MKURUGENZI Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka matatu, likiwamo la matumizi mabaya ya ofisi, na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni 221.
Mbele ya Hakimu, Hadija Msongo, Liyumba na Maneja Miradi wa benki hiyo, Deogratias Kweka, walipandishwa kizimbani jana Jumanne wakituhumiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh 221, 197, 299, 200.95 katika ujenzi wa majengo pacha ya BoT.
Amatus Liyumba
Watuhumiwa wote wawili ambao walipelekwa rumande kutokana na kukosekana muda wa kuhakiki masharti ya dhamana, walikana mashitaka hayo ambayo yalisomwa na waendesha mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Mashitaka mawili ya kwanza yanamkabili Liyumba pekee, ambaye alidaiwa mahakamani hapo kwamba kati ya mwaka 2001 na 2006 akiwa Mkurugenzi wa Utawala wa BoT, alitumia vibaya madaraka kwa kuchukua maamuzi mazito ya upanuzi wa majengo ya BoT bila kibali cha Bodi ya Wakurugenzi.
Majengo Pacha ya BoT
Liyumba pia kwa kufanya maamuzi mazito ya upanuzi wa mradi wa ujenzi wa majengo pacha bila idhini ya Bodi aanadaiwa alikiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2002 na taratibu za utendaji za ndani ya BoT.
Yeye na Kweka, wanaunganishwa katika shitaka la tatu wanalodaiwa kuwa wameisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 153,077,715.71 sawa na Sh. 221,197,299,200.95 kwa kushindwa kuwajibika kwa nafasi zao kwa kuipotosha Bodi ya BoT, ambayo iliidhinisha malipo hayo.
Hakimu Msongo alitoa nafasi ya washitakiwa wote wawili kudhaminiwa lakini kutokana na muda kuwa haukutosha wadhamini wao walishindwa kutimiza masharti, baada ya upande wa mashitaka kutaka hati na nyaraka nyingine kuhakikiwa kwanza kabla ya mahakama kuzipokea.
Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, Hakimu Msongo alisema kutokana na kubanwa na muda, ingekuwa vigumu kwa taratibu za uhakiki kufanyika jioni ya jana Jumanne, ikiwa tayari ilikwisha kukaribia saa 10.00 Alasiri. Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Februari 10, mwaka huu.
Kwa kufikishwa mahakamani jana, Liyumba na Kweka sasa wanaungana na watumishi wengine wa BoT waliokwisha kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, hususan waliohusika katika kuidhinisha utoaji wa mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).
Hao ni Mkuu wa Idara ya Madeni, Imani Mwakosya; Kaimu Mkurugenzi Idara ya Madeni, Ester Komu; Kaimu Mwanasheria wa BoT, Bosco Kimela na Mwanasheria wa benki hiyo, Sofia Joseph.
Wote wanne walikwisha kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kusutu wakikabiliwa na jumla ya mashitaka matano, kuhusu Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Maofisa hao walifikishwa mbele ya Mahakimu wawili tofauti, Hakimu Mkazi Hezron Mwankenja na Hakimu Mkazi Warialwande Lema kwa tuhuma za kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, wizi na kujipatia ingizo isivyo halali na kuisabanishia Serikali hasara ya Sh. bilioni 4.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar