RAIS Jakaya Kikwete huenda akalazimika kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri kama hatua ya kusafisha serikali yake na kupata timu atakayoingia nayo katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2010.
Kulazimika kwa Kikwete kufanya mabadiliko hayo kunatokana na matukio ya ufisadi yaliyoikumba mwaka jana na kuwahusisha baadhi ya watendaji wake wakiwamo mawaziri.
Habari zilizopatikana ndani ya serikali zinaeleza kuwa katika kujiandaa na uchaguzi mkuu ujao, Kikwete ameamua kuingia katika uchaguzi ujao akiwa na timu mpya ya watu wasafi ambao hawataipa shida CCM kujinadi kwa wapiga kura.
Katika mwaka wa pili tangu kuingia madarakani, kashfa mbalimbali za ufisadi, wizi na uingiaji mikataba mibovu zimeikumba serikali yake na kumpa wakati mgumu mno kutawala.
Kashfa hizo ni pamoja na mkataba wa Richmond, Wizi wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Kashfa ya mikataba ya madini, Kampuni ya kufua umeme ya IPTL, wakala wa mizigo bandarini (TICTS), matumizi mabaya ya madaraka na nyinginezo huku zikihusisha mawaziri na watendaji mbalimbali wa serikali.
Kashfa ya Richmond Februari mwaka jana ilisababisha Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa pamoja na Mawaziri wengine wawili kujiuzulu katika kile walichoeleza ni kuwajibika baada ya kutajwa kuhusika katika sakata hilo.
Kashfa hizo zilisababisha wananchi kupunguza imani kwa serikali na viongozi wao, huku wakidai kufanyika kwa uchunguzi zaidi na wahusika wa mikataba hiyo mibovu na wizi wa fedha za EPA wachukuliwe hatua za kisheria.
Matukio hayo na lile kubwa la Waziri Mkuu kujiuzulu yaliacha wingu zito jeusi hata kuzua hofu kuhusu mustakabali wa taifa na usalama wake.
Kutokana na matukio hayo, Rais Kikwete alilazimika kulivunja baraza lake la mawaziri na baada ya siku tatu aliunda baraza jipya la mawaziri pamoja na kubadilisha muundo wa baadhi ya wizara na nyingine kuziunganisha huku Mizengo Pinda akiteuliwa kuwa Waziri Mkuu.
Aidha katika kipindi hicho cha mwaka 2008 taifa lilishuhudia kuingia kwa mustakabali uliozusha mjadala wa Zanzibar ni nchi au la ulioliopandisha joto katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuzua hofu ya mpasuko katika muungano huo.
Pamoja na hayo kundi la wana mtandao linalodaiwa kuwa ndilo lililomwingiza madarakani Rais Kikwete lilidaiwa kugawanyika katika makundi mawili, yaani wanamtandao wasafi na wanamtado wanaodaiwa kujihusisha na ufisadi.
Ingawa hatua kadhaa tayari zimeanza kuchukuliwa na serikali ikiwamo kuwafikisha watuhumiwa wa kashfa hizo mahakamani lakini bado kuhusishwa kwa baadhi ya mawaziri walio madarakani, watendaji wa CCM na baadhi ya watendaji wa juu wa serikali na ufisadi, kunaonyesha kuwachosha wananchi, kukichafua chama hicho na kwamba kinahitaji kusafishwa.
"Kikwete sasa amechoka na kuchafuliwa na watendaji wake anataka kuwa na timu safi ya ushindi katika uchaguzi mkuu ujao," alidokeza mwanasiasa mmoja nchini aliyepo karibu na Kikwete.
Pamoja na kuchoshwa na hayo wananchi pia wamekuwa wakitarajia kutimia kwa ahadi ya ‘maisha bora kwa kila mtanzania’ iliyotumika kuinadi serikali ya awamu ya nne, ambayo sasa wananchi wanaiona kama ndoto isiyoweza kutimizwa.
Hali halisi inaonyesha kuwa uchaguzi umekaribia na CCM inataka kuendelea kutawala nchi huku Rais Kikwete aliye madarakani kwa sasa naye kwa tiketi ya chama hicho akiwa na uwezo kikatiba kuwania tena kiti hicho kwa awamu nyingine ya kipindi cha miaka mitano ingawa pia wanachama wengine wa CCM wanaruhusiwa kugombea.
"Ikiwa Kikwete atawania urais kwa mara ya pili uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 atalazimika kuzingatia hali halisi na historia iliyoukumba utawala wake katika miaka mitatu ya mwanzo na kuhitaji kujipanga upya," alionya mwanasiasa huyo.
"Ni wazi kuwa historia ya matukio hayo, CCM inaweza kupata hukumu mbaya kutoka kwa wapiga kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu na hata uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ya kukataliwa na wananchi,"alisema.
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa kutokana na umuhimu wa jambo hilo, Kikwete anaweza kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawazri wakati wowote kuanzia sasa ili kuondoa makapi na kupata timu bora na safi ya watendaji itakayombeba yeye na CCM katika uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar