Wana wa Nyerere na Amin kukutana Butiama | ||||||||||
Kuanzia Alhamisi ya tarehe 9 mwezi Aprili, Idhaa ya Kiswahili ya BBC itakuwa ikikuletea taarifa za historia kwa kuwakutanisha watoto wa viongozi wa nchi mbili za Afrika Mashariki ambao uhasama wao ulishuhudia vita kali mwishoni mwa miaka ya sabini - vita vya Kagera. Katika tukio la kipekee litakalosimamiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Jaffer Remo Amin, mwana wa kiume wa Idi Amin aliyekuwa rais wa Uganda, na Madaraka Nyerere, mwana wa kiume wa Mwalimu Julius Nyerere “Baba wa Taifa”, wamekubaliana kukutana kwa mara ya kwanza kabisa. Ifikapo tarehe 10 Aprili, itakuwa imetimia miaka 30 tangu kung’olewa madarakani kwa Idi Amin wa Uganda, kutokana na mapambano makali, majeshi ya Tanzania chini ya rais wa wakati huo Mwalimu Julius Nyerere yakikamilisha kazi hiyo. Uhusiano baina ya viongozi hao haukuwa mzuri kwa muda, mnamo Oktoba 1978 hali ilizidi kuwa mbaya wakati Idi Amin alipoishambulia Tanzania na kujitangazia kuumega mkoa wa Kagera ulioko kaskazini-magharibi mwa Tanzania. Hatimaye, kiongozi huyo wa Uganda alilazimika kukimbilia uhamishoni, akianzia Libya na baadaye Saudi Arabia ambako aliishi maisha yake yote yaliyobakia kabla ya kuaga dunia Agosti 2003. Matangazo BBC itawashirikisha wachambuzi hodari wa maswala ya kisiasa kutathmini athari zilizotokana na vita hivyo kwa nchi za Afrika Mashariki na bara zima la Afrika. Mada muhimu kwa muda wote wa matangazo yetu itakuwa kukutana kwa wana wa viongozi hao wawili, waliotawala katika siasa za eneo hilo. Arua mpaka Butiama
Kila hatua ya safari ya Jaffer, mwenye umri wa miaka 42, itanaswa na mwandishi Idd Seif wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, atakayesafiri naye mpaka kwenye makutano. Butiama Kwa kipindi chote cha msafara wa Amin kuelekea Butiama, BBC itarusha taarifa kuhusu mwitikio wa wananchi wakizungumzia mkutano huo wa watoto wa viongozi wa pande zilizokuwa zikihasimiana. Mratibu wa mpango huo, Caroline Karobia, tayari amekuwa akifanya mahojiano na watu waliokuwepo nyakati hizo za miaka ya sabini. Anasema: "Haijawahi kutokea Afrika Mashariki, kabla au baada kuona mapambano makali kama yale kwa majeshi ya nchi mbili, na miaka 30 baadaye kumbukumbu bado ni dhahiri miongoni mwa watu walioshuhudia vita. Idhaa ya Kiswahili ya BBC itarekodi kumbu kumbu hizi na pia kualika wasikilizaji wetu kutupia macho yatakayofuata siku za usoni." Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Solomon Mugera, anaongeza: "Idi Amin and Julius Nyerere walikuwa maadui wakubwa. Tofauti zao ziligubika siasa za eneo zima kwa kipindi chote cha miaka ya sabini. Uongozi wao ulikuwa na athari kubwa kwa raia wao, na hiba isiyosahaulika. Katika kuchambua athari za vita kwa Tanzania, Uganda na eneo zima la Afrika Mashariki, Idhaa ya Kiswahili ya BBC imeratibu mkutano wa wana wa kiume wa mahasimu hao wawili. Tunatarajia kunasa kila lililo muhimu katika safari yao ya kihistoria." Je una maoni yoyote kuhusu swala hili au vita vya Kagera kwa ujumla? Tuandikie barua pepe kupitia assenga@gmail.com |
Minggu, 29 Maret 2009
mtoto wa Idd Amin Bw Jaffar Amin................................ Mtoto wa Nyerere Bw Madaraka Nyerere
Langganan:
Posting Komentar (Atom)
Tidak ada komentar:
Posting Komentar