani wanasema ni zaidi ya 100.
Na wazee wa Pemba walioshiriki kuandaa barua ya kuuomba Umoja wa Mataifa uwasaidie kupatikana kwa serikali huru ya kisiwa hicho, ndio walioibua hoja hiyo wakisema wanakusudia kumfikisha rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa Mahakama ya The Hague kutokana na mauaji waliyoyaita ya kikatili ya Wapemba yaliyotokea Januari 27 mwaka 2001.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, katibu mtendaji wa wazee hao, Hamad Ali Musa, alisema tayari walishafikisha suala hilo kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa kwani mauaji hayo yalitokea wakati viongozi hao wakiwa madarakani.
Idadi ya watu waliouawa baada ya kutangazwa kwa matokeo iliibua mjadala na katika mahojaino na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Mkapa alionekana kupata hasira baada ya mtangazaji kumweleza kuwa idadi ya waliouawa ni zaidi ya 100.
Mkapa alisema katika kipindi hicho cha Hard Talk kuwa, anashangaa waandishi kuokota habari wakati mtoaji rasmi wa taarifa kama hizo ni serikali.
Musa pia alisema wanakusudia kumfikisha katika mahakama hiyo aliyekuwa mkuu wa Jeshi la Polisi, Omary Mahita wakidai kuwa, damu iliyomwagika bila hatia katika kipindi hicho haiwezi kufumbiwa macho na hivyo ni muhimu haki itendeke na sheria kuchukua mkondo wake.
Kiongozi huyo alisema, hivi sasa wapo katika mchakato wa mwisho wa kutafuta mawakili watakaosimamia kesi yao ipasavyo wakati itakapoanza kusikilizwa.
Katika suala la kumfikisha Waziri Seif Khatib mahakamani, Musa alisema kuwa, mapema mwishoni mwa mwezi huu mchakato huo utakuwa umekamilika, kwani mawakili wa kusimamia kesi hiyo tayari wameshapatikana.
"Ni vema viongozi wetu wakaelewa kuwa hakuna haja ya kuwafumba midomo watu wanapotafuta haki zao za msingi. Waziri Khatib alitufumba midomo kwa kutumia nguvu za dola na ndiyo maana tukawekwa ndani," alisema Musa.
Katika hatua nyingine, mjumbe wa kikundi cha wazee hao, Ally Makame alisema bado wanaendelea kuzitaka jumuiya za kimataifa kushughulikia suala la kisiwa hicho kujitenga na kuwa na dola yake kwani hatua iliyopo hivi sasa inaonyesha dhahiri kuwa watu wake wameendelea kudhalilishwa kila siku.
Alisema mapema mwezi uliopita walipeleka maombi yao ya kutaka kujitenga katika ofisi za Umoja wa Mataifa, lakini walijibiwa kuwa Pemba haina sababu za kujitenga kutokana na ukweli wa mambo kwamba, Rais Jakaya Kikwete anashughulikia mpasuko uliopo ndani ya Zanzibar.
"Jambo hili ni uongo kwani suala letu halihusiani kabisa na masuala ya siasa, katika suala la kutaka Pemba iwe na dola yake si suala la CUF, ni suala letu wananchi, hivyo ni vema viongozi wakafahamu jambo hili," alisema Makame.
Alisema baada ya kupokea majibu hayo ya awali ya barua yao kutoka UN, tayari wameshaandika barua nyingine wakieleza hisia zao kuwa, kama suala la mpasuko lisiposhughulikiwa mapema, hali itakuwa mbaya tena kwenye uchaguzi wa mwaka 2010.
"Wapemba hawatakubali kuendelea kufedheheshwa kama wakimbizi, hivyo ni vema mashirika ya UN yakaanza kujiandaa mapema kupokea wakimbizi nchini Kenya wakati wa uchaguzi," alisema Makame.
Baada ya vurugu hizo za mwaka, watu kadhaa kutoka Pemba walikimbilia Shimoni, Mombasa wakisaka hifadhi ya kisiasa.
Juni mwaka jana kikundi cha wazee 12 wa Kisiwa cha Pemba waliibuka na kuzua hoja ya kutaka kujitenga kwa kisiwa chao kwa madai kuwa, serikali ya CCM inawabagua kimaendele
Tidak ada komentar:
Posting Komentar