Rabu, 04 Februari 2009

ZANZIBAR ISITEGEMEE UPENDELEO KAMA ILIVYO KISIASA


Maximo amshukia Waziri wa Michezo

KOCHA wa Taifa Stars, Marcio Maximo amejibu tuhuma za Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mahmoud Thabit Kombo wa Zanzibar kwamba amekuwa akibagua visiwa hivyo katika suala la kufanya ziara ya kusaka vipaji kwa kuwa zaidi upande wa Tanzania Bara.

Akizungumza jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Maximo ameiambia Mwananchi kwamba wasitegemee suala la upendeleo maalum kutoka kwa kikosi chake kupitia suala la Ubara na Uzanzibar kwa kuwa Stars si timu ya kisiasa.

�Sipendi taifa Stars iingie katika masuala ya siasa, pia sifurahii kuona viongozi wanazungumza mambo bila kuyafanyia utafiti kitu ambacho kinaweza kufanya uchinganishi na chuki ndani ya timu yetu. Sipendi watu wenye lengo la kutuvuruga.

�Yoyote yule asitegemee kuwa na upendeleo fulani kutoka katika kikosi changu, Zanzibar waache lawama na moja kwa moja waboreshe ligi yao kwanza. Inahitaji kuwa imara ili iweze kutoa wachezaji wa uhakika. Wana vipaji vingi na nimeenda Zanzibar mara kadhaa na kushuhudia hilo,� alisema Maximo akionyesha kukerwa na kushangazwa na kauli hiyo ya Kombo.

�Zanzibar ina mikoa mingapi, tuliweke hili wazi,� alihoji. �Huku bara iko mingapi, mbona sijasikia Iringa wanalalamika sijaenda, kuna mikoa mingi tu. Suala la kwamba kuna wachezaji wengi kutoka bara nalo pia si kitu cha kuzungumza namna hiyo kwa kuwa tuna wachezaji kutoka Zanzibar.

�Hata siku moja sijawahi kusikia watu wanaulaumu kwamba Taifa Stars ina wachezaji wengi kutoka Mwanza na Mbeya. Wanaijumlisha na kusema Tanzania Bara tu, sioni kama wana sababu ya msingi na ningependa wajue naangalia ubora kuteua timu yangu.

�Sipendi nichague wachezaji eti kwa kuwa leo ninao wengi kutoka Mwanza na Mbeya basi niwapunguze na kuangalia wengine kutoka mikoa mingine. Au lazima walingane idadi na wale wa Zanzibar, huu ni mpira.

�Kama nimekosea nakubali kukosolewa kwa lengo la kujenga, lakini kama ni vingine basi ni vema tukatumia busara zaidi na kutofautisha soka na mambo ya siasa,� alisema Maximo akionyesha kujiamini.

Kombo alisema hayo katika baraza la wawakilishi la Zanzibar na kusisitiza watampeleka Maximo visiwani humo kwa gharama zao ingawa alikuwa amesahau kwamba kocha huyo amefanya ziara visiwani humo mara mbili kwa ajili ya kusaka vipaji, huku Tanzania Bara akiwa amefanya katika baadhi tu ya mikoa.

Mwakilishi huyo pia alilaumu TFF kutowagawia fedha kutoka Fifa, kitu ambacho Katibu Mkuu, Frederick Mwakalebela alifafanua kwamba, shirikisho hilo halileti fedha nchini kwa ajili ya kuzigawa na badala yake kutekeleza majukumu ya maendeleo ya soka nchini ikiwamo Zanzibar.

Kikosi cha Maximo kina wachezaji watatu kutoka Zanzibar ambao ni Nadir Haroub �Cannavaro�, Farouk Ramadhani, Abdi Kassim �Babi� pamoja na kocha msaidizi Ally Bushir ambaye Maximo amefanya naye kazi kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Mara kadhaa, Zanzibar imekuwa ikilalama kutopewa ushirikiano na TFF ingawa kila kukicha imekuwa ikiendelea na juhudi za kutaka kujitenga na kuomba uanachama kwa Fifa huku ikigonga mwamba kila mara.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar