Hali ya utulivu imeshuhudiwa alasiri ya leo katika eneo la Gaza huku juhudi za kimataifa zikiendelea katika miji mbali mbali kuutanzua mzozo huo.
Viongozi wa mataifa ya Kiarabu walikutana leo mjini Doha, Qatar, huku mawaziri wa mambo ya nchi za Nje kutoka mataifa ya Kiarabu wakifanya mkutano mwengine nchini Kuwait. Je hizi ni juhudi za kutanzua mzozo wa Gaza au ni kuoneshana misulu miongoni mwa viongozi wa mataifa ya Kiarabu katika eneo la Mashariki ya kati?
Labda mtu anaweza kusema viongozi wa mataifa ya Kiarabu kwanza wanapasa kutatua tofauti zao kabla ya kujitwika jukumu la kuutanzua mzozo wa Gaza.
Tofauti miongoni mwa viongozi wa mataifa ya Kiarabu zilijitokeza wazi hii leo, baada ya ya viongozi wa mataifa hayo kukutana mjini Doha, Qatar, kuendelea na mkutano ulioitishwa wiki iliyopita kuzungumzia suala la Gaza, licha ya mkutano huo kukosa kuidhinishwa na idadi inayohitajika kuitisha kikao cha dharura.
Kwa mujibu wa katiba ya muungano wa mataifa hayo, mkutano huo haukupasa kufanyika kwa vile uliungwa mkono na wanachama 14 pekee badala ya 15 wanaohitajika.
Wakati wa mkutano huo, uliohudhuriwa na mpinzani mkuu wa Israel, ambaye ni Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, kiongozi wa chama cha Hamas aliyeko uhamishoni, Khaled Meshaal, alitoa onyo kali kwa Israel kwamba chama chake hakitakubali masharti yanayotolewa na Israel kabla ya kusitishwa mapigano.
Kuweko kwa kiongozi huyo na Rais Ahmedinejad, pasi na kuhudhuriwa na Rais wa Palestina. Mahmud Abbas, kumezua maswali mengi kuliko majibu.
Huku mkutano huo ukiendelea, mkutano mwengine wa mawaziri kutoka mataifa ya Kiarabu ulikuwa ukifanyika nchini Kuwait,ambako wajumbe walikubaliana kwa kauli moja kwamba mashambulizi hayo yanapasa kukomeshwa mara moja na kuanzishwa harakati za kulijenga upya eneo la Gaza.
Mkutano huo pia unaitaka Israel kuondoa vizuizi vyote na kufungua maeneo ya mpakani, huku nao wafuasi wa chama cha Hamas wakitakiwa wakomeshe mashambulizi ya marokreti ndani ya Israel.Katika mapendekezo yao mawaziri hao waliahidi kiasi cha dala milioni 500 kusaidia utawala wa Palestina.
Katibu mkuu wa jumuiya hiyo ya mataifa ya Kiarabu, Amr Musa, anayehudhuria mkutano huo wa Kuawait alikiri kuwepo mgawanyiko mkubwa miongoni mwa mataifa ya Kiarabu.
Huku Hayo ya kijiri, Rais Mahmud Abbas alikuatana na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa mjini Ramallah kuzungumzia mzozo huo wa Mashariki ya Kati unaoingia siku yake ya 21.
Katibu mkuu huyo alikariri msimamo wake wa kuzitaka pande mbili kwenye mzozo huo zikomeshe mashambulizi zaidi ili kutoa nafasi ya juhudi ya kutafuta amani na misaada ya kibinadamu katika eneo hilo la Gaza.
Ban Kii Moo alikutana na rais Abbas baada ya kufanya mashauriano na viongozi wa serikali ya Israel mjini Tel Aviv hapo jana.
Wakati huo huo, mjumbe wa Israel kwenye mpango wa amani unaoongozwa na Misri, Amos Gilad, alirejea nchini mwake huku kukiwa na habari kwamba Israel haikuridhia baadhi ya mapendekezo yaliyomo kwenye mpango huo.
Duru zinaarifu kuwa mjumbe huyo wa Israel alikataa pendekezo la kusitishwa mapigano kwa muda wa mwaka mmoja na sasa linalosubiriwa ni uamuzi wa baraza la usalama la Israel kuhusiana na mwelekeo utakaochukua mpango huo wa amani.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel, Tzipi Livni, pia amesafiri nchini Marekani kufanya mashauriano na Rais George W. Bush kuhusu mpango unaokusudia kuwakomesha Hamas kutumia maeneo ya mpakani kuingiza silaha ndani ya Gaza
Hali kadhalika chama cha Hamas, kwa mara nyingine tena, kimetuma wajumbe wake mjini Cairo kufanya mashauriano zaidi kwenye mpango huo.
Zaidi ya Wapalestina 1,100 wameuliwa na wengine 4,500 kujeruhiwa nao upande wa Israel ukiwapoteza 10 raia watatu tangu vita hivyo vianze disemba 27.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar