Rais Jakaya Kikwete juzi aliongoza mamia ya waombolezaji kumzika mmoja wa wanasiasa magwiji mkoani Mara na nchini, Ezekiel Mirumbe Waryuba.
Baada ya kuwasili nyumbani kwa marehemu katika Kijiji cha Masurura, kiasi cha kilomita 30 kutoka mjini Musoma kwenda Tarime, Rais Kikwete alisalimiana na wanafamilia wa marehemu, wakiwamo wajane zake wanne; alitia saini kitabu cha rambirambi, kabla ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu.
Mwili wa Waryuba aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania kati ya mwaka 1973 hadi 1977 na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mara kwa miaka 20 mfululizo kuanzia mwaka 1977, uliteremshwa kaburini saa 7:55 mchana kwa heshima zote za Chama Cha Mapinduzi.
Rais Kikwete aliyekatisha ziara yake ya Zanzibar kwenda kuhudhuria maziko hayo, akifuatana na Mama Salma Kikwete, aliwasili nyumbani kwa marehemu saa 7:25 mchana kuungana na viongozi wengine wengi kwenye maziko hayo.
Miongoni mwa viongozi wengine waliohudhuria maziko hayo ni Mkuu wa Mkoa wa Mara Issa Machibya, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wassira aliyetoa shukurani kwa niaba ya familia, na wanasiasa wakongwe Kingunge Ngombale-Mwiru na Pancras Ndejembi aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma kwa miaka mingi.
Wengine ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa Shinyanga Khamis Mgeja, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza Clement Mabina, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Saleh Ramadhani Ferouz, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kusini Pemba, Abdallah Mshindo, na Katibu Mtendaji wa Nyerere Foundation Joseph Butiku.
Waryuba aliyekuwa na umri wa miaka 74, alifariki dunia mwanzoni mwa wiki hii nchini India, alilolazwa kwa ugonjwa wa kansa ya tumbo. Ezekiel Mirumbe Waryuba alizaliwa mwaka 1935 katika Kijiji cha Masurura, akiwa mtoto wa saba katika familia ya watoto 19. Baada ya elimu yake ya msingi na kati, alijiendeleza mwenyewe kwa masomo ya elimu kwa njia ya posta. Ameacha wajane wanne, watoto 27, wajukuu 37 na vitukuu sita.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar