Lawrence waziri wa mambo ya ndani Masha sasa ni majaliwa
2009-02-04 17:12:19
Na Mwandishi Wetu, Jijini
Wakati Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ilitarajia kuketi leo kujadili sakata linalomkabili Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Lawrence Masha, kuna taarifa kuwa kibarua cha mheshimiwa huyo kiko mashakani kutokana na baadhi ya wabunge kuandaa nondo kibao za kumtia hatiani kiongozi huyo.
Nondo hizo inadaiwa zina ushahidi kadhaa unaobainisha kuwa Mheshimiwa Masha alitaka kuibeba kampuni moja ili ipate tenda ya kutengeneza vitambulisho vya taifa, mradi utakaogharimu takribani shilingi bilioni 200 za Kitanzania.
Chanzo kimoja cha gazeti hili kimedai kuwa kikundi hicho cha wabunge waliokomalia sakata hilo, kimeapa kuwa kitaendelea kulivalia njuga sakata hilo hadi Mhe. Masha aachie ngazi ama kwa kujiuzulu au kwa kuwajibishwa na Rais Jakaya Kikwete aliyemteua.
Habari zaidi zinadai kuwa miongoni mwa wabunge hao, yumo Dk. Wilbroad Slaa wa Jimbo la Karatu (CHADEMA).
Vyombo vya habari mbalimbali vimesema kuwa, Dk. Slaa tayari ameandaa hoja binafsi kwa ajili ya kuwasilisha Bungeni akitaka sakata hilo lijadiliwe kwa kina na uamuzi kutolewa.
Habari zaidi zinasema hoja ilishatua kwa Spika wa Bunge ambaye aliipeleka kwenye kamati hiyo ya mambo ya nje, ambayo inaketi leo.
Imeelezwa kuwa Waziri Masha na Dk. Slaa wameitwa kwenye kamati hiyo ambapo kila mmoja atatoa hoja zake.
Alasiri ilipojaribu kuwasiliana na Dk. Slaa kupata maelezo yake kuhusiana na sakata hilo alisema, ingawa ameitwa kwenye kamati hiyo, hadhanii kuwa atasitisha dhamira yake ya kuwasilisha hoja hiyo bungeni.
Amesema anachofahamu yeye ni kwamba,kamati hiyo haina uwezo wa kuzuia hoja, isipokuwa inao uwezo wa kuichelewesha endapo itakuwa haijakamilisha uchunguzi wake.
``Kwa mujibu wa mamlaka ya bunge, kamati haina uwezo wa kuzuia hoja, isipokuwa inaweza kuchelewesha tu endapo itasema haijakamilisha uchunguzi wake,`` Dk. Slaa aliliambia gazeti hili.
Ameongeza kuwa endapo atahisi kuwa inafanyika mbinu yoyote ya kumnyamazisha au kuzuia hoja yake, wahusika wa suala hilo wataumbuka zaidi kwa sababu mahakama kuu ya suala hilo itakuwa ni umma wa Watanzania.
Wakati tukienda mitamboni, kamati ya mambo ya nje ambayo mwenyekiti wake ni Mbunge wa Muleba Kaskazini, Mhe. Wilson Masilingi, ilitarajiwa kukutana na kujadili suala hilo.
Hivi karibuni, Mhe. Masha alidaiwa kuingilia mchakato wa mradi wa vitambulisho vya taifa, jambo ambalo Dk. Slaa aliliibua bungeni Alhamisi iliyopita wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu, Mhe.Mizengo Pinda.
Hata hivyo, Spika aliingilia kati suala hilo na kumtaka Slaa, kama ana hoja ya msingi kuhusiana na suala hilo, basi aiwasilishe ili ijadiliwe.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar