Waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan, amepokelewa kishujaa nchini mwake akirejea kutoka katika kikao cha dunia kinachojadili masuala ya kiuchumi huko Davos, Uswisi.Hapo jana kiongozi huyo wa Uturuki aliondoka katika kikao hicho baada ya kurushiana maneno makali na rais wa Israel, Shimon Peres, kuhusiana na mzozo wa Gaza.Erdogan aliilaumu Israeli kwa mauaji ya Wapalestina wa Gaza.
Maelfu ya watu walikusanyika mapema hii leo katika uwanja wa ndege wa Ataturk mjini Istanbul Uturuki kumpokea waziri mkuu Erdogan akirudi kutoka Davos Uswisi ambako alizusha sokomoko la hali ya juu.
Waturuki walimiminika katika eneo la uwanja wa ndege wakipeperusha bendera za nchi yao na Palestina huku wakiimba Uturuki tunajivunia kuwa nawe.Hatua hiyo imechukuliwa baada ya hapo jana bwana Erdogan kumshambulia kwa maneno mazito rais Shimon Peres wa Israeli .Wakati wa majadiliano kuhusu suala la mashariki ya kati, rais Peres alianzisha mazungumzo yaliyoonekana kuitetea sana nchi yake kuhusiana na hatua yake ya kuizingira na kuishambulia Gaza wiki kadhaa zilizopita,Peres alizungumza akionyesha hisia kali na kumuonyeshea kidole waziri mkuu Tayyip Erdogan na kumuuliza ni kwanini maroketi yanarushwa dhidi ya Israeli.
Shimon Peres aliongeza kumuuliza Erdogan angefanya nini ikiwa nchi yake ingeshambuliwa kwa maroketi kila usiku.Lakini ukali wa bwana Peres ulimhamakisha waziri mkuu huyo wa Uturuki ambaye alimkatiza na kutaka apewe nafasi ya kuzungumza na kujibu hoja ya rais Peres, lakini muongoza kikao hicho ambaye ni Mmarekani akaonekana kutaka kumzima lakini hilo halikufua dafu kwa waziri mkuu Erdogan ambaye alin'gan'gania kupewa nafasi hiyo na alipopewa uwanja akasema tunamnukuu,
''Sababu inayokufanya bwana Peres kuwa mkali ni kwasababu unajihisi kuwa na hatia,ukweli ni kwamba linapokuja suala la kuua basi nyinyi waisraeli mnaijua sana kazi hiyo''
Baada ya kutoa matamshi hayo moja kwa moja akakurupuka na kuondoka kwenye kikao hicho akisema huenda hatokanyaga tena jukwaa hilo linalofanyika kila mwaka katika mji huo wa kitajiri wa Davos.
Hata hivyo Erdogan akizungumza na waandishi wa habari punde alipowasili nchini mwake alisema Uturuki haina kitu chochote dhidi ya watu wa Israeli au Wayahudi, bali mtazamo wa Uturuki unapinga utawala wa Israeli. Kwa upande mwingine, Waturuki wamekuwa na maoni yanayotofautina kuhusiana na hatua ya waziri mkuu wao, huku baadhi yao wakisema itazidisha mvutano kati ya Israeli na nchi hiyo na huenda ikadhoofisha msimamo wa Ankra kama mpatanishi asiyependelea upande wowote katika suala la mashariki ya kati.
Msemaji wa jukwaa hilo la kiuchumi duniani amethibitisha kwamba Peres na Erdogan walizungumza kwa njia ya simu baada ya sokomoko hilo na kuondoa hasira zao.
Peres alimuomba msamaha Erdogan na kumwambia kuwa marafiki baadhi ya wakati wanakuwa na mvutano na kwamba anamuheshimu pamoja na uturuki.
Wakati huohuo, ripoti ya Davos imesema kwamba dunia huenda ikakabiliwa na ukosefu wa maji kutokana na kuongezeka mahitaji ya bidha hiyo muhimu kabisa.
Akizungumza katika mkutano huo, katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki Moon, alisema tatizo la maji ni kubwa na hivyo panahitajika juhudi nzito za kushughulikia tatizo hilo.Kwa upande mwingine, katika mkutano huo waziri wa mambo ya nje wa Iran alisema nchi yake iko tayari kushirikiana na rais Barack Obama ikiwa Marekani itabadili sera zake na vitendo vyake katika eneo hilo.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar