RAIS Mstaafu wa serikali ya awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, jana alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya mtu asiyejulikana kumfuata jukwaani wakati akihutubia na kumpiga kibao shavuni.
Mwinyi, ambaye alipata umaarufu wakati serikali yake ilipolegeza masharti ya kiuchumi na kisiasa hadi kuruhusu mfumo wa vyama vingi na kusababisha apachikwe jina la Mzee Ruksa,
alishambuliwa na mtu huyo jana majira ya saa 12:20 jioni wakati alipokuwa akihutubia Baraza la Maulid kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) lililohudhuriwa na waumini wengi wa dini ya Kiislamu kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee.
Shambulizi hilo lilitokea wakati Mwinyi akizungumzia masuala ya afya na hasa malezi bora ya wazazi kwa watoto na kusisitiza matumizi ya kinga wakati wa ngono, akimaanisha kondomu na ndipo alipojitokeza mmoja wa waumini aliyekuwa amevalia kanzu.
Mtu huyo alijifanya kama anataka kumsalimia Kaimu Mufti, Sheikh Suleyman Gorogosi.
Kwa kuwa imezoeleka katika shughuli za kidini kutawaliwa na amani, watu waliokuwa karibu na mtu huyo hawakuwa na shaka naye ndipo mtu huyo akarudisha mkono ghafla na kumpiga kibao Mzee Mwinyi.
"Sisi tulishangaa kuona yule jamaa akipanda jukwaani na kujifanya kama anasalimiana na Mufti. Lakini cha kushangaza tukaona akageuka na kumpiga kibao Mzee Mwinyi... sisi tulishikwa butwaa," alisema Hussein Kauli mmoja ya watu waliohudhuria sherehe hizo.
Baada ya tukio hilo, Kaimu Mufti wa Tanzania, Alhaj Suleyman Gorogosi alimuomba radhi rais huyo wa awamu ya pili akisema kwamba kijana aliyefanya tukio hilo ni mtu mwenye upungufu wa akili.
Akaongezea kwamba kijana huyo huwa anaonekana katika shughuli mbalimbali za kidini na huwa anashiriki, lakini matukio yake yote mara nyingi yamekuwa ni ya kipunguani.
Naye sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa alitumia fursa hiyo kumuomba radhi mzee Mwinyi akisema kuwa kitendo hicho kimemsikitisha kila Muislamu na kwamba hakikutarajiwa.
"Ni fedheha kubwa imetupata kwa mtu kumkabili mtu tunayemheshimu na tena mwenye hadhi kubwa namna hii katika jamii haipendezi. Tunahisi suala hili limepangwa na kundi la watu wenye malengo yao kwa sababu kijana yule asingeweza kujiamini kiasi kile. Ana kundi kubwa linamuunga mkono," alisema Sheikh Mussa baada ya kutoka ndani ya ukumbi.
Hata hivyo, Sheikh Mussa hakueleza ni kundi gani analihisi kuwa liliandaa mpango huo wa kumshambulia rais mstaafu, ambaye amekuwa akihudhuria hafla nyingi za Kiislamu.
Alisema kuwa anamfahamu kijana huyo kwa sura lakini hatambui jina lake kwani amekuwa akishiriki katika shughuli mbalimbali za kidini na mara zote hizo amekuwa akifanya mambo ya kipunguani.
Hata hivyo muda mfupi baadaye askari polisi wakishirikiana na walinzi wa Mzee Mwinyi walimbeba mtuhumiwa huyo na kumuadhibu na baadaye kumpeleka kituo cha polisi.
Baadaye, Mzee Mwinyi aliendelea na mawaidha yake akisisitiza masuala mbalimbali, likiwemo la Waislamu kutunza afya zao na kujikinga na ugonjwa wa Ukimwi ambao umeleta madhara makubwa katika jamii.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar