Kanisa hilo kwa mujibu wa bango la uzinduzi, limeingia katika historia ya kuzinduliwa na maaskofu wa makanisa mengi kwa pamoja wakiwamo Alex Malasusa wa KKKT, Boniface Kwangu wa Anglikana, Severin Niwemugizi na Aloysius Balina wa Katoliki, Daniel Nungwana wa AICT na Sylvester Gamanywa wa Pentecoste.
Kanisa hilo lililozinduliwa Septemba 5, mwaka 2008 na limepewa jina la Mtakatifu Joseph ambalo pia ni jina la baba yake mzazi wa Magufuli, Joseph John aliyefariki Septemba 5, mwaka 2007, lipo katika eneo la Mlimani au Mji Mpya jirani kabisa na Makao Makuu ya Wilaya yas Chato na Ofisi za Halmashauri ya Wilaya hiyo mpya.
Utata wa kanisa hilo umekuja kutokana na waumini wa Kanisa Katoliki na wenzao wa AICT kukataa kulitumia kwa sababu mbalimbali ikiwamo ya tofuati za taratibu za kusali licha ya kwamba walikabidhiwa kanisa hilo walitumie kwa pamoja.
Paroko wa Parokia ya Chato, Padri Ladislaus Mwilinde amekiri kanisa lake kukataa kutumia kanisa hilo kwa ibada zake za kawaida.
Alisema wamejitoa miongoni mwa watumiaji wa kanisa hilo kwa sababu wana kigango chao katika eneo jirani na lilipojengwa kanisa hilo.
Vile vile alisema kanisa lake limeamua kutolitumia kanisa hilo kutokana na kuwa na taratibu tofauti za ibada na makanisa mengine, jambo ambalo linakwamisha kuwekwa kwa baadhi ya vifaa vya ibada maalum kwa dhehebu lake katika kanisa hilo.
"Siyo kwamba hatutalitumia kanisa hilo, tutalitumia kwa ajili ya ibada za umoja na madhehebu mengine kama vile kuombea mvua na mambo mengineyo, lakini kwa ibada zetu za kawaida hatutaweza kulitumia kutokana na kanuni zetu za imani na taratibu za kuabudu kuwa tofauti na makanisa mengine," alieleza.
Kwa mujibu wa paroko huyo, wakati kanisa hilo likijengwa hawakuwa wakijua kuwa lilikuwa kwa matumizi hayo, hata lilipokamilika walialikwa kwa ajili ya ibada ya ufunguzi ambayo walishiriki, na kuongozwa na maaskofu wa kanisa lake.
"Unajua ibada zetu zinakuwa na utaratibu wake na wala dini siyo kitu cha kutengeneza bali ni kitu cha kiroho zaidi, ukiwa katika kanisa hilo huwezi kupanga maendeleo yako na kanisa lako, maana hilo ni la watu wengi, lakini pia kunaweza kuzuka ugomvi wa nani amlipe mlinzi au nani afanye usafi, hii siyo hoja isipokuwa kunaweza kuibuka malumbano ya kiimani, kwamba hawa wanatumia msalaba au mambo mengine," alieleza Paroko.
Alisema kutokana na kuwa na kigango chao jirani na eneo hilo na kuwapo mipango ya kujenga jingine wameamua kutolitumia kanisa hilo kwa utaratibu wa ibada zao.
Akizungumza jana na Mwananchi Jumapili, Mchungaji Reuben Mahugi wa Kanisa la Free Pentecost Church of Tanzania (FPCT) ambaye ndiye msimmizi mkuu wa matumizi yake kwa sasa, alisema kanisa hilo limekuwa likitumiwa na makanisa mawili, la kwake na Anglikana baada ya makanisa mengine kujitoa.
Alisema ingawa kanisa hilo limejengwa kwa ajili ya matumizi ya wote, madhehebu mengine yamejitoa kutokana na sababu za kiimani na lile la kutumia na watu wa madhehebu tofauti.
"Kanisa Katoliki walijitoa kutokana na utaratibu wao wa ibada kutofautiana na makanisa mengine, AICT wao walidai hawana maono ya kuhusiana na matumizi ya kanisa hili, hivyo nao kuamua kukaa pembeni," alieleza Mahugi.
Alisema baada ya kukabidhiwa jengo hilo na Waziri Magufuli ambaye pia ni Mbunge wa Chato, walipangiana utaratibu wa kulitumia kwa kufuata muda maalum ili kila kanisa liweze kunufaika, lakini makanisa mengine walijitoa.
Ratiba iliyowekwa awali ilikuwa ni kuanza kutumiwa na wakatoliki kuanzia saa 2:30 hadi 4:00 asubuhi, FPCT kuanzia saa 4:00 hadi saa 7:00 mchana na kisha Anglikana kuanzia saa 9:00 alasiri hadi saa 11:00 jioni.
Baada ya wakatoliki kujitoa ratiba ilibadilishwa na kuanza na Anglikana kuanzia saa 2:30 hadi 4:00 asubuhi kisha Kanisa la FPCT kuanzia saa 4:00 hadi saa 7:00 mchana na baadaye kutumika tena na Anglikana kuanzia saa 9:00 alasiri hadi saa 11:00 jioni.
Baadhi ya waumini wa kanisa la Pentekoste katika eneo hilo walisema kujitoa kwa kwa madhehebu hayo kumeepusha msuguano ambao ulikuwa ukielekea kutokea.
Mmoja wa waumini hao, Zacharia Gabriel alisema kutokana na kuwepo kwa msalaba ndani ya kanisa hilo baadhi ya waumini wa Kipentecoste nao waligoma kuingia katika kanisa hilo hali ambayo imepunguza waumini wanaosalia humo hadi 20 kila Jumapili.
Akizungumzia kanisa hilo, Mwinjilisti Yohana Lucas alisema kuwa amelipokea kwa furaha kanisa hilo kwa ni linasaidia kuhuduamia waumini wa eneo hilo la Mtaa wa Mlimani.
Alisema kuwa kabla ya kuwapo kanisa hilo waumini waliokuwa wakiishi mtaa huo walikuwa wakipata taabu ya kusafiri umbali mrefu kufika Chato mjini ambako walilazimika kulipia nauli ya Sh 500 kwenda kanisani.
"Hapa unaniona naendesha mafundisho ya biblia, haya ni moja ya matunda ya kanisa hili, awali hatukuwa tukifika huku, lakini leo ibada imefika tunasali," alieleza Mwinjilisti huyo.
Mzee wa Kanisa la Anglikan, Elias Kaswahili alisema wao wamefurahi kujengwa kwa kanisa hilo kwa sababu linawasaidia waumini wao kupata sehemu ya kumwabudu Mungu lakini akaonyesha kusitikika kwa wenzao kujitoa.
Juhudi za kumtafuta waziri magufuli zilishindikana baada ya simu yake kuita muda mrefu bila majibu.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar