Minggu, 15 Februari 2009

MAWAZIRI WAMEGUSHI VYETI....

KASHFA ya kughushi vyeti vya taaluma mbalimbali imeendelea kulitafuna taifa, baada ya kubainika uwepo wa mawaziri wanne wanaodaiwa kughushi vyeti vya elimu ya juu.
Kugundulika kwa mawaziri hao kunatokana na kuwapo kwa taarifa kuwa baadhi ya wasomi nchini wamepata taaluma hizo kupitia kwenye vyuo visivyotambulika kimataifa, hivyo elimu yao kutokuwa halali.
Aidha, kuna kundi linalodaiwa kughushi vyeti vya vyuo mbalimbali vya nje ambavyo havina umaarufu au sifa zinazotambulika kimataifa.
Miongoni mwa wasomi ambao wamo katika kundi la mawaziri ni wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, ambao wamepata shahada za falsafa (PhD) lakini zimebainika kupatikana kupitia katika tovuti mbalimbali za vyuo hivyo visivyo na sifa.
Kutokana na wahadhiri wao kutopata elimu hiyo kwenye vyuo vinavyotambulika, uongozi wa chuo hicho pamoja na Kamisheni ya Vyuo Vikuu vya Elimu ya Juu (TCU) imewataka wale wote waliopata elimu katika vyuo hivyo kusomea upya shahada zao katika vyuo vinavyotambulika kimataifa.
Habari ambazo zimeifikia Tanzania Daima Jumapili, zinadai kuwa mawaziri hao wanne (majina tumeyahifadhi), ambao ni madaktari wa fani mbalimbali hadi sasa hawajaweza kusomea upya shahada zao kama walivyoshauriwa na vyombo vya kitaaluma.
Hadi sasa mawaziri hao wamekuwa wakihaha kuhakikisha kuwa utata wa elimu yao hauwekwi hadharani ili kulinda heshima yao waliyojijengea ndani na nje ya nchi.
“Kuna mawaziri wanne ambao taaluma zao zina utata, hasa kutokana na wengine kughushi na wengine kusoma katika vyuo visivyotambulika kimataifa, uchunguzi wa walikozipata taaluma zao unaendelea,” kilidokeza chanzo chetu cha habari.
Mmoja wa mawaziri hao siku za hivi karibuni amekuwa akionekana zaidi katika vyombo vya habari, kwa msimamo wake wa kuitetea nchi ili isiingie katika mikataba na makubaliano na nchi nyingine bila kufanya tathmini ya kina.
Waziri mwingine anayedaiwa kuwemo kwenye mkumbo huo aliwahi kuingia katika malumbano na vyombo vya habari kutokana na kumuandika kuwa anatetea ufisadi, pamoja na kuwemo kwenye kundi la wanamtandao.
Kutokana na sakata hilo, mawaziri hao huenda wakalazimishwa kuachia nyadhifa walizonazo ndani na nje ya chama au kufukuzwa, iwapo suala lao litavaliwa njuga na viongozi wao au wananchi.
Kashfa hiyo ya mawaziri kughushi vyeti imekuja huku Baraza la Mitihani la Taifa NECTA likiandamwa kwa shutuma za uvujaji wa mitihani pamoja na uuzaji wa vyeti vya elimu ya sekondari.
Matukio ya kughushi vyeti yamekuwa yakiongezeka kila kukicha hapa nchini, jambo linalohatarisha mustakabali wa taifa katika nyanja ya elimu, hasa katika zama hizi za utandawazi, ambapo nchi kadhaa zimekuwa zikielekeza nguvu zaidi katika sekta ya elimu ili ziweze kuwa na wataalamu watakaozisaidia kuandaa mipango ya maendeleo.
Mmoja wa wabunge aliyewahi kukumbwa na kashfa ya kughushi vyeti vya elimu ya juu ni Ali Ramadhani Kihiyo, wa Jimbo la Temeke (CCM), ambaye alifunguliwa kesi na Chama cha NCCR-Mageuzi iliyosimamiwa na mwanasheria wake maarufu wakati huo, Masumbuko Lamwai.
Mbunge huyo alilazimika kuachia wadhifa huo baada ya kubainika kuwa hakuwa na elimu hiyo kama vyeti vyake vilivyokuwa vikionyesha na hatimaye kuachia ngazi na kuitishwa uchaguzi mwingine.
Mbali ya Kihiyo, Mbunge wa Buchosa, Samwel Chitalilo (CCM), amekumbwa na tuhuma za kughushi vyeti, lakini hadi sasa anaendelea na ubunge, licha ya kuwapo kwa kelele za baadhi ya watu wakimtaka aachie ngazi kutokana na kashfa hiyo.

from http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=2438

Tidak ada komentar:

Posting Komentar