2009-02-06 16:12:53
Operesheni ya kuondoa magari madogo ya abiria yanayofika katikati ya Jiji la Dar almaarufu kama vipanya imeanza kwa kasi ambapo hadi kufikia jana, jumla ya daladala zaidi ya 100 za aina hiyo zimekamatwa na kutakiwa kusitisha huduma zake kuelekea kwenye maeneo hayo.
Ofisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), katika Kanda ya Mashariki na Pwani, Bw. Walukani Luhamba, ameliambia Alasiri kuwa operesheni hiyo ilianza jana na kwamba tayari magari zaidi ya 100 yameshatimuliwa.
Akafafanua kuwa operesheni hiyo ambayo itadumu kwa muda wa wiki mbili, inatokana na mpango wa SUMATRA wa kuyaondoa magari yote madogo yaendayo katikati ya Jiji, lengo mojawapo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari.
Akasema daladala zinazoruhusiwa kutoa huduma hizo ni zile zenye uwezo wa kubeba abiria 26 na kuendelea na kwamba daladala hizo za aina ya vipanya, zinatakiwa kuhudumia katika maeneo ya pembezoni mwa Jiji.
``Vipanya vingi havina leseni kwa sababu leseni zao zimeshaisha muda wake na hawa hawataki kuja kukata leseni nyingine, hali inayowafanya kufanya biashara kwa kuibia tu,`` akasema.
Akasema zoezi hilo linaendeshwa na kitengo cha usalama wa barabarani cha Polisi kwa kushirikiana na kikosi cha farasi cha FFU na maofisa wa SUMATRA.
Akabainisha kuwa daladala lolote litakalokamatwa kwa kosa la kufanya biashara huku likiwa halina leseni za usafirishaji, litalazimika kulipa faini ya Sh. 250,000.
Akasema baada ya kulipa faini hiyo, wamiliki wanatakiwa kuchagua njia wanayotaka kuhudumia ambayo ni lazima iwe ya permbezoni na kisha kwenda moja kwa moja Mamlaka ya Ufundi (VETA), kupigwa mistari inayoonyesha barabara watakazohudumia.
Alipoulizwa kuhusiana na daladala zinazoweza kuziba pengo la usafiri katika maeneo hayo, akasema wamekuwa wakisajili daladala zaidi ya nane kila siku katika maeneo hayo.
``Wakazi wa Jiji hawana haja ya kuhofia kuhusiana na shida ya usafiri kwa sababu kutakuwa na daladala kubwa nyingi zitakazotoa huduma hiyo katika maeneo ya katikati ya Jiji,`` akasema Bw. Luhamba.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar