Jumat, 30 Januari 2009

VYUO VIKUU SASA KUPEWA 100% YA MIKOPO

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imefanya mabadiliko ya utaratibu wa utoaji mikopo kwamba, sasa watatoa asilimia 100 kwa wanafunzi wa vitivo mbalimbali kulingana na vipaumbele vya serikali.

Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Nicolaus Mbwanji, alisema jana kuwa utaratibu huo utaanza kutumika katika mwaka mpya wa fedha wa 2009/2010 kwa kuanzia na wanafunzi wa fani za sayansi.

Katika marekebisho hayo bodi hiyo imeongeza makundi yatakayopata mikopo kutoka sita hadi 11, pamoja na kutoa mikopo ya kujiendeleza kwa wahadhiri wa vyuo binafsi sawa na wale wa serikali.

Akizungumza jana jijini Mwanza alisema kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kutembelea vyuo 17 na kuzungumza na wanafunzi, viongozi wa serikali zao na wakuu wa vyuo hivyo.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, bodi hiyo ilikuwa ikitoa mikopo kwa makundi na asilimia zake katika mabano A(100), B(80), C(60), D(40), E(20) na F(0), lakini sasa imeongeza idadi ya makundi hayo hadi kufikia 11, ambayo ni na viwango vyake vya asilimia za mkopo katika mabano A(100), B(90), C(80), D(70), E(60), F(50), G(40), H(30), I(20), J(10) na K(0).

Alisema lengo la mabadiliko hayo ni kuondoa pengo kutoka kundi moja hadi lingine na kuleta uwiano mzuri katika makundi ya uchangiaji na kuwa sasa mikopo haitatolewa kwa kufuata madaraja ya viwango vya kufaulu vinavyotumika sasa (daraja la kwanza na la pili).

"Kwa sasa utoaji mikopo hautafuata 'division' (daraja), bali utakuwa ukizingatia udahili wa wanafunzi katika vyuo na kwa utaratibu huu, chuo kitapewa idadi ya wanafunzi watakaokopeshwa kulingana na programu zake na idadi itapangwa kulingana na vipaumbele vya taifa, kama itakavyoelekezwa na serikali, ikiwemo elimu na sayansi," alieleza.

Mbwanji alifahamisha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2009/2010, bodi yake itatoa kipaumbele kwa wadahili wote wa sayansi ambapo watapewa mkopo kwa asilimia 100, hii ni kutokana na wanafunzi wa sayansi ambao wamekuwa wakinufaika na mkopo kuwa pungufu ya asilimi 35.

Marekebisho mengine ambayo bodi imefanya ni kuongeza kiwango cha mikopo kwa vitabu na viandikwa (stationary) kutoka sh. 120,000 ya sasa hadi kufikia 200,000 kwa mwaka kwa wanafunzi wote.

"Eneo lingine ni ulipaji wa ada kwa maombi ya mikopo, katika mabadiliko haya itatozwa sh. 30,000 mara moja kwa mwaka wa kwanza, badala ya utaratibu wa nyuma wa kutoza kwa kila mwaka.

Mabadiliko mengine ni utoaji mikopo kwa wahadhiri wa vyuo vya elimu ya juu binafsi, kwa ajili ya kusoma shahada za uzamili na uzamivu. Hawa pia watapewa badala ya wale wa serikali pekee.” alisema.

Akielezea mabadiliko hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, George Nyatega alisema wanafunzi watakaopata mikopo watapaswa kupitishwa na bodi za elimu za kijiji, kata, tarafa na wakuu wa wilaya, ili kuwatambua zaidi na kuepuka udanganyifu kwa waombaji.

Hata hivyo alisema kuwa, utaratibu huo mpya umepelekwa serikalini kwa ajili ya kuthibitishwa na kwamba, utaanza kutumika mwaka huu kwa wadahiliwa wapya na kwamba, waliopo vyuoni sasa wataendelea na utaratibu wa zamani mpaka watakapohitimu masomo yao.

Alisema katika kufanikisha mpango huo mpya, bodi yake inatarajiwa kudahili wanafunzi 60,000 watakaokopeshwa ikiwa ni zaidi ya mwaka jana walipodahili 55,685 na kwamba, mwaka huu wanatarajia kutumia kiasi cha Sh175 bilioni.

Hadi kufikia mwaka jana bodi ilikuwa imekopesha jumla ya sh 62.2 bilioni kwa wanafunzi 56,07. Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosoma nchini ni 23,061, wanoendelea na masomo 32,012 na wanaosoma nje ya nchi ni wanafunzi 998.

Jijini Dar es Salaam, Benjamain Sawe na Zawadi Msalla wanaripoti kuwa, Mkurugenzi wa Usambazaji wa Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu, Lubambula Machunda amewashauri wanafunzi kufuata utaratibu uliowekwa na bodi ya mikopo nchini, ikiwa ni pamoja na kufuta vigezo sahihi vilivyopangwa katika kufuatilia madai na matatizo mbalimbali yanayoshughulikiwa na bodi hiyo.

Alisema bodi imejiandaa kufungua ofisi zake katika kila kanda na kwamba, wataanzia Dodoma na Zanzibar, lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na vyuo.

Alivishukuru vyuo mbalimbali nchini kwa kutoa maofisa wake katika kukusanya matatizo ya wanafunzi, kuhusiana na mikopo na kuyashughulikia kwa utaratibu uliopangwa na bodi hiyo.

Sera mpya ya uchangiaji elimu ya juu, ambayo iliweka mfumo wa kutoa mikopo kufuatana na makundi, imesababisha wanafunzi kugoma kwa madai kuwa unalenga kuwanyima haki watoto wa masikini kupata elimu ya juu na hatimaye vyuo kufungwa.

Wanafunzi hao pia waliitaka serikali itoe mikopo kwa asilimia 100 kwa wanafunzi wote na vitivo vyote, badala ya kutenga makundi ambayo hata hivyo, hayazingatiwi kutokana na baadhi ya watoto wa wenye uwezo kulipiwa zote na wale wa masikini wakiwekwa kwenye makundi ya kuchangia.

Hata hivyo hivi sasa vyuo vikuu vya umma vilivyokuwa vimefungwa, vinaendelea kudahili upya, ingawa hatua hiyo imekuwa ikipingwa na wanafunzi.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar