Kamis, 19 Februari 2009

NAO WAJA TZ KUSOMA?

Waswaziland waja Tanzania kujifunza mfumo mpya NSSF

VIONGOZI waandamizi 11 kutoka nchi ya Swaziland umewasili nchini jana, kwa lengo la kujifunza namna ya kubadilisha mfumo wa malipo ya mkupuo unaotumika nchini humo kupitia mfuko wa Penshieni wa nchi hiyo (Swaziland National Provident Fund) na kuingia katika mfumo mpya wa malipo ya awamu unaotumika nchini.

Msafara huo unaongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Shirika la Akiba ya Uzeeni nchini Swaziland (SNPF), Prince Lonkhokhela Dlamini upo nchini kwa ziara vya siku tatu za mafunzo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF nchini, Dk Ramadhan Dau, alisema wajumbe hao watajifunza jinsi ya kuachana na mfumo wa zamani na jinsi ya kuingia mfumo mpya ambao unaotumika kwa mafanikio nchini.

“Kwa sasa nchi nyingi za Afrika bado zinatumia mfumo wa zamani ambao hauna faida kwa jamii, hali ambayo inazifanya nchi nyingi kubadilika na kuiga mfumo mpya baada ya kuona mafanikio ya mfumo huo nchini,” alisema Dau

Dau, aliwataja wajumbe wengine waliopo katika msafara huo kuwa ni Meneja Mkuu wa shirika hilo, Miccah Nkabinde, Naibu Kamishna Wizara ya Kazi na Ustawi wa Jamii, E.L.B Dlumini, na kutoka shirikisho la wafanyakazi nchini humo wapo, Vicent Ncongwane na Alex Fakundze.

Wengine ni Mwenyekiti wa bodi Muungano wa wafanyakazi nchini humo, Mdududzi C. Gina, mbunge wa Bunge la nchi hiyo, Henry Dlamini na maofisa wakuu kutoka vyama vya wafanyakazi, Jumuiya ya wafanyakazi na waajiri, ambao ni Jobe Mashwama, Bongani Mtshali, Tums du-Pont na Samuel Shongwe.

Dau, alisema wajumbe hao, jana walikutana na Waziri wa Ajira, Kazi na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya, lakini pia watakutana na viongozi mbalimbali wa vyama vya wafanyakazi na waajiri nchini kwa dhumuni la kujifunza masuala hayo.

“Kutokana na mabadiliko tuliyoyapata kupitia mabadiliko ya mfumo huo, miaka ya hivi karibuni NSSF imekuwa ikipigiwa chapuo katika nchi za Afrika na kufanya wageni mbalimbali kutoka nchi zao kuja kujifunza namna ya kuendesha mifuko ya jamii na baadhi ya nchi zilizowahi kuleta wajumbe wake kwa lengo la kujifunza ni Ghana, Msumbiji, Sierra Leone, Kenye na Gambia,” alisema Dau

Naye, Mwenyekiti wa Bodi Muungano wa Wafanyakazi nchini humo, Mdududzi C. Gina, alisema wapo nchini kwa mafunzo hayo kwa kuwa tanzania ni moja ya nchi zilizobadilisha mfumo ambao unatumika nchini kwao na kuwa na mfumo mpya ambao umeonyesha mafanikio hivyo nao kuvutiwa na kutaka kuingia katika mfumo huo.

“Tumefurahishwa na mapokezi ya ugeni wetu na tumekuja Tanzania kwa mafunzo kwa kuwa ni moja ya nchi ambazo zimebadilisha mfumo wao kutoka mfumo wa mkupuo hadi mfumo mpya wa malipo ya awamu, ambayo nasi tunataka kuyatumia nchini kwetu Swaziland kwa ajili ya mafanikio ya wananchi wetu,” alisema Gina

Tidak ada komentar:

Posting Komentar