Tayari serikali imeshawafikisha mahakamani watuhumiwa 21 kwenye sakata la wizi wa jumla ya Sh133 bilioni, mawaziri wawili wa zamani na katibu mkuu wa wizara kwa makosa ya kutumia vibaya ofisi; na jana ilikuwa zamu ya kashfa iliyoitikisa nchi mwaka jana kuhusu utoaji wa zabuni ya ufuaji umeme wa dharura kwa Richmond.
Kashfa hiyo, iliyoingia hadi ndani ya Bunge la Muungano, ilisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu baada ya kuhusishwa na sakata hilo. Baadaye mawaziri wawili wa serikali ya awamu ya nne, Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha, nao waliachia ngazi.
Jana, Gire alipandishwa kizimbani majira ya saa 9:00 alasiri kujibu tuhuma za kueleza uongo kuwa Richmond ina uwezo wa kuzalisha megawati 100 za umeme nchini.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Kisutu, Wariyalwande Lema, Gire alisomewa mashtaka yake na wakili wa serikali, Boniface Stanslaus ambaye alidai kuwa Machi 13 mwaka 2006 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alighushi nyaraka akionyesha kwamba, Mohamed Gire, ambaye ni mwenyekiti wa Richmond Development Company LLC ya Texas nchini Marekani, alisaini kumruhusu Naeem Adam Gire kufanya shughuli za kampuni hiyo hapa nchini.
Katika shtaka la pili, wakili huyo alidai kuwa Machi 20 mwaka 2006 katika eneo la Ubungo Umeme, mshtakiwa alitoa hati za uongo zilizoonyesha kwamba, Mohamed Gire amezisaini kumuidhinisha kufanya shughuli za kampuni hiyo nchini.
Katika shtaka la tatu mshtakiwa huyo anadaiwa kutoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kwamba Kampuni ya Richmond ina uwezo wa kuzalisha megawati 100 za umeme nchini.
Inadaiwa kuwa, mshtakiwa huyo alitoa taarifa hizo ili wajumbe wa bodi hiyo waipendekeze Kampuni ya Richmond kufanya kazi hiyo.
Wakili huyo alidai kuwa, katika shtaka la nne mwezi Juni mwaka 2006, mshtakiwa alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kwamba, Richmond ina uwezo wa kuzalisha megawati 100 za umeme ili wajumbe hao waweze kuipendekeza.
Kwa mujibu wa wakili huyo, mshtakiwa huyo anadaiwa katika shtaka la tano kuwa mwezi Juni mwaka 2006, alitoa nyaraka za kughushi akionyesha kwamba Mohamed Gire amezisaini kumuidhinisha mshtakiwa kufanya shughuli za kampuni hiyo Tanzania.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Wakili anayemtetea mshtakiwa huyo, Kato Zake aliiomba mahakama kutoa masharti nafuu ya dhamana kwa kuwa makosa anayotuhumiwa yanaruhusu kupata dhamana.
"Tunaomba masharti nafuu ya dhamana kwa sababu mshtakiwa wakati wote amekuwa akitoa ushirikiano katika upelelezi na afya yake sio nzuri," alisema Zake. Wakili huyo pia alidai mshtakiwa huyo alikuwa anafuatilia hati yake ya kusafiria kwa ajili ya kwenda kwenye matibabu na kwamba ameshatoa baadhi ya hati zake za nyumba kwa Jeshi la Polisi.
Baada ya kusikiliza hoja zote, Hakimu Lema aliahirisha kesi hiyo hadi leo atakapotoa uamuzi wa dhamana. Akiongea na wahariri mwishoni mwa mwaka jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwatoa hofu wananchi akisema kuwa, tuhuma nyingi za ufisadi zinashughulikiwa na kwamba katika uchunguzi huo mambo mengi mapya yamebainika.
Kufikishwa mahakamani kwa Gire kunathibitisha kauli hiyo ya Pinda na sasa mambo mengi mapya yanasubiriwa katika kashfa hiyo iliyowekwa hadharani na Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa mbunge wa Kyela, Harrison Mwakyembe.
Kashfa hiyo ilitokana na tatizo kubwa la umeme lililoibuka miaka miwili iliyopita, mara baada ya serikali ya awamu ya nne kuingia madarakani. Ukosefu huo wa umeme ulitokana na ukame mkubwa ulioikumba nchi kiasi cha kusababisha serikali kutafuta umeme mbadala badala ya ule unaotengenezwa katika mabwawa ya maji ambayo kwa wakati huo mengi yalikuwa hayana maji ya kutosha.
Kesi ya Gire ni mwendelezo wa harakati za serikali kushughulikia tuhuma za ufisadi. Katika robo ya mwisho ya mwaka jana, serikali iliwapandisha kizimbani watu wanaotuhumiwa kujichotea jumla ya Sh133 bilioni kutoka Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika kipindi cha mwaka 2005/06.
Watu 21 wameshapandishwa kizimbani, akiwemo mfanyabiashara maarufu, Jeetu Patel. Pia waziri wa zamani wa Fedha na Uchumi, Basil Mramba na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kutumia vibaya ofisi zao na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh11 bilioni.
Katika kesi hiyo ameunganishwa Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja kwa makosa kama hayo.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar