BAADA ya kuripotiwa sana kwamba angefikishwa mahakamani, hatimaye mbunge wa jimbo la Simanjiro mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka jana alipandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kumshambulia mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) mkoani Arusha, James Ole Milya.
Tangu mapema wiki hii, kumekuwa kukiripotiwa habari kadhaa kuwa Ole Sendeka amepandishwa kizimbani kwa madai ya kufanya kosa hilo, lakini suala lake lilikuwa polisi hadi jana wakati mbunge huyo alipofikishwa kwenye mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Arusha akikabiliwa na shitaka la shambulio la kudhuru mwili.
Sendeka, mmoja wa wabunge machachari, aliwasili mahakamani hapo kwa gari aina ya Land Rover, Defender ya polisi na kupelekwa katika chumba cha mapumziko kabla ya kupandishwa kizimbani.
Mbunge Sendeka alikuwa amesindikizwa na watu wa kada mbalimbali waliosababisha umati mkubwa mahakamani hapo, akiwemo mwenyekiti mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, mbunge wa jimbo la Vunjo, Aloyce Kimaro pamoja na wananchi mbalimbali na wanachama wa CCM kutoka mkoani Manyara na Arusha.
Akisomamewa hati ya mashitaka mahakamani hapo mbele ya hakimu anayesikiliza kesi hiyo, James Kalayamaha, mbunge huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 9 mwaka huu majira ya saa 10:30 wilayani Monduli wakati alipompiga Mallya kibao upande wa shavu la kulia na kumsababishia maumivu mwilini mwake.
Inadaiwa kuwa tukio hilo lilitokea wakati Ole Sendeka pamoja na Mallya wakiwa katika semina ya wazee wa kimila iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Monduli.
Mbunge Sendeka anatetewa na mawakili, Michael Ngalo wa kampuni ya Ngalo and Company yenye ofisi zake jijini Dar es salaam na Arusha akisaidiwa na wakili wa kujitegemea, Neema Mtayangula huku upande wa mashitaka unaongozwa na wakili Hashimu Ngole akisaidiwa na wakili Augustino Kombe.
Akizungumza mahakamani hapo wakili wa upande wa mashitaka, Ngole aliiomba mahakama kuwapa muda wa kukamilisha upelelezi wa keshi hiyo kwa kuwa bado haujakamilika na kuomba mahakama hiyo kuipangia tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Kwa upande wao mawakili wa upande wa mtuhumiwa walimuomba hakimu kumpatia dhamana mteja wao kwa kuwa ni mtu anayefahamika ambaye hawezi kutoroka na ni mbunge ambaye anatakiwa kufanya shughuli zake za kibunge hadi hapo atakapohitajika.
Hakimu aliikubali hoja hiyo kwa masharti ya kudhaminiwa na watu wawili ambao kila mmoja anatakiwa adhamini kwa Sh500,000 na kuhakikisha mtuhumiwa anafika mahakamani pindi atakapohitajika.
Hakimu alikubali na kusema masharti ya dhamana yako wazi na hivyo wadhamini kujitokeza, akiwemo meneja wa Bonite mkoani Arusha, Mwangole Segule ambae alipingwa kuwa mdhamini kutokana na hati yake kukosa muhuri wa uongozi wa kampuni hiyo.
Baadaye, mfanyabishara wa madini ya Tanzanite, Baraka Kanunga alijitokeza badala yake na kuungana na mfanyabiashara mwenzake Joel Sabore Lesirya ambao wote kwa pamoja walifanikiwa kumdhamini mbunge huyo wa Simanjiro.
Wadhamini hao walitakiwa kuhakikisha Ole Sendeka anatinga mahakamani Februari 10 kwenye kesi hiyo ma iwapo kutakuwa na tatizo watapaswa kutoa taarifa mahakamani hapo.
Akizungumza nje ya mahakama, Sendeka aliwashukuru wote waliofika mahakamani hapo na kuwataka kuliacha suala hilo kwenye vyombo vya sheria ili vifanye kazi yake na kuwatahadharisha dhidi ya maneno machafu na kuwatuhumu watu kuhusu suala hilo pamoja na kuacha kufanya maandamamo wakati wanapotoka mahakamani hapo.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar