Senin, 09 Maret 2009

BUNGE LA MWAKA 2010 KUWAKA MOTO....WAGOMBEA URAIS WOTE ISIPOKUWA LIPUMBA KUWANIA UBUNGE..

KUNA uwezekano mkubwa kwamba Rais Jakaya Kikwete akapata mgombea mpya kutoka kambi ya upinzani baada ya kuwapo taarifa za wagombe waliojitokeza uchaguzi uliopita kuamua kuwania ubunge na kubadilika kwa upepo wa kisiasa nchini.

Hali hiyo imeelezwa kuchochewa na hali ya kisiasa duniani ambako sasa wapiga kura wameonekana kutamani kuwa na wagombea mbadala kutoka wale waliozoeleka katika nyanja za kisiasa.

Kutokana na hali hiyo viongozi kadhaa wa vyama vya siasa waliogombea urais katika chaguzi zilizopita wametajwa sasa kuamua kuwania ubunge majimboni kwa kile wanachokisema ni kujaribu kupata viti vingi bungeni.

Kwa sasa kuna taarifa za uwezekano wa kutokea wagombea wapya katika ngazi ya urais kutoka vyama vya upinzani na huenda hata wakaweza kutokea ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Ndani ya CCM kumekuwapo na mpasuko wa wazi wazi ambao umesababisha hata kuibuka kwa malumbano miongoni mwa viongozi wa kisiasa, hali inayoelezwa kuchochea kuibuka kwa kundi litakaloamua kuweka mgombe urais kukabiliana na Kikwete.

Wiki iliyopita, mmoja wa viongozi hao ambaye amegonbea urais tangu mwaka 1995 na kushindwa, Augustine Mrema wa Tanzania Labour Party (TLP) aliviambia baadhi ya vyombo vya habati kwamba alikuwa ameitika wito wa kumtaka akagombee katika Jimbo lake la zamani la Vunjo, Kilimanjaro.

Mwingine, mgombea urais wa mwaka 2005, Freeman Mbowe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amekuwa akitajwa kuwa atakwenda kugombea ubunge katika Jimbo la Hai, Kilimanjaro, jimbo alilopata kuwa mbunge wake.

Habari za ndani ya CHADEMA zinasema kwenda kwa Mbowe Hai ni sehemu ya mkakati wa chama hicho wa kutaka kujizolea majimbo mengi ambayo sasa yanaonekana yana utata wa ugombea na ikiwezekana, kwa wingi huo, kuunda serikali, hata kama hakitakuwa na kiongozi katika ngazi ya urais.

Habari zinasema pia kwamba mwingine ambaye angeweza kuwania urais kutokana na nafasi yake ya uenyekiti wa chama, James Mbatia Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, anataja kwenda katika Jimbo la Kawe ambako Mbunge wa sasa, Rita Mlaki upepo umamvumia vibaya hata ndani ya chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mwaka 2005, NCCR- Mageuzi kilimsimamisha Dk. Sengondo Mvungi, mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye kwa matokeo mabaya aliyopata mwaka huo, mazingira hayampi nafasi kubwa ya kuwania tena urais kupitia chama hicho.

Kujitoa katika kinyang’anyiro hicho cha urais mwakani kwa Mrema, Mbowe, Mbatia na ukweli kwamba Mwenyekiti mwingine wa chama cha upinzani ambaye angeweza kujitupa ulingoni, John ‘Bwana Mapesa’ Cheyo wa United Democratic Party (UDP) alikwisha kuona muda mrefu busara ya kwenda bungeni, kunamfanya mgombea pekee anayesalia kutoka wapinzani waliogombea mwaka 2005 kuwa Profesa Ibrahim Lipumba.

Wiki hii Profesa Lipumba alifanya mahojiano maalumu na Raia Mwema, kuhusu pamoja na mambo mengine, kama atawania urais mwakani, majibu yake hayakuonyesha kuwa hatasimama.

Tidak ada komentar:

Posting Komentar